Friday, January 14, 2011

Pengo: Sikutarajia Polisi Kuua Raia


Pengo: Sikutarajia Polisi Kuua Raia
 

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo amesema
kitendo cha polisi waliopewa dhamana ya kulinda wananchi kuua watu wasio na hatia kinaashiria maafa makubwa kutokea nchini.

Akihutubia waumini wa Kanisa Katoliki wa Jimbo la Dar es Salaam katika misa ya kuwaombea wafiadini wa Pugu iliyofanyika Kituo cha Hija, Pugu juzi, Kardinali Pengo alisema hakutarajia jambo hilo linaweza kutokea Tanzania bara, ambako kuna historia ya kuitwa kisiwa cha amani duniani.

"Sikutegemea hata mara moja kwamba walinda usalama wanaweza kutumia silaha wakaua watu. Sikutegemea kwamba wanaweza kuua hata mtu mmoja. Wale wanapaswa kutetea uhai wa Watanzania. Wachukue silaha dhidi ya Watanzania, waue watu haidhuru wamekosaje, ni jambo ambalo sikutegemea kamwe kwamba lingeweza kutokea," alisema kardinali Pengo.

Kutokana na tukio hilo kiongozi huyo aliwataka Watanzania bila kujali madhehebu yao wasimpuuze Mungu, bali warejee kumuomba ili arejeshe amani Tanzania iliyoachwa na waasisi wa nchi hii, Mwalumu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume.

Kardinali Pengo alisema tukio la polisi kuua raia lililotokea Arusha kwa wananchi wasio na hatia kupigwa risasi liimetia doa Tanzania, limeipaka matope Tanzania.

Kiongozi huyo aliwataka Watanzania watambue kuwa hana lengo la kueneza hisia za chuki, woga wala hisia za aina yoyote, bali lengo lake kuwafanya watu watambue kwamba kama tumeishi kwa amani ni mwenyezi aliyetuopa amani hiyo.

"Tutambue kwamba tulipoitwa kisiwa cha amani ilitokana na waasisi wa taifa letu kujenga misingi ya amani, kama tukidhani ilitokana na nguvu yoyote ya kibinadamu tutakuwa tunajidanganya," alisema.

"Kitendo cha watu kutegemea nguvu ya silaha wakifiriki kwamba njia hiyo ndiyo italeta amani au wataweza kuleta ushindi wao, huko ni kujidanyanganya na kumtukana Mungu, kwa vile hayo ni maandalizi ya maafa makubwa kwa ajili ya taifa la Tanzania," alisema na kuongeza Mwenyezi atuepushie na laana hiyo..

Kutokana na hali hiyo iliyosababisha watu watatu kuuawa kwa risasi na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa, Kardinali pengo aliwataka Watanzania waungane naye kuomba ili laana inayonyemelea Tanzania kutokana kwa kumpuuza Mungu iepukwe.

Habari na Gazeti la Majira

No comments:

Post a Comment

SEIF SHARIFF HAMAD AKIRI KUWA YEYE NI BABU KIZEE.

Seif Shariff Hamad Seif Shariff Hamad KWA mara ya kwanza Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Seif Shariff Hamad amek...