Friday, January 7, 2011

Ni kweli Majembe walishindwa kazi?

Na Joachim Mushi

HIVI karibuni Waziri wa Uchukuzi aliipa maelekezo Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa nchi Kavu na Majini (SUMATRA) kuhakikisha inavunja mkataba na kampuni ya udalali ya Majembu wa kufanya shughuli kwa niaba yao.

Majembe awali waliingia mkataba kufanya kazi za SUMATRA ikiwa ni pamoja na kufuatilia na kuhakikisha sheria mbalimbali za usafirisaji zinafuatwa kwa wadau wa usafirishaji. Wameifanya kazi hiyo jijini Dar es Salaam kwa muda na yapo mabadiliko tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Awali SUMATRA walikuwa wakifanya kazi hiyo wenyewe kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi yaani Kikosi cha Usalama Barabarani. Kikosi cha SUMATRA kilichokuwa kinafanya kazi hizo kwa jiji la Dar es Salaam ni kidogo hivyo ilikuwa ni vigumu kuendesha oparesheni maeneo yote na kufanikiwa.

Baadhi ya viongozi wa mamlaka hiyo na wafanyakazi mara kadhaa walikiri kuwa kutokana na idadi ndogo ya wafanyakazi wao walikuwa wakishindwa kuthibiti kila eneo, hasa kwa jiji moja la Dar es Salaam na kufanikiwa.

Malalamiko ya ukiukwaji wa sheria za usafirishaji yalipozidi kutoka kwa abiria, mara kadhaa mamlaka ilikiri upungufu wa watendaji hao. Kimsingi siwezi kujua ni kwanini mamlaka muhimu kama hii inakuwa na upungufu mkubwa kiutendaji kiasi hicho.

Hata hivyo pamoja na mambo mengine baadhi ya kazi zao zimekuwa pia zikifanywa na kikosi cha usalama barabarani yaani trafiki polisi. Hawa wamekuwa wakijitahidi kadri ya uwezo wao lakini hali bado ni mbaya. Sheria kwa jiji la Dar es Salaam zinavunjwa kupindukia.

Mbali na kuvunjwa ndani ya Jiji la Dar es Salaam, pia zimekuwa zikivunjwa sana na wasafirishaji wa abiria kwa mabasi yanayofanywa safari zake mikoani. Tena wahusika wanazivunja bila uwoga wowote, sijui wanapata wapi ujasiri wa kufanya hivyo.

Na kibaya zaidi kwa wadau wa usafirishaji ndani ya jiji na hata kwa mabasi ya mikoani wamekuwa wakivunja sheria hizo hata mbele ya trafiki bila woga. Wajua kwanini wanafanya hivyo? Ukweli ni kwamba wamezoeana na baadhi ya matrafiki ambao ni waangalizi wa usalama wa vyombo hivyo na sheria nyingine.

Tena wapuuzi wachache wanapovunja kwa makusudi sheria hizo hutoa 'kitu kidogo' kwa baadhi ya askari na kisha kuendelea na safari. Kwa daladala za jiji hii ndio kazi yao kubwa. Na kwa mabasi yanayosafirisha abiria kwenda mikoani kwa baadhi ya njia hii ndio kazi yao.
Yapo mabasi yanayofanya safari zake Dar es Salaam na Morogoro hayaogopi kabisa kuvunja sheria wawapo safarini, baadhi ya mabasi yameamua kutembea na viti vidogo vya mbao ambavyo huvitumia kuvipanga katikati ya basi na kujaza abiria kupita kiasi.

Utaona askari anaingia ndani ya mabasi hayo na kushuhudia upuuzi huo lakini hakuna anachokifanya zaidi ya kufanya mazungumzo na dereva au kondakta na baadae gari huendelea na safari. Hali hii hufanywa maeneo yote njiani kwenye vituo vya trafiki. Binafsi mdau 'Madamoto' sitaki kujua askari wetu hupewa nini hadi kushindwa kuzuia upuuzi huu.

Mabasi yanayofanya safari za Tanga na Dar es Salaam nayo yamechonga viti vidogo maalumu kama vigoda kwa ajili ya kuzidisha abiria wanapokuwa safarini. Magari haya hupita na kukaguliwa na baadhi ya askari wa usalama barabarani, lakini hufubwa macho. Hawaoni hatari hiyo ya kuzidisha abiria.

Suala la mikanda sasa halifuatiliwi tena. Yapo mabasi yanayofanya safari kwenda mikoani viti vingi havina mikanda tena, na vilivyo na mikanda vingi haifanyi kazi (mibovu) hakuna askari wanaohoji kwanini abiria hawafungi mikanda hiyo. Natumai kinachosubiriwa ni kutokea kwa ajali ndipo tujipange.

Sasa nirudi kwenye mada yangu ya kuondolewa kwa Majembe. Ukweli ni kwamba kwa jiji la Dar es Salaam wavunjaji wakuu wa sheria za barabarani yaani daladala hushindwa kuwahonga Majembe, hii ni kutokana watu hawa hutembea kwa makundi.
 Wakati mwingine kundi moja hutembea hata na zaidi ya watu nane.
Kundi hili dereva wa daladala hawawezi kuwahonga hawa. Na hata wakifanya hivyo fedha wanayotoa ni nyingi tofauti na wanavyofanya kwa tarafiki mmoja. Kimsingi uwepo wa kampuni ya Majembe kwa daladala ni kilio. Wanajua ili kukwepa hasara hiyo hulazimika kufuata sheria kiasi kikubwa.

Uzoefu unaonesha kwa askari wa barabarani kwa kuwa huwa mmoja mmoja hutoa mpaka kiasi cha shilingi 2,000 kwa kosa jambo ambalo sio hasara kwa kazi yao. Ndio maana hawawataki Majembe kuendelea kufanya kazi hiyo, kwani wamekuwa wakibanwa sawasawa. Wamekuwa wakiomba mungu majembe kuondolewa muda mrefu tena kwa visingizio vingi.

Wanataka polisi ndiyo wafanye kazi hiyo ili waendelee kufanya wanavyotaka. Huu ndio ukweli halisi, hivyo kuondolewa kwa Majembe ni kicheko kwao.
Kwa mawasiliano tembelea; joemushi.blogsport.com uache ujumbe au barua pepe; jomushi79@yahoo.com na Simu: 0717030066, 0756469470, 0786030066.  

  

No comments:

Post a Comment

SEIF SHARIFF HAMAD AKIRI KUWA YEYE NI BABU KIZEE.

Seif Shariff Hamad Seif Shariff Hamad KWA mara ya kwanza Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Seif Shariff Hamad amek...