Wednesday, March 29, 2017

RC Simiyu amaliza mgogoro wa wanakijiji na wawekezajiMkuu wa Mkoa wa Simiiyu, Anthony Mtaka akifungua kikao cha usuluhishi baina ya mwekezaji wa Mwiba Holdings na wadau wa maendeleo mkoani Simiyu kilichofanyika mwishoni mwa wiki.Na Mwandishi Wetu, Meatu

MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amefanikiwa kumaliza mgogoro wa muda mrefu kati ya mwekezaji katika Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) Makao iliyopo wilayani Meatu, na baadhi ya vijiji vinavyounda jumuiya hiyo. Mwekezaji huyo Mwiba Holdings, amekuwa na mgogoro wa mipaka, mkataba wa kumiliki ardhi na uanzishaji wa ranchi na baadhi ya vijiji hivyo kiasi cha kusababisha kuwa na mahusiano mabaya na wananchi ambao wamekuwa wakisusia  misaada mbalimbali inayotolewa na mwekezaji huyo.

Hata hivyo, chanzo halisi cha mgogoro huo kimegundulika kuwa ni viongozi wa baadhi ya vijiji ambao wamekuwa wakipigania maslahi yao binafsi huku wakisambaza taarifa za upotoshaji juu ya mwekezaji huyo na kujenga chuki kwa wananchi. Vijiji vinavyounda WMA ya Makao ni pamoja na Makao, Iramba ndogo, Sapa, Mwangudo, Jinamo, Lukale, Mbushi, Mwabagimu na Sunga.

Baadhi ya viongozi hao wa vijiji pia wamekuwa wakisambaza taarifa potofu kwa wananchi kwamba Mkuu huyo wa mkoa na mkuu wa wilaya ya Meatu wamehongwa na mwekezaji ili kuwakandamiza wananchi, jambo lililothibitika kuwa si la kweli. Kutokana na mgogoro huo kuzidi kuota mizizi huku uongozi wa CCM Mkoa wa Simiyu nao ukichukua upande, Mtaka alilazimika kuitisha kikao cha usuluhishi

kilichoshirikisha wadau wote wakiwamo Kamati ya Siasa ya CCM mkoa na wilaya, viongozi na watendaji wa serikali ngazi ya mkoa na wilaya, viongozi wa vijiji tisa vinavyounda WMA Makao, mwekezaji na wadau wengine akiwamo Mbunge wa Meatu na Mwakilishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika mwishoni mwa wiki mjini hapa, Mtaka  aliwakemea viongozi wanaoeneza taarifa potofu wilayani humo na kusababisha shughuli za maendeleo kukwama huku akiahidi kuwachukulia hatua zinazostahili viongozi wa namna hiyo.

“Katika  masuala ya maendeleo ya wananchi sina mzaha. Nipo tayari kuwa kiongozi unpopular (asiyependwa) ili mradi shughuli za maendeleo za wananchi zinaenda mbele.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu, Dk Titus Kamani akizungumza katika kikao cha  suluhishi baina ya wananchi wa Meatu na Mwekezaji wa Mwiba Holdings 
kilichofanyika mjini Mwanhuzi mwishoni mwa wiaki.

“Mgogoro na Mwiba umekuwa kama mkuki mnaojichoma wenyewe kila siku kwa sababu wenyewe ndiyo mlioingia mikataba na mwekezaji wakati sisi hatukuwapo na wala hatuna maslahi yoyote binafsi hivyo acheni maneno maneno, kaeni chini mzungumze tusonge mbele,” alisisitiza Mkuu huyo wa mkoa.

“Mmefikisha malalamiko, tena kwa maandishi hadi kwa Waziri Mkuu lakini uhalisia ni kuwa mengi mliyopeleka hayana ukweli, ni hisia na mengine ni fitna tu. Sasa wekeni kila kitu hadharani hapa, tumalize suala hili leo na tujikite zaidi katika mambo ya maendeleo,” alisema.

Kuhusu mgogoro wa mpaka hasa katika kijiji cha Buhongoja ambako alama ya mpaka yenye namba 314 inadaiwa kusogezwa kinyemela kwa umbali wa kilomita 10, Mkuu huyo wa mkoa alizitaka pande zinazohusika kukutana na kutatua tatizo hilo kwa kurejea katika eneo la awali bila ya mikwaruzano yoyote. Aliamuru pia pande

zinazohusika katika suala la mkataba wa umiliki wa ardhi,kukaa meza moja na kuacha mambo ya kukimbilia kwa wasuluhishi ambao wamekuwa wakidai fedha nyingi ambazo zingeweza kutumika kwa maendeleo ya vijiji au wilaya ya Meatu.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini aliahidi kupeleka wataalam watatu watakaosaidiana kutatua mgogoro huo wa umiliki wa ardhi watakaosaidiana na wake wa wilaya ili kutatua suala hilo ndani ya wiki mbili.

Awali, Mwenyekiti wa Kijiji cha Makao, Anthony Phillipo alieleza kuwa kijiji kilazimika kupelaka suala hilo kwenye Tume ya Usuluhishi wa Migogoro Dar es Salaam ambako kijiji walishindwa kulipa gharama za usuluhishi huo walizotozwa na Jaji Mstaafu Thomas Mihayo. Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu, Dk. Titus Kamani alieleza chama hicho tawala kusikitishwa na mgogoro huo unaokwamisha shughuli za maendeleo ya wananchi na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama hicho.

“Ndugu zangu, sisi tunajiandaa kushinda katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, kwa hiyo tunawaomba tusikubali kuingizwa katika migogoro kama hii ambayo haina tija kwa wananchi.

“Tunataka wakati wa uchaguzi utakapofika tushinde pila pressure (msukumo) yoyote na tunachotaka ni mshikamano,maelewano mazuri baina ya wadau wote ili tufanye shughuli za maendeleo kwa faida ya mkoa wetu wa Simiyu na wilaya ya Meatu,” alisisitiza.

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Mpina Luhaga ambaye pia ni mbunge wa Kisesa wilayani Meatu alisema katikA kikao hicho kuwa mwekezaji huyo amekuwa akifuata sheria zote za nchi katika utekelezaji wa majukumu yake na ni wazi kwamba wananchi watashindwa katika madai yote wanayofungua katika Tume ya Usuluhishi wa migogoro.

“Mimi nimefuatilia malalamiko haya ya wananchi serikalini na hasa Wizara ya Maliasili na Utalii na hawa jamaa wamefuata taratibu zote na wanalipa tozo zote wanazostahili kulipa hivyo tunapaswa kuwa waangalifu,” alisema.

Mkurugenzi wa Mwiba Holdings, Abdulkadir Mohamed Luta alisema kuwa Kampuni hiyo ipo tayari kukaa meza moja na kusaidia usuluhishi wa mgogoro wowote ili wajikite zaidi katika shughuli za maendeleo ya wananchi. Aliongeza kwamba kampuni hiyo ilikuwa tayari kugharamia hata suala la mkataba wa umiliki wa ardhi lililofikishwa Tume ya Usuluhishi wa Migogoro ili mradi tu suala hilo liishe na waendelee na mambo ya maendeleo.

Alisema watazifanyia kazi hoja zote zilizotolewa na wananchi katika kikao hicho na kwamba sera ya kampuni hiyo ni kushirikiana na wananchi na wamekuwa wakitekeleza sera hiyo kwa vitendo.

Mbunge wa Meatu, Salum Khamis maarufu kwa jina la Mbuzi, alisema kuwa hana mgogoro na mwekezaji yoyote lakini hatakaa kimya kutetea maslahi ya wananchi wake ambao ndio waajiri wake kila atakapoona kuna sababu ya kufanya hivyo.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Pius Machungwa aliahidi kuipatia kiwanja cha kujenga ofisi Kampuni ya Mwiba Holdings katika makao Makuu ya wilaya hiyo ili iwe karibu na wananchi, na kwamba watashirikiana na kampuni hiyo katika shughuli za maendeleo wilayani humo.

Harusi ya Mwanahabari George Binagi iliyofanyika Mwanza

Jana March 26,2017 ilikuwa siku muhimu kwa mwanahabari wa 102.5 Lake Fm Mwanza na mwanablogu wa BMG, George Binagi wa Tarime Mara pamoja na Miss Upendo Kisaka wa Moshi Kilimanjaro baada ya kuuaga ukapela.

Wapendanao hao walifunga pingu za maisha katika Kanisa la EAGT Lumala Mpya Jijini Mwanza na baadaye hafla kufanyika Ukumbi wa Sun City Hotel, Ghana Green View Jijini Mwanza.

"Ahsanteni nyote mliotusaidia kutimiza ndoto yetu kubwa katika maishani yetu. Familia yangu, ndugu, jamaa na marafiki zangu. Waumini wote wa Kanisa la EAGT Lumala Mpya Jijini Mwanza chini ya Mchungaji Daniel Kulola na kila mmoja kwa nafasi yake, Mungu awabariki. 

Mmenionesha upendo wa ajabu mno.
Wazazi wangu hususani mama mpendwa, nimetimiza deni mliloniachia duniani, hakika sasa mtapumzika kwa amani, pahali pema, peponi, Amina. Ndoa na iheshimiwe na watu wote, Mungu atuongoze vyema". Mr & Mrs George Binagi.

Shukurani za pekee pia ziwaendelee best man na best lady, Mr and Mrs, Joel Maduka kutoka Storm Fm Geita na Maduka Online kwa kufanikisha shughuli hiyo kwenda vyema.

BMG inakusihi uendelee kutazama picha za awali za shughuli hiyo wakati wataalamu wetu wakiendelea kukuandalia picha nyingine ikiwemo picha za kanisani.


Saturday, February 4, 2017

Sheria Ngowi kuteka soko la fashion nchini, Afunguka zaidi maisha yake

Sio kila unachosoma ndio ndoto yako ya baadae, unaweza ukasoma Udaktari au Sheria lakini pia ukawa na kipaji cha zaidi ya ulichosomea na kujikuta unavutiwa kukitumia kipaji hicho kwa ajili ya jamii inayokuzunguka.

The Beauty TV ilizungumza mambo mengi na Sheria Ngowi na unaweza kumtazama hapa na usisahau ku-subscribe kwa ajili ya taarifa zaidi kutoka The Beauty TV.

Tuesday, January 31, 2017

Wabunge wa uzazi salama wataka bajeti ya afya ya uzazi na mtoto kuboreshwa

Mwenyekiti wa Kundi la Wabunge wa Uzazi Salama Mh. Jenista Mhagama (katikati) akifungua mkutano kati ya Muungano wa Utepe Mweupe (WRATZ) na Wabunge wa uzazi salama.


Meneja Mradi wa Muungano wa Utepe Mweupe (WRATZ), Bi. Sizarina Hamisi (mbele) akiwasilisha mada katika mkutano kati ya WRATZ na kundi la Wabunge wa uzazi salama mjini Dodoma.


Mkutano kati ya Muungano wa Utepe Mweupe (WRATZ) na Wabunge wa uzazi salama ukiendelea.

WABUNGE wa kundi la uzazi salama wametakiwa kuhamasisha na kutetea Bajeti ya Afya ya Uzazi na Mtoto ili ipewe kipaumbele katika mipango ya Halmashauri kwa mwaka 2017/2018. 

Hamasa hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kundi la Wabunge wa Uzazi Salama, Mh. Jenista Mhagama wakati akifungua mkutano uliowakutanisha wabunge wa kundi hilo wapatao 30 pamoja na Muungano wa Utepe Mweupe wa Uzazi Salama (WRATZ) mjini Dodoma kujadili kuhusu mchango wa wabunge katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.

 Akiwasilisha mada katika mkutano huo Meneja mradi wa Muungano wa Utepe mweupe (WRATZ) Bi Sizarina Hamisi alisema kwa mujibu wa takwimu ya Idadi ya Watu na Afya Tanzania ya mwaka 2015-2016 zinaonyesha kuwa kwa sasa wakina mama 30 na watoto wachanga 180 wanapoteza maisha kila siku kutokana na matatizo yatokanayo na uzazi. 

Kwa upande wao baadhi ya wabunge wamekiri kuwa pamoja na jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali bado vifo vya mama na mtoto vitokanavyo na uzazi ni changamoto hivyo kuna haja yakuongeza jitihada ili kutatua tatizo hilo ikiwemo bajeti ya afya ya mama na mtoto hasa huduma za muhimu na dharura kupewa kipaumbele kuanzia ngazi za halmashauri mpaka serikali kuu.

Viongozi Wanawake Watakiwa Kuwaandaa Viongozi Bora wa Baadaye...

Kamishna Mkuu wa TGGA, Symphorosa Hangi, akimpongeza Anna Abdalah


Na Richard Mwaikenda


MJUMBE wa Bodi mpya ya Tanzania Girl Guides Association (TGGA), Anna Abdalah, amewataka viongozi Wanawake kukutana na Wasichana kuwapiga msasa wa kuwaaandaa kuwa viongozi bora wa baadaye. Anna Abdalah ambaye amekuwa kiongozi wa muda mrefu nchini, aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Bodi mpya ya TGGA, Mikocheni Dar es Salaam juzi.

Alisema ana mpango wa kuwaalika viongozi mbalimbali Wanawake akiwemo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan akutane na Wasichana wanachama wa TGGA wawafundishe maadili ya uongozi kwa lengo la kuwaandaa kuwa viongozi bora wa baadaye.

Anna Abdalla alisema kuwa hata yeye na Zakia Meghji pamoja na baadhi ya viongozi wengine wanawake walioshika nyadhifa mbalimbali nchini, enzi za usichana wao walipitia kwenye chama hicho na kulelewa vizuri.

Pia katika kikao kijacho cha Bunge, anatarajia kukutana na Wabunge Wanawake na kuwaeleza umuhimu wamara kwa mara kukutana na wasichana kuwafundisha kwa kuwapa hamasa uongozi ili nao wawe kuwa wabunge na hata miongoni mwao kuwa Spika na mawaziri.

"Nataka siku za usoni,tuwaalike viongozi mbalimbali akiwemo, Samia Suluhu Hassan, Naibu Spika wa Bunge, Wabunge na Mawaziri Wanawake ili mje mjumuike nao pamoja, mjifunze mambo mbalimbali ya uongozi na mhamasike, ili siku moja nanyi mje kuwa kama, Samia, Kamishna, Spika wa Bunge, Wabunge na hata uwaziri pia" alisema Anna Abdalah, huku akipigia makofi na waalikwa katika hafla hiyo.

Katika hafla hiyo ambayo mgeni rasmi alikuwa Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufaa, Engera Kileo, ilihudhuriwa na wanachama wa chama hicho, wakiwemo pia wasichana watatu waliotoka Rwanda, Uganda na Madagasca waliokuwepo nchini katika mafunzo ya uongozi, maadili na utamaduni. Wasichana hao ni; Michelline Uwiringiyimana (Rwanda), Recheal Baganyire (Uganda) na Andriambolamanana Vahatrimama.


Kamishna Mkuu wa TGGA, Symphorosa Hangi, aliwataja Wajumbe wa Bodi hiyo kuwa ni; Zakia Meghji, Anna Abdalah, Grace Makenya, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema na Mke wa Waziri Mkuu mstaafu, Tunu Pinda. Mwenyekiti wa Bodi hiyo atateuliwa miongoni mwao.
Mwenyekiti wa Taifa wa Tanzania Girl Guides Association (TGGA), Profesa Martha Qorro (kushoto), akimpongeza Mjumbe wa Bodi ya Udhamini wa TGGA, Anna Abdalah wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bodi hiyo, Mikocheni Dar es Salaam juzi. 
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya TGGA, Sophia Mjema (aliyekaa kulia) akiwa katika picha ya pamoja na wanachama wa TGGA wakati wa hafla hiyo. Aliyekaa kushoto ni Mariamu Kimbisa ambaye ni Kamishna wa Kimataifa wa TGGA. Wa tatu kulia waliosimama ni Kamishna Mkuu wa TGGA, Hangi.
Wasichana Michelline Uwiringiyimana (Rwanda), kulia, Recheal Baganyire (Uganda), katikati, na Andriambolamanana Vahatrimama wa Madagascar ambao wapo nchini katika programu ya mafunzo ya kubadilishana uzoefu katika masuala ya utamaduni, uongozi na maadili.wakiwa katika hafla hiyo.
Wakipiga makofu baada ya kufurahishwa na hotuba ya Anna Abdalah

Anna Abdalah akihutubia katika hafla hiyo
Mmoja wa wabia wa moja kati ya majengo ya TGGA, akisalimiana na Anna Abdalah
Katibu wa Taifa wa TGGA, Grace Shebe akitoa shukrani kwa wajumbe wapya wa bodi na wageni waalikwa kwa kuhudhuria uzinduzi huo.
Wajumbe wa Bodi wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa TGGA pamoja na wanachama wa chama hicho.
Sasa ni wakati wa msosi
Wajumbe wa Bodi wakijadiliana jambo na watendaji wa TGGAProfesa Qooro akimuaga Zakia Meghji. Katikati ni Kamishna Mkuu wa TGGA, Hangi.
Qooro akigana na Anna Abdalah. Kushoto ni Hangi. (PICHA ZOTE NA RICHARD MWAIKENDA)

Azam Marine Kusafirisha Abiria Tanga - Unguja na Pemba kwa Meli Kubwa ya KisasaMeli Kubwa inayoweza kuingia abiria na mizigo kwa pamoja ambayo itafanya safari zake kati ya Tanga-Unguja na Pemba ikiwa inaingia bandari ya Tanga leo wakati wa uzinduzi wake ambapo uwekezaji huo mkubwa umefanywa na kampuni ya Azam Marine ili kuwanusuru wananchi wa mkoa wa Tanga na changamoto za usafiri huoMeli Kubwa inayoweza kuingia abiria 1600 na magari hamsini yenye mizigo kwa pamoja ambayo itafanya safari zake kati ya Tanga-Unguja na Pemba ikiwa inaingia bandari ya Tanga leo wakati wa uzinduzi wake ambapo uwekezaji huo mkubwa umefanywa na kampuni ya Azam Marine
Meneja Mkuu wa Azam Marine Husein Mohammed wa pili kulia akitazama namna wananchi wanavyoshuka kwenye meli hiyo itakayopunguza adha na usumbufu kwa wananchi wanaosafiri kutoka mkoani Tanga kwenda Unguja na Pemba
Meneja Mkuu wa Azam Marine Husein Mohammed katikati akizungumza na watumishi wa mamlaka ya Bandari Mkoani Tanga wakati wa ujio wa meli hiyo kwenye bandari ya Tanga kulia ni Kaimu Meneja wa Bandari ya Tanga,Tryphoni Ntipi kushoto ni PRO wa Mamlaka hiyo,Moni Jarufu.
Meneja Mkuu wa Azam Marine Husein Mohammed katikati akisalimiana na Kaimu Meneja wa Bandari ya Tanga, Tryphoni Ntipi wakati wa ujio wa meli hiyo kushoto ni PRO wa Mamlaka hiyo, Moni Jarufu.
Meneja Mkuu wa Azam Marine Husein Mohammed akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na ujio wa meli hiyo kulia Mkurugenzi Mkuu wa Ulinzi na Usalama wa vyombo vya majini (SUMATRA) Kaptain Mussa Mandia.Mkurugenzi Mkuu wa Ulinzi na Usalama wa vyombo vya majini (SUMATRA) Kaptain Mussa Mandia katikati akizungumza na waandishi wa habari kushoto ni Meneja Mkuu wa Azam Marine Husein Mohammed.
Waandishi wa Habari wakiwa kazini kushoto ni Amina Omari wa Gazeti la Mtanzania katikati ni Mariam Shedafa wa Azam TV.
 Vifaa vya uokozi wakati wa majanga ya ajali hivyo.
Baadhi ya Sehemu ya VIP ndani ya Meli hiyo kama inavyoonekana
Habari kwa Hisani ya Blog ya Kijamii, Tanga Raha