Friday, December 17, 2010

Makala na chambuzi mbalimbali zinazoandikwa na mdau wa blog yetu


17/12/2010

Tumeshindwa kuziepuka
ajali za mwisho wa mwaka?

HUU ni mwezi wa mwisho kabla ya kuingia Mwaka Mpya 2011. Ni kati ya miezi yenye siku kuu nyingi ambazo hujumuisha watu ulimwenguni kote. Miongoni mwa Sikuu Kuu kubwa ni Chrismas, ‘Boxing Day’ pamoja na Mwaka Mpya ambao huanza kusherehekewa usiku wa mwezi huu.

Kipindi hiki ndicho hutokea matukio mengi ya ajali hasa za vyombo vya moto huku mengine yakisababishwa kizembe na baadhi ya madereva wa vyombo hivyo. Wengi tumejijengea imani potofu kuwa kutokea kwa matukio hayo kuna ulazima kipindi hiki.

Kimsingi matukio haya ya ajali hayana uhusiano wowote na mwisho wa mwaka wala siku kuu za kipindi hiki. Ni uzembe ambao usababishwa na baadhi ya madereva wanaoshindwa kutumia busara na hekima wa kufanya mambo.

Mdau ‘Madamoto’ nimeliona hili vipindi tofauti na leo tutajadili kwa pamoja. Matukio ya ajali za kipindi hiki huchangiwa na makundi mengi tena kipuuzi zaidi. Nitaanza na kundi la kwanza ambalo huenda likawa linaongoza kwa kusababisha ajali hizi kiasi kikubwa.

Hawa ni madereva na wamiliki wa vyombo vya moto hasa vya usafirishaji abiria nje na ndani ya mikoa. Kimsingi kipindi hiki kinakuwa na idadi kubwa ya wasafiri hasa wanaoelekea mikoani. Kutokana na uwepo wa idadi kubwa ya wasafiri vyombo vya usafiri huelemewa.

Wapo baadhi ya wamiliki wa vyombo vya usafiri hukiuka taratibu za usafiri kwa makusudi. Wengi baada ya kuona ongezeko la idadi ya abiria huchukua hata magari ambayo yalikuwa yameweka pembeni kutokana na kuchakaa.

Magari haya hufanyiwa ukarabati kidogo na kurejeshwa barabarani hivyo mengi huwa katika hali mbaya. Mengi huwa mabovu hivyo kufanya safari ndefu kwa kubahatisha na hivyo kuwa hatari zaidi kiusalama wa abiria.

Kama hiyo haitoshi baadhi ya madereva wasio waaminifu nao hutumia magari madogo ya abiria yanayofanya safari fupi za jijini kama vile ‘Coster’ na DCM hivyo kuyatumia kinyemela kusafirisha abiria kwenda mikoani, tena kwa kutoza nauli zilezile.

Kimsingi magari haya huwa si salama kwani huwa yamechoka sana japokuwa wengi huyakarabati kwa kuyapaka rangi upya. Hata hivyo yanakuwa hayana uwezo wa kusafiri masafa marefu ya kwenda mikoani mfano Arusha, Dodoma, Morogoro na Kilimanjaro.

Kibaya zaidi huwa yakiendeshwa na madereva ambao pia hawana uzoefu wa kutembea masafa marefu, hali hii pamoja na mwendo mkali wanaoutumia katika vyombo hivyo ndiyo huongeza matukio ya ajali. Ndio maana madereva wengi wanaosababisha ajali hizo hutoweka mara moja.

Pamoja na hali hiyo magari mengi hujaza abiria kupindukia jambo ambalo ni hatari nyingine kwa abiria na mali zao. Madereva na wamiliki wa vyombo vya abiria hasa wa mikoani kipindi hiki hukifananisha na msimu wa mavuno. Hali hii huwafanya kuwa na tamaa kupindukia.

Wasimamizi wa vyombo vya usafiri wakiwemo trafiki nao hubweteka kwa kupewa ‘kitu kidogo’ hivyo kuwaacha wapuuzi wachache waendelee kuchezea roho za watu mikononi. Nasema hivyo maana mazingira ya hatari wanayoyaandaa kipindi hiki baadhi ya madereva na wamiliki wa vyombo vya usafiri hayana tofauti na kuchezea roho za watu mikononi.

Kwa magari makubwa ya mikoani wapo baadhi ya wahusika hupanga mabechi au kuweka viti vidogo (vigoda) katikati ya gari na kuwapanga abiria wengine kuvikalia viti hivyo. Hali hii huwa ni hatari zaidi kwani mbali na gari kuwa limezindisha abiria, lakini abiria huwa wamekaa au kisimama hivyo kutokuwa na msaada wowote kiusalama baada ya kutokea ajali.

Mdau ‘Madamoto’ juzi nilisafiri kwenda Tanga na gari moja la kapuni maarufu tu ya kusafirisha abiria kwenda mikoani. Gari hilo lilikuwa limejaza kupindukia. Wafanyakazi walidiriki kupanga viti vidogo katikati ya gari na kuendelea kupakia abiria njiani.

Hali hii ilikuwa ni hatari japokuwa tulikuwa tukipishana na askari wa usalama barabarani takribani vituo vyote na baadhi walikuwa wakiingia na kushuka kwenye gari letu bila kuhoji chochote. Watasema nini wakati kila wanapoyasimamisha mabasi hayo baadhi hupewa ‘chochote’ yaani sh. 2,000, 3,000 hadi 5,000 kwa kila gari?

Kibaya zaidi hata suala la mikanda ya abiria ndani ya mabasi haikaguliwi tena kutokana na wahusika wengi kupewa chochote barabarani. Na madereva wengine huendesha huku wakiwa wametumia vileo jambo ambalo pia ni hatari kwa abiria na mali zao.

Naabiria nao tuache kushabikia mwendo mkali wa vyombo vya moto, tufunge mikanda tunapoingia kwenye vyombo hivyo na tushirikiane kwa pamoja kusimamia sheria zisifunjwe ili kupunguza mianya ya wakiukaji sheria za usalama barabarani.

Tukifanya hivyo kwa pamoja tunaweza kudhibiti matukio mengi ya ajali yanayotokea mara nyingi kipindi cha Siku Kuu za mwishoni mwa mwaka, ambazo wengi wetu huamini kuna ulazima na sababu ya kuongezeka kwa ajali hizo.

By Joachim Mushi 0717030066/0786030066/
Barua pepe: jomushi79@yahoo.com



25/11/2010
Timu hii ndio itakayoinusuru CCM 2015

RAIS wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete tayari ametangaza
baraza lake la mawazi ambao ndiyo watakao kuwa na jukumu la kumsaidia
kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Baraza la kipindi hiki ni tofauti na lililopita. Halikuwa kama kila mmoja alivyotaka hasa kwa wale wadau wengi wa masuala ya siasa ambao ndio walikuwa mstari wa mbele kutoa maoni kwenye vyombo vya habari.

Baadhi ya wadau walitaka baraza liendelee kundwa dogo ili kuipunguzia Serikali
mzigo, lisijumuishe wakongwe, liwe na sura mpya na lisijumuishe wanasiasa wenye tuhuma mbalimbali hasa za urasimu wa fedha za Serikali.

Kwa kiasi fulani amefanikiwa kwa baadhi ya vipengele. Baraza jipya limeziacha
sura zilizokuwa zimezoeleka, kama Profesa David Mwakyusa, Profesa Juma Kapuya, John Chiligati, Profesa Peter Msolla na wengineo.

Majina hayo baadhi ni wakongwe wa muda mrefu Serikalini. Yalikuwa yamezoeleka hivyo hakufanya vibaya kujaribu kuchanganya na kuwapumzisha wengine. Mchanganyiko kama huu wawezakuwa chachu ya mabadiliko ya kasi kiutendaji.

Baraza lililopita lilikuwa na mawaziri 28, pamoja na manaibu waziri 21 hili lilipungua ukilinganisha na aliloliunda Rais Kikwete mara ya kwanza aliposhika wadhifa huo. Baraza la awamu yake ya kwanza lilikuwa na mawaziri na manaibu waziri zaidi ya 60.

Baraza jipya aliloliunda juzi lina jumla ya mawaziri 29 na manaibu waziri 21 ambao wanafanya idadi ya mawaziri wote kufikia 50. Baraza hili limeongezeka tofauti na lililomaliza muda wake kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Lililopita lilikuwa na jumla ya mawaziri 49. Yapo mambo yanalolifanya baraza jipya kuonekana laweza kuwa bora licha ya kuongezeka. Kwanza ni sura mpya ambazo huenda zikaleta chachu kubwa katika utendaji. Kuna jumla ya sura mpya takribani 24 jambo ambalo laweza kuwa na matumaini.

Kama hiyo haitoshi mawaziri wengi waliokuwa wakikabiliwa na tuhuma kadhaa wameachwa nje, licha ya kuwa wakitajwa mara kadhaa kwamba huenda wangejitokeza katika baraza hilo. Hii ni ishara ya kwanza ya kutia matumaini kwa wananchi.

Lingine ni kwamba viongozi wabunge ambao walionekana kufanya vizuri wamekumbukwa bila kujali misimamo yao. Wabunge wa CCM kama Dk. Harrison Mwakyembe, Dk. John Magufuli, William Ngeleja, Dk. Cyril Chami na aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta wamepewa uwaziri.

Kimsingi hapa tunataka kuona mchango wao kwa wananchi, kwani wengine walikuwa mstari wa mbele bungeni kupinga hoja na wabunge ambao walionekana kutetea hoja zilizokuwa tata, huku zikiwa hazina maslahi kwa wananchi.

Dk. Magufuli ambaye anafanya vizuri karibu kila wizara anayopelekwa sasa kapewa Wizara ya Ujenzi ambayo awali iliitwa Maendeleo ya Miundombinu. Wizara hii katika baraza jipya imegawanywa na kupata wizara mbili ambayo ya pili itajulikana kama Wizara ya Uchukuzi.

Miundombinu ya barabara bado ni tatizo kubwa nchini, ipo miradi ya barabara ambayo imekuwa ikihujumiwa na makandarasi miaka nenda rudi huku siku zikipotea. Usimamizi wa mashaka umechangia barabara nyingi kujengwa bila viwango na kudumu muda mfupi kabla ya kuanza kuharibika.

Magufuli akitumia makali yake ufanisi anaweza kuibadili Wizara ya Ujenzi. Naibu wake amepewa Dk. Mwakyembe ambaye ni machachari. Dk. Mwakyembe ni miongozi mwa wabunge walioongoza kamati iliyochunguza mkataba tata wa Richmond na kusababisha idadi kubwa ya mawaziri kujiuzulu akiwemo aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.

Mwingine ni aliyepewa Wizara ya Ushirikiano Afrika Mashariki yaani Samuel Sitta. Mbunge huyu amejizolea umaarufu baada ya kuliongoza Bunge la Tisa kama Spika na kuliendesha wizuri kiasi cha kupendwa hadi na kambi ya upinzani. Kitendo hicho kimelifanya bunge kuwa na nguvu na kuleta changamoto kwa Serikali kwa masuala mbalimbali.

Mdau ‘Madamoto’ anaona mbali na mawaziri wengi wapya kuzungumzwa kwa kutumainiwa na wananchi, matumaini makubwa ni kwa aliyekuwa Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN- Habitat), Profesa Anna Tibaijuka, ambaye amepewa kuongoza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mbunge huyu amefanya mengi akiwa ndani ya UN-Habitat nje na ndani ya Tanzania. Ameendesha miradi mbalimbali ambayo imekuwa ikiwasaidia Watanzania hasa miradi ya huduma za kijamii. Wizara aliyopewa inaendana na kazi alizokuwa akizifanya nje ya nchi ngazi ya kimataifa kwa muda mrefu. Hali hii ndiyo inayonipa ujasiri wa kuamini kuna mabadiliko makubwa na ya kimanufaa yataibuka katika wizara hiyo.

 Kimsingi sura nyingi mpya, mabadiliko ya kimuundo wa baraza na changamoto kutoka kwa vyama vya upinzani, iliyoipata Serikali iliyopita iliyoundwa na CCM ni mambo yanayotoa matumaini ya wateule wote kuchapa kazi ili kuendelea kujenga heshima ya chama inayoanza kuporomoka. Na timu hiyo ya baraza zima la mawaziri ndiyo itakayoinusuru CCM Uchaguzi Mkuu 2015.

Joachim Mushi, anapatikana kwa barua pepe;
jomushi79@yahoo.com au
Simu; 0717 030 066/ 0786 030 066   


15/10/2010
Ahadi zetu kiama cha vyama, wagombea

WENYEWE wanasema ahadi ni deni. Kwamba chochote unachoahidi ni lazima ukitekeleze, hata kama hautafanya hivyo unatakiwa kujua hilo tayari ni deni. Na wahenga walisema dawa ya deni ni kulipa na si vinginevyo.

Semi hizi zote nilizozitaja hapo juu zinaeleza na kutufundisha mambo kadhaa juu ya ahadi zetu tunazozitoa maeneo mbalimbali katika maisha ya kila siku. Miongoni mwa mambo hayo ni kwamba hatuna budi kuwa makini na ahadi tunazozitoa kwa watu, kwani kila unachokiahidi unapaswa kukitekeleza kama ulivyo ahidi.

Pia semi hizo zinatukumbusha kuwa wakweli juu ya mambo kadha wa kadha, kwani chochote utakachoahidi na kwa namna yoyote utalazimika kukitekeleza, na kama hautofanya hivyo wapaswa kujua uliowaahidi wana kila sababu ya kukudai utekeleze.

Mdau ‘Madamoto’ nimelazimika kulikumbushia suala la ahadi kwasababu nimeguswa na hata kitishwa. Si kwamba nimetishiwa na kitu kibaya katika maisha, lakini ni juu ya kauli za wagombea wa nafasi mbalimbali hasa za urais.

Mdau “Madamoto’ nimekuwa nikifuatilia mikutano mbalimbali ya wagombea wa nafasi za udiwani, ubunge na hata urais. Wamekuwa wakiahidi mengi katika mikutano yao kwa wapiga kura. Wanasema ahadi zote hizo watazitimiza pale watakapofanikiwa kushika nafasi wanazogombea.

Kimsingi wanasema na kuahidi mengi na wakati mwingine mdau nimekuwa nikipima na kutafakari bila kupata majibu ya kuuridhisha mtima wangu. Nasema hivyo maana wakati mwingine nimekuwa nikidhani labda wanachokieleza ni utani kwa wananchi ambao ni wapiga kura. Lakini nakumbushwa kuwa hapana, haiwezekani wakawatani hadi wapiga kura tena kipindi hiki muhimu.

Nasema haiwezekani wakawa wanatania maana nakumbushwa upande mwingine na semi nilizoanza nazo katika mada hii kuwa, ahadi ni deni. Hivyo chochote wanachokiahidi kwenye majukwaa ya siasa watalazimika kukitekeleza pindi watakapofanikiwa kuingia madarakani.

Mdau wa ‘Madamoto’ ahadi hizi ni kali na kwa mazingira mengine zaonekana ngumu kutekelezeka kwa mazingira yetu. Kwa nafasi za uraisi wapo baadhi ya wagombea wamekuwa wakiahidi watakapofanikiwa kuunda Serikali (nafasi ya urais) elimu itatolewa bure kuanzia shule za awali hadi chuo kikuu.

Wapo wagombea walioahidi watakapofanikiwa kuingia ikulu watahakikisha Serikali yao inawagharamia watu wote wenye ulemavu ambao kutokana na hali zao hawajiwezi. Mbali na hilo pia Serikali itagharamia familia zao kwa masuala yote muhimu ya kiafya.

Kama hiyo haitoshi wapo walioahidi kuwa Serikali yao itakuwa ikitoa huduma zote bure kwa wazee na kuweka utaratibu wa kulipwa kwa kila kipindi fulani. Wagombea wengine ili kuonekana wao ni tofauti wamekwenda mbele zaidi na kudai wao mishahara kwa wafanyakazi itakuwa ikitolewa kila wiki na si kusubiri hadi mwisho wa mwezi.

Upo utaratibu ambao umewekwa na baadhi ya viongozi kulinda bidhaa fulani fulani zisitoke bila utaratibu unaotambulika. Lakini ili kila mmoja aonekane tofauti wapo wagombea tayari wameahidi endapo watafanikiwa kuingia madarakani wataruhusu wakulima kwenda kuuza bidhaa zao mbalimbali wenyewe nje ya nchi wanavyotaka.

Wengine wameahidi kuwaongezea mishahara wafanyakazi mara dufu ili waondoke katika hali walizonazo sasa na kuwa na maisha mazuri zaidi. Wagombea urais wengine tena wenye ushawishi mkubwa wameahidi kuwakamata watu wote wanaotuhumiwa kuwa mafisadi, kuwafilisi na kuwafunga.

Kama hiyo haitoshi wapo walioahidi neema kwa wakulima wa Tanzania, kwamba pindi watakapoingia madarakani watahakikisha wakulima wote wanaachana na matumizi ya majembe ya mkono na kutumia plau na nyenzo nyingine za kisasa kwa kilimo.

Zipo ahadi kochokocho zilizotolewa na viongozi hao hasa nafasi za urais. Na ahadi hizi zimetolewa zikitolewa na wagombea wote wa nafasi za urais. Mdau naziita neema za Watanzania kama kweli zitatekelezwa kwa baadhi yao watakao kubalika na kuchaguliwa kweli.

Ahadi hizi tayari nyingi zimetolewa na zitaendelea kutolewa kwa wananchi. Lakini hala hala kwa wagombea ambao ni watoaji wa ahadi hizo. Tukumbuke kwamba kila marefu yana mwisho tusifikiri kuwa kipindi tutakachopewa madaraka ni kirefu kisicho na mwisho.

Au ahadi tunazotoa zitasahaulika kutokana na muda huo tutakapokuwa madarakani, la hasha. Kama mtu atapewa nafasi na iwe ni ubabaishaji kwa wananchi akumbuke kwamba tutazunguka na kurudi kipindi kingine cha uchaguzi.
Isije kuwa tunatoa ahadi kwa kujua kwamba kipindi tutakapo hojiwa na wananchi kutaka majibu wengi hatutakuwa madarakani. Hii itakuwa ni kuuwa nguvu ya chama na uaminifu kwa wapiga kura. Nasema hivyo kwa kuwa Watanzania wengi sasa ni waelewa, makini na wafuatiliaji wa mambo. Kila uchao hali ya muamko kwao inazidi kupanda.

Ahadi hizi zisije kuwa kiama kwa wangombea na vyama vyao.

Joachim Mushi 0717030066/0786030066
Barua pepe; jomushi79@yahoo.com





22/10/2010
Wapinzani hawawezi ingia madarakani ng’o

NI takribani mwaka wa 17 tangu nchi yetu iingie katika mfumo wa vyama vingi sasa. Ni wazi vyama vingi vimeleta changamoto kiasi kikubwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho ni chama tawala tangu tulipoingia katika mfumo mpya wa vyama vingi.

Nasema hivyo maana huwezi kulinganisha uchaguzi uliokuwa ukifanywa enzi za chama kimoja na unavyofanyika hivi leo. Kunamabadiliko makubwa kiushindani katika uchaguzi, kunamabadiliko kiutendaji kwa wagombea wanaokuwa madarakani na pia blaa blaa bila maneno zimepungua hasa majimboni.

Hakuna asiejua kuwa awali wapo wagombea ndani ya chama tawala walijisahau, walikuwa wakidhani wao waweza kuongoza miaka yote madarakani hasa katika nafasi za uwakilishi wa wananchi (ubunge)-ndio maana hata wengine waliyabatiza majimbo ya uchaguzi na kuyaita ‘majimbo yao’.

Kweli tulijisahau ndio maana hata wengine leo hii wakianguka katika majimbo ya uchaguzi wamekuwa wakiamini wamehujumiwa. Hakuna, lazima tukubali uongozi ni kupishana-ukishindwa rudi nyuma jipange upya na uangalie wenzako wanavyo watumikia uliokuwa ukiwatumikia.

Hata hivyo, licha ya ya kuwepo kwa mabadiliko na changamoto hizo safari bado ni ndefu kufikia mageuzi ya moja kwa moja, nasema hivi najua wapo watakao pinga na wengine kudhani mdau ‘Madamoto’ ni kikwazo cha mapinduzi yoyote- la hasha hawa watakuwa wanapotoka.

Leo nataka nikueleze sababu kadhaa zinazonilazimisha kuamini bado kuna safari ndefu ya mageuzi. Kwanza kabla ya kusema ni vema nikatoa angalizo hili; kwa wanaofuatilia masuala ya siasa chama cha upinzani kilichoanza kwa mbwembwe kiasi cha kukinyima usingizi chama tawala kipindi cha nyuma kilikuwa NCCR-Mageuzi.

Kwa wanaokumbuka chama hiki ambacho hapo nyuma kilianza mithili ya kundi la wanaharakati, kiliwahi kuwa na nguvu si mchezo. Baadae kilitulia tuli na kuibuka Chama cha TLP, hiki kilivuma pia na kuitingisha CCM kabla nacho kufifia. Lakini haikuishia baadae kilianza kuvuma Chama cha Wananchi (CUF) kwa wakati wake nacho kwa bara kiliambulia patupu.

Wapo wanaoweza kupinga hili lakini niweke wazi kwa muonekano wa kawaida lazima tukubali kuwa chama kinachoinyima CCM usingizi ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Hiki ndicho kinachovuma sasa karibia kila kona ya nchi hasa upande wa Tanzania Bara.

Historia inaonesha vyama hivi huvuma na kufifia kwa vipindi tofauti, lakini hasa nyakati za uchaguzi. Tafsiri rahisi wengi waweza kuamini hakuna wapinzani wa kweli nchini, ukiachilia mbali sababu nyingine ambazo zimekuwa zikitolewa na wagombea na hata vyama vingine.

Hii ni kwa kuwa hata tunaosema ni wapinzani wamekuwa wakihama kutoka chama kimoja kwenda kingine kila baada ya mchakato wa uchaguzi, na pengine vyama husika kufifia kabisa mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi. Pengine baada ya uchaguzi kingelikuwa kipindi muhimu cha chama kujipanga zaidi na kufanya vizuri hapo baadae.

Hata hivyo, mdau ‘Madamoto’ leo sitaki hili litawale zaidi mada yangu. Nataka kutaja kwanini itakuwa vingumu wapinzani kutwaa madaraka. Ukweli ni kwamba hakuna wapiga kura wanaotaka mapinduzi. Huu ndio ukweli amini usiamini.

Wananchi wengi wenye upeo na wanaotaka madaraka si wapiga kura. Wanapuuzia. Hawashiriki katika uchaguzi zaidi ya kushiriki kwa midomo na malumbano kwenye vyombo vya habari na vinginevyo. Siku zote wao hushiriki kwa malumbano kwenye majukwaa na mitandao ya intaneti tu.

Kwa mfano baadhi ya taasisi na vyombo vya habari wakati wa uchaguzi huanzisha utaratibu katika mitandao ya intaneti ya kukusanya maoni kwa mtindo wa kupiga kura na kuwashirikisha wagombea kadhaa, hasa wa nafasi za uraisi. Mara nyingi matokeo kama hayo kwa sasa endapo utawashindanisha wagombea wenye wafuasi wengi yaani Jakaya Kikwete (CCM), Dk. Willibrod Slaa (CHADEMA) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF)-aweza kushinda wa chama cha upinzani.

Matokeo hayo lazima yawe tofauti kabisa na matokeo halisi ya Uchaguzi Mkuu. Nasema hivyo kwa kuwa wapigaji kura wengi wa kwenye mitandao na malumbano si wapiga kura wa kweli, kwani huwa hawashiriki katika uchaguzi wa kweli. Ni wavivu wa kutumia haki zao. Hawawezi kupanga folini kupigwa jua kwa ajili ya kupiga kura siku ya uchaguzi.

Hawa wamekuwa wakishiriki wazuri wa uchaguzi wa kwenye mitandao ya intaneti zaidi ya kupiga kura halali siku ya uchaguzi na kumchagua kiongozi wanaeona anafaa. Hawa ni washabiki zaidi ya washiriki kwenye uchaguzi. Wanatoa matumaini hewa kwa wagombea hasa wa upinzani.

Ndio maana miaka yote wameishia kulalama kwenye mitandao, vyombo vya habari na majukwaa huku wakihoji kwanini Chama Cha Mapinduzi kinaendelea kufanya vizuri sehemu kubwa ya nchi. CCM huwashika zaidi wapiga kura wake wa kweli na si wapiga blaa blaa.

Sasa katika hali kama hii tutaendelea kulalamika hadi lini? Wapinzani hawawezi kwenda madarakani hadi pale tutakapokuwa na idadi kubwa ya Watanzania wapiga kura wa kweli na wanaopenda mapinduzi kweli.

Joachim Mushi, Simu; 07170030066,
Barua pepe: jomushi79@yahoo.com.

 

No comments:

Post a Comment

SEIF SHARIFF HAMAD AKIRI KUWA YEYE NI BABU KIZEE.

Seif Shariff Hamad Seif Shariff Hamad KWA mara ya kwanza Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Seif Shariff Hamad amek...