Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeondoa utaratibu wa awali kwa walipakodi wadogo kulipia kodi kabla ya kuanza kufanya biashara na badala yake kuwataka kulipia robo ya kwanza ndani ya siku tisini tangu kusajiliwa.
Kamishna wa Kodi za Ndani, Elijah Mwandumbya ameyabainisha hayo leo Jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa Kampeni ya Usajili wa Walipakodi.
Mwandumbya amesema jukumu la usajili wa walipakodi kwa Mamlaka hiyo ni chanzo cha kuongeza idadi ya walipakodi, wigo wa ulipaji kodi, kuongeza makusanyo pamoja na kuwa na taarifa sahihi za walipakodi wanaostahili kukadiriwa na kutozwa kodi ili kuchangia Pato la Taifa.
“kampeni hii inaenda sambamba na mabadiliko makubwa tuliyoyafanya kwa walipakodi wadogo kwa kuwapa siku tisini za kulipa kodi kwa robo ya kwanza ya malipo pindi tu watakapokuwa wamesajiliwa hivyo mabadiliko hayo yatakuwa chachu katika usajili kwani tunatarajia kusajili walipakodi takribani milioni moja nchi nzima,”alisema Mwandumbya.
Kamishna wa Kodi za Ndani amesisitiza kuwa usajili wa TIN ni bure na utafanyika katika ofisi zote za Mamlaka hiyo na katika vituo maalum vitakavyokuwa vimeteuliwa na kutangazwa kupitia vyombo vya habari na matangazo katika maeneo husika.
Aidha, Mwandumbya amewataka wananchi kujihadhari na vishoka wanaoweza kutumia mwanya wa kuharibu nia njema ya kampeni hiyo kwani hakuna wakala yeyote aliyepewa jukumu la kusajili wala kutoa fomu za usajili wa zoezi hilo.
Amefafanua kuwa muhusika lazima aende mwenyewe ili apigwe picha na kuchukuliwa alama za vidole pia atatakiwa aende na mkataba wa pango au uthibitisho wa umiliki wa mahali pa biashara, barua yenye muhuri na namba ya simu ya Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa pamoja na kitambulisho cha muhusika kama vile hati ya kusafiria, leseni ya udereva, kitambulisho cha uraia au cha mpiga kura.
Kampeni hiyo imezinduliwa nchi nzima kwa nia ya kuhakikisha kila mwananchi anayestahili kupatiwa namba ya utambulisho ya mlipakodi anasajiliwa na kupata namba hiyo kwa urahisi na haraka.
No comments:
Post a Comment