Sunday, January 2, 2011

Kikwete 'aridhia' katiba mpya

Rais Jakaya Kikwete.


Ijumaa, ya Desemba 31, 2010

HATIMAYE, Rais Jakaya Kikwete ametangaza kuanza kwa mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya kama ilivyo kuwa ikililiwa na baadhi ya wananchi, viongozi na wanaharakati.

Kwa mujibu wa hotuba aliyoitoa kama salamu zake za mwaka mpya kwa Taifa Desemba 31, 2010, amesema ameamua kuunda tume itakayoratibu mchakato wa awali.

"...nimeamua kuunda Tume maalum ya Katiba,  'Constitutional Review Commission'.  Tume hiyo  itakayoongozwa na mwanasheria aliyebobea, itakuwa na wajumbe wanaowakilisha makundi mbalimbali katika jamii yetu kutoka pande zetu mbili za Muungano," alisema Kikwete.

Alilitaja kuwa jukumu kubwa la tume hiyo itakuwa ni  kuongoza na kuratibu mchakato utakaowashirikisha wananchi wote vikiwemo vyama vya siasa, wanasiasa, wafanyabiashara, asasi za kiraia, mashirika ya dini, wanataaluma na makundi mbalimbali ya watu wote, katika kutoa maoni.

Alisema baada ya kukamilisha kukusanya maoni, Tume itatoa mapendekezo yatakayofikishwa kwenye vyombo stahiki vya Kikatiba kwa kufanyiwa maamuzi zaidi.

"Baada ya makubaliano kufikiwa, taifa letu litapata Katiba mpya kwa siku itakayoamuliwa ianze kutumika," alisema Kikwete.

Hata hivyo aliongeza kuwa lengo la kuandikwa Katiba mpya ni kuiwezesha nchi kuwa na Katiba inayoendana na taifa lenye umri wa nusu karne na kwamba mchakato huo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

"La nne ambalo tulilokubaliana kufanya ni kuanzisha mchakato wa kuitazama upya Katiba ya Nchi yetu kwa lengo la kuihuisha ili hatimaye Katiba yetu ya sasa tuliyoachiwa na waasisi wa taifa letu, imeifanyia nchi yetu mambo mengi mazuri na kuifikisha Tanzania na Watanzania hapa tulipo," alisema Kikwete.

"....mwaka 2011, nchi yetu inatimiza miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, miaka 47 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar na miaka 47 ya Muungano wa nchi zetu mbili.  Yapo mabadiliko mengi yaliyotokea katika nyanja mbalimbali za maisha ya nchi yetu na watu wake katika kipindi hiki.  Kwa ajili hiyo ni vyema kuwa na Katiba inayoendana na mabadiliko na matakwa na hali ya sasa". 

"Wananchi watapewa fursa ya kutosha ya kutoa maoni yao kwa uhuru na pawepo kuvumiliana kwa hali ya juu pale watu wanapotufautiana kwa mawazo," alisema.

"Naomba washiriki waongozwe kwa hoja badala ya jazba.  Tukiwa na jazba, hasira na kushinikizana kamwe hatutaweza kutengeneza jambo jema.  Na inapohusu Katiba ya Nchi itakuwa hasara tupu.  Haitakuwa endelevu na kulazimika kufanyiwa marekebisho mengi mwanzoni tu baada ya kutungwa," alisema.

Hata hivyo tamko la kikwete linapingana na baadhi ya washauri wa Serikali yake katika masuala ya kisheria akiwemo Mwanasheria Mkuu, Jaji Frederick Werema ambaye hivi karibuni alikaririwa na vyombo vya habari akipinga kuandikwa kwa katiba mpya na kushauri iliyopo iendelee kufanyiwa marekebisho (kuwekewa viraka).

“Kuandika Katiba mpya hapana, lakini kufanya marekebisho kwa kuondoa au kuongeza mambo fulani kwenye katiba, ruksa,” alisema Jaji Werema.
Na Mdau wa Blog.



No comments:

Post a Comment

SEIF SHARIFF HAMAD AKIRI KUWA YEYE NI BABU KIZEE.

Seif Shariff Hamad Seif Shariff Hamad KWA mara ya kwanza Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Seif Shariff Hamad amek...