Tuesday, January 4, 2011

Werema anachakujifunza juu ya kauli ya Kikwete


Jaji Frederick Werema
                                                       
Na Joachim Mushi

DESEMBA 31, 2010 wakati, Rais Jakaya Kikwete akitoa salamu za mwaka mpya yaani 2011 kwa Watanzania alitamka kuanza kwa mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya kama ilivyo kuwa ikililiwa na baadhi ya wananchi, viongozi na wanaharakati.

Kwa mujibu wa hotuba aliyoitoa, anasema ameamua kuunda tume maalumu itakayoratibu mchakato mzima wa awali. Tume hiyo itakayojulikana kama 'Constitutional Review Commission' anasema itaongozwa na mwanasheria aliyebobea.

Anaendelea kusema kuwa tume itasheheni wajumbe wanaowakilisha makundi mbalimbali katika jamii yetu kutoka pande zetu mbili za Muungano, yaani Tanzania Bara na kule Visiwani ili kupata maoni ya pande zote zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kikwete katika taarifa yake anaendelea kubainisha kuwa jukumu kubwa la tume hiyo itakuwa ni kuongoza na kuratibu mchakato utakaowashirikisha wananchi wote vikiwemo vyama vya siasa, wanasiasa, wafanyabiashara, asasi za kiraia, mashirika ya dini, wanataaluma na makundi anuai ya watu, katika kutoa maoni yao.

Anasema kitakachofuata baada ya tume hiyo kukamilisha kazi ya kukusanya maoni, ni tume kutoa mapendekezo yatakayofikishwa kwenye vyombo stahiki vya Kikatiba kwa lengo la kufanyiwa kazi na hatimaye maamuzi sahihi.

Hata hivyo anaenda mbali zaidi kwa kutamka kuwa lengo la kuanza mchakato wa kuandikwa kwa Katiba mpya ni kuiwezesha nchi kuwa na Katiba inayoendana na taifa lenye umri wa nusu karne, na kwamba mchakato huo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Anasema; "....mwaka 2011, nchi yetu inatimiza miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, miaka 47 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar na miaka 47 ya Muungano wa nchi zetu mbili. Yapo mabadiliko mengi yaliyotokea katika nyanja mbalimbali za maisha ya nchi yetu na watu wake katika kipindi hiki. Kwa ajili hiyo ni vyema kuwa na Katiba inayoendana na mabadiliko…" 

Kimsingi anachokisema Rais Kikwete juu ya Katiba ya nchi ni jambo jema. Amesoma alama za nyakati na kuona kuna kila sababu suala hili liwashirikishe wengi kuelekea mchakato wa mabadiliko. Hii ni busara ya namna ya kipekee.

Lakini hofu yangu ni kwa watu ambao Rais anaowategemea kiushauri kuwa tofauti naye tena hasa kwa mambo ambayo wao ndiyo wataalamu kwenye fani hiyo. Eneo hili nataka kumzungumzia mshauri mkuu wa masuala ya sheria wa Serikali, yaani Mwanasheria Mkuu, Jaji Frederick Werema.

Pamoja na kazi nyingine za mtaalamu huyu wa sheria wa Serikali ni kuishauri vizuri tena kitaalamu Serikali juu ya masuala mbalimbali yanayozigusa sheria. Kikawaida huwezi kuzitenganisha sheria zetu na Katiba ya nchi, vitu hivi hutegemeana.

Katiba ni mama wa sheria zote. Katiba inapokuwa imepitwa na wakati hata sheria nyingi zitakuwa vivyo hivyo. Nazo zitakuwa zimepitwa na wakati kiasi ambacho utekelezaji wa uamuzi wake utakuwa na utata.

Kwa wale wafuatiliaji wa mambo wanatambua fika Katiba tunayoitumia kwa sasa ilikotoka. Hatuwezi kumshangaa mtu anayesema kuwa Katiba hiyo imepitwa na wakati.

Ni jambo la kushangaza kuona wanaoijua vizuri Katiba yetu, kama Jaji Werema wanashindwa kuwa wawazi na hata kutumia taaluma yao kuishauri Serikali kuelekea katika mabadiliko yenye tija kwa taifa zima. Mabadiliko ambayo hayata kuwa na migogoro ya bila sababu.

Ukweli ni kwamba Rais Kikwete amesoma alama za nyakati kuna jambo kalibaini kwa anaowaongoza ndiyo maana ameridhia kuanza kwa mchakato wa mabadiliko ya Katiba, wasaidizi wake wajifunze kwa hili kwani wameteuliwa kufanya kazi kulingana na taaluma zao na si vinginevyo.


No comments:

Post a Comment

SEIF SHARIFF HAMAD AKIRI KUWA YEYE NI BABU KIZEE.

Seif Shariff Hamad Seif Shariff Hamad KWA mara ya kwanza Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Seif Shariff Hamad amek...