Wednesday, January 19, 2011

Mchungaji adaiwa kukutwa na marehemu watatu

Tarehe: 19th January 2011

WANANCHI wa kijiji cha Nyankanga, Musoma Vijijini, mkoani Mara wamevamia kwa Mchungaji Paulo Magesa wa kitongoji cha Iginaimwe na kuchoma nyumba zake tatu na kuharibu bustani yake kwa tuhuma za ushirikina.

Tukio hilo lilitokea Januari 16 saa 3 asubuhi, wakati Mchungaji huyo alipokutwa akiwa na vijana watatu wa kijiji hicho ambao wanasadikiwa walishafariki dunia miaka mingi iliyopita.

Waandishi wa habari walifika eneo la tukio na kujionea uharibifu mkubwa uliofanywa na wananchi hao, lakini mtuhumiwa na familia yake hawakuwapo, kwa madai kuwa walitorokea kusikojulikana.

Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho, walidai kuwa Mchungaji huyo alikuwa anatoa huduma za kiroho kwa familia yake pekee alifika kijijini hapo takribani mwaka mmoja na nusu uliopita na kununua eneo la ekari zaidi ya 10 kutoka kwa Marwa Kitamara.

“Aliuziwa eneo hilo, lakini kitu cha kushangaza baada ya kuhamia vifo vya ajabu ajabu vilianza kutokea, lakini siku ya tukio alikutwa akiwa na watu waliokufa siku nyingi, kuna kijana wa Bweri na mama aitwaye Mama Asha, na mwingine hawakumfahamu jina.

“Ndipo vijana hao wakapiga yowe na kumhoji kuwa alikuwa anawapeleka wapi na wakati wakiendelea kumhoji watu hao walitoweka kusikojulikana ndipo wananchi walipopandwa hasira na kwenda kuchoma na kubomoa nyumba zake tatu na kuharibu bustani na shamba lake,” alisema Mamkama Imanyi wa Iginaimwe.

Wananchi hao walidai kuwa ilipofika saa 12 jioni aliokotwa kijana anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 14 karibu na eneo la Mchungaji huyo akidaiwa ni msukule na baada ya kumhoji anatoka wapi alitaja zaidi ya vijiji vitano na jina lake halijui, ndipo wakamkabidhi kwa polisi wa doria na kupelekwa kituo kikuu cha Polisi mjini hapa.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Masau Magalu, alikiri kupokea malalamiko ya wananchi kuwa Mchungaji huyo alikuwa anajihusisha na mambo ya kishirikina lakini Serikali haiamini mambo ya uchawi ingawa walikuwa wanaendelea na uchunguzi wa kubaini ukweli wa jambo hilo.

“Tulishapata malalamiko kutoka kwa wananchi wetu, lakini sisi Serikali hatuamini mambo ya kishirikina, ingawa tulikuwa tunafuatilia malalamiko na jana (juzi) wananchi walimvamia kwa madai kuwa alikutwa na watu watatu akiwapeleka mjini, ndipo wakachoma na kubomoa nyumba zake tatu na kuharibu mashamba yake na sasa hatujui aliko,” alisema Magalu.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Robert Boaz, alisema: “Habari za kuchomewa na kubomolewa nyumba zake na kuharibiwa mashamba tumezipata, lakini cha kushangaza Mchungaji wa Kanisa atawezaje kuwa mchawi.

“Pia kijana ambaye wananchi wanadai kuwa ni msukule si kweli, kijana yule alikuwa amepotea njia lakini kwa kuwa alikuwa mazingira hayo, wananchi wakamhusisha na tukio hilo, lakini ameshachukuliwa na wazazi wake,” alisema Kamanda Boaz.

Kamanda aliongeza kuwa wanafanya uchunguzi wa kina kubaini wananchi waliohusika na uharibifu huo, ili sheria ichukue mkondo wake kwa kuwafikisha mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Taarifa zilizopatikana kutoka kwa baadhi ya wananchi wa kijiji hicho na mjini hapa zilisema matukio ya kuchomewa nyumba Mchungaji huyo yametokea mara nyingi kwani hata katika maeneo ya Majita, Musoma Vijijini, alichomewa nyumba na kufukuzwa kwa tuhuma hizo hizo za ushirikina.

Alihamia mjini Musoma na mwaka juzi aliripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari baada ya kuchomewa nyumba katika kitongoji cha Zanzibar karibu na Mlima Balima akidai kuwa alikuwa anafanya utafiti wa madini huku akijihusisha pia na masuala hayo
hayo. ……………..
                                                         Na Thomas Dominick, wa Habari Leo Musoma;

No comments:

Post a Comment

SEIF SHARIFF HAMAD AKIRI KUWA YEYE NI BABU KIZEE.

Seif Shariff Hamad Seif Shariff Hamad KWA mara ya kwanza Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Seif Shariff Hamad amek...