WATUMISHI wa umma 4,788 wako hatarini kufukuzwa kazi endapo utetezi wao kuhusu kushindwa kuwasilisha tamko la mali zao, hautakubalika.
Watumishi hao ambao ni kati ya viongozi 8,410 wa umma na siasa waliotakiwa kuwasilisha tamko la mali zao kabla ya Desemba 31 mwaka jana, watatakiwa kuwasilisha utetezi huo kwa Baraza la Maadili la Sekretarieti ya Viongozi wa Umma.
Kamishina wa Sekretarieti ya Maadili ya Umma, Jaji Salome Kaganda aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa hadi Desemba 31 mwaka 2010, viongozi 4788, walikuwa hawajatoa tamko hilo.
Jaji Kaganda alisema viongozi hao sasa wataandikiwa barua zinazowataka watoe sababu zilizowafanya kushindwa kutekeleza amri hiyo ya kisheria kabla baraza halijaanza kuchukua hatua dhidi yao.
"Kama maelezo yao hayataridhisha, viongozi husika wataitwa mbele ya Baraza la Maadili, ambalo litawasikiliza na kutoa mapendekezo kwa kamishna wa maadili juu ya hatua zinazofaa kuchukuliwa dhidi yao," alisema jaji Kaganda.
Aliongeza “Taarifa ya baraza itawasilishwa kwa Rais na nakala yake kupelekwa kwa Spika kwa hatua zaidi za kiutumishi na kiutawala.” Kufungu cha 8 (d) cha Sheria namba 13 ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1995, kimetaka kiongozi asiyetoa tamko la mali afukuzwe kazi.
"Masharti katika sehemu hii yatakuwa ni sehemu ya maadili ya viongozi wa umma kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ukiukwaji wa maadili utasababisha kuchukuliwa kwa hatua…,” inasema sehemu ya sheria hiyo.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, adhabu zinazotolewa kwa wanaokiuka kifungu hicho ni pamoja na kuonywa na kupewa tahadhari, kushushwa cheo, kusimamishwa kazi, kufukuzwa kazi, kumshauri kiongozi kujiuzulu wadhifa unaohusu ukiukwaji huo, kupewa adhabu nyingine zinazoruhusiwa kwa mujibu wa sheria za nidhamu kuhusu wadhifa wa kuiongozi na kuhimiza kuchukuliwa hatua kwa kiongozi kwa mujibu wa sheria za nchi zilizopo.
Jaji Kaganda alisema katika taarifa yake kuwa kati ya viongozi wa umma 4064 waliopewa fomu hizo, ni viongozi 2324 tu ndio waliozirejesha huku viongozi wengine 1741 wakikwepa kutekeleza agizo hilo la kisheria.
Taarifa imeeleza pia kuwa kati ya viongozi wa 4346 wa siasa wanaoanzia ngazi ya madiwani hadi Rais, waliopewa fomu hizo, viongozi waliozirejesha ni 1446 na viongozi 3047 hawakurejesha.
“Mwitikio kwa viongozi wa siasa unaweza kutafsiriwa kuwa ni mdogo kwa sababu kundi hili linabebwa kwa kiasi kikubwa na waheshimiwa madiwani, ambao taratibu za uteuzi na uundwaji wa mabaraza ya halimashauri nyingi mchakato wake ulikuwa bado hauajakamilika,” ilisema sehemu ya tarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo hadi kufikia Desemba 31 mwaka jana, madiwani 1,032 kati ya 3,876 ambao ni asilimia 26.62 ya madiwani wote nchini, walikuwa wamerejesha fomu hizo za tamko.
“Hii inamaanisha kuwa jumla ya madiwani 2,844 sawa na asilimia 73.37 hawakuweza kuzirejesha…, Hali hii inabainisha kuwa ni viongozi waandamizi wa siasa 56 sawa na asilimia 11.9 ya viongozi waandamizi 470 hawakurejesha fomu za tamko kwa wakati ukiondoa madiwani,” iliendelea kueleza taarifa hiyo.
Kwa upande wa viongozi wa umma wasiokuwa wanasiasa, Mahakimu ndio wanaoongoza kwa kutorejesha fomu hizo.
Taarifa imeeleza kuwa mahakimu ambao wanakadiriwa kufikia 1,631, sawa na asilimia 40.13, hawakurejesha fomu hizo kutokana jiografia ngumu ya mawasiliano. “Hii inamaanisha kuwa ukiondoa kada ya mahakimu, ni viongozi 109 waandamizi wa utumishi wa umma kati ya 2,433 ndio ambao hawakuwasilisha fomu zao kwa wakati.
Hii ni asilimia 4.48,” taarifa hiyo iliendelea. Alipotakiwa kueleza utaratibu unaotumiwa na tume hiyo kujiridhisha matamko ya viongozi hao, Jaji Kaganda, alisema “Tuna vijana wetu hapa, kama tukipokea malalamiko ama sisi tukiwa na wasiwasi, tunawatuma kwenda kuchunguza na kupata ukweli halisi.”
Alifafanua mwaka 2005 sekretarieti hiyo ilipokea malalamiko 78, mwaka 2006 malalamiko 222 na mwaka 2010 malalamiko 69 na kuyafanyia kazi.
Na Fredy Azzah wa Gazeti la Mwananchi.
No comments:
Post a Comment