Friday, January 7, 2011

Serikali yawataja wamiliki Dowans

Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja (katikati) akizungumza na wanahabari kufafanua malipo ya tozo itakayolipwa na TANESCO kwa Dowans Januari 6, 2011. Picha na Richard Mwaikenda.
*Sasa TANESCO kuilipa Dowans bil 94

UTATA uliokuwa umetanda juu ya wamiliki wa kampuni ya Dowans hatimaye umekoma baada ya Serikali kuwatafuta wamiliki wake pamoja na majina ya wakurugenzi wa kampuni hiyo.

Akizungumza na wanahabari jana Dar es Salaam Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja amesema baada ya Serikali kufuatilia taarifa kutoka kwa Wakala wa Usajili wa Makampuni na Biashara nchini (BRELA), imewapata wamiliki na kuyataja majina yao.

Ngeleja alisema wamiliki wa kampuni hiyo kwa mujibu wa taarifa ya BRELA ni Dowans Holdings S. A, kampuni ambayo inamiliki hisa 81 ya nchini Costa Rica, huku akimtaja mmiliki mwingine kuwa ni kampuni ya Portek Systems and Equipment PTE ltd ya Singapore.

“Kwa mujibu wa taarifa tulizopata kutoka Wakala wa Usajili wa Makapuni na Biashara nchini (BRELA) kupitia barua ya BRELA yenye Kumb. Na. MITM/58550/22 ya tarehe 5, Januari, 2011 wamiliki/ wanahisa wa Dowans Tanzania Limited ni Dowans Holdings S. A hisa 81 na Portek Systems and Equipment PTE Limited hisa 54,” alisema Ngeleja.

Alisema taarifa zinaonesha kuwa wakurugenzi wa Dowans Tanzania Limited ni Andrew James Tice kutoka Canada, Gopalakrishnam Balachandran wa India, Hon Sung Woo kutoka nchini Malaysia.

Aidha Ngeleja aliwataja wakurugenzi wengine kuwa ni pamoja na Guy Arthur Picard kutoka nchini Canada, Sulaiman Mohammed Yahya Al Adawi wa nchini Oman pamoja na Stanley Munai wa nchini Kenya.

Aidha akitoa ufafanuzi juu ya suala zima la tozo ambayo ni uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi chini ya Kitengo cha Biashara cha Kimataifa (ICC) iliyolitaka Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kulipa kiasi cha dola za Kimarekani 65,812,630.00 kwa Dowans.

Amesema baada ya kupata ushauri kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wanasheria wa TANESCO, Serikali imekubali shirika hilo kulipa kiasi hicho cha fedha kwa Dowans na taratibu zinafanywa kulipa kiasi hicho cha fedha.

Hata hivyo Ngeleja amesema Serikali haitaiachia mzigo huo TANESCO yenyewe na badala yake itatoa kiasi cha fedha kwa lengo la kulisaidia shirika hilo.

“Kutokana na ushauri uliotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wanasheria wa TANESCO kwamba kupinga tozo/uamuzi huo dhidi ya TANESCO hakutafanikisha azma yoyote isipokuwa kuchelewesha utekelezaji wa tozo/ uamuzi huu…Serikali haina budi kutekeleza uamuzi uliotolewa na Mahakama hiyo na kuepuka gharama zaidi ikiwa maamuzi ya Mahakama ya Usuluhishi yatapuuzwa,” alisema.

Kwa hatua hiyo Serikali na TANESCO inatakiwa kulipa kiasi cha sh. bilioni 94 za fedha za Kitanzania, hii ikiwa ni kwa mujibu wa bei ya soko la mabadiliko ya dola kwa jana (yaani Januari 6, 2011).

Waziri Ngeleja alipinga vikali kuwa ongezeko la gharama za umeme silizopitishwa juzi hazina uhusiano wowote na tozo inayotakiwa kulipwa na TANESCO kwani maombi ya kuomba gharama za umeme kupanda yaliombwa na shirika hilo muda mrefu, hata kabla ya hukumu iliyotolewa juzi na ICC.

Aidha kwa upande mwingine alisema Serikali inaunga mkono ongezeko la gharama za umeme lililopewa TANESCO, kwani tangu mwaka 2007 haijawahi kupandisha gharama za umeme ili hali gharama za uzalishaji zipo juu kwa sasa.

Wakati huo huo Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, William Mhando amesema makali ya mgawo wa umeme yanaoendelea kwa sasa maeneo mbalimbali yataendelea kuwepo kutokana na dosari za uzalishaji wa nishati hiyo katika gridi ya Taifa.

Akifafanua alisema mgawo wa sasa unatokana na kupungua kwa maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme ya Kihansi, Kidatu, Pangani pamoja na kushuka kwa uzalishaji wa gesi kwa megawati 50.

Akizungumzia madeni alisema TANESCO inaidai Serikali takribani kiasi cha shilingi bilioni 70, huku deni la jumla kwa wateja wote yaani Serikali na watu binafsi ikifikia shilingi bilioni 270.
  Na mdau Joachim Mushi, Dar es Salaam








No comments:

Post a Comment

SEIF SHARIFF HAMAD AKIRI KUWA YEYE NI BABU KIZEE.

Seif Shariff Hamad Seif Shariff Hamad KWA mara ya kwanza Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Seif Shariff Hamad amek...