Wednesday, January 31, 2018

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi aipa siku 3 TBA kumalizia bomoabomoa Tanesco

Bomoabomoa jengo la Tanesco.

KATIBU Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga ameipa siku tatu Wakala wa Nyumba nchini (TBA), kuhakikisha inamaliza kazi ya uvunjaji wa jengo la ghorofa 10 la Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Nyamhanga alitoa agizo hilo ikiwa ni takribani siku 63 tangu TBA kuanza ubomoaji wa jengo baada ya Rais John Magufuli Nevemba 15 kuagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuvunja jengo hilo na Ofisi ya Wizara ya Maji kwa kuwa zimejengwa katika hifadhi ya barabara.

Rais Magufuli alisema hakuna kumuonea mtu huruma au aibu katika kipindi hiki na kwamba kama Serikali imeenda kinyume na taratibu ivunjiwe kama walivyovunjiwa wananchi wengine.

Katibu mkuu alisema ubomoaji wa jengo hilo umechukua muda mrefu hivyo ikifika Februari mosi haitaji kuona jengo hilo likiwepo hivyo kuruhusu shughuli nyingine za ujenzi ziendelee.

“Wametoa maelezo ya kwanini wamechelewa kumaliza ubomoaji nimewaelewa ila ikifika Februari mosi sihitaji kuona sehemu iliyobakia tunataka ujenzi wa barabara ya kupishana uanze,” alisema.

Nyamhanga alisema mkandarasi amefanikiwa kuhamisha miundombinu mbalimbali ambayo ipo katika eneo litakalojengwa barabara za kupishana (interchange) hivyo kinachosubiriwa ni TBA kumalizika uvunjaji.

Alisema baada ya kukagua amegundua kuwa kati ya ghorofa 10 nane zimeshavunjwa hivyo amewaagiza kumalizia ghorofa mbili zilizobakia ili mradi wa barabara za ya kupishana eneo la Ubungo uanze kama inavyotakiwa.

“Nimekagua ubomoaji naona maendeleo ni mazuri hivyo nimewaagiza ikifika kesho kutwa Alhamisi wawe wamemaliza ili kazi zingine ziendelee kwani wakandarasi wanawasubiri,” alisema.

Alisema dhamira ya Serikali ni kuona mradi wa barabara za kupishana unamalizika kwa wakati kama walivyokubaliana ambao ni miezi 36.

Mhandisi Nyamhanga alisema kwa mujibu wa mkataba kati ya Wakala wa Barabara Tanzania Tanroads na Mkandarasi kampuni ya China Civil Engeneering Contract Corporation (CCECC) ujenzi wa barabara hiyo utagharimu zaidi ya sh. bilioni 177.

Aidha, Nyamhanga alisema ujenzi wa barabara ya kilomita 16 njia nne kutoka Kimara hadi Kiluvya unatarajiwa kuanza mapema mwezi Machi.

Alisema ni imani yake kuwa hatua zinahitajika ili kupatikana mkandarasi zitachukuliwa haraka kwani fedha zipo.

“Pamoja na ujenzi wa barabara za kupishana hapa Ubungo Serikali imedhamiria kuifungua Dar es Salaam ambapo mwezi Machi ujezi wa barabara ya njia nne utaanza kutoka Kimara hadi Kiluvia,” alisema.

Akizungumzia hatua zilizofikiwa hadi sasa kuhusu ujenzi huo Meneja wa Tanroads mkoa wa Dar es Salaam, Julius Ndyamukama alisema uchambuzi wawakandarasi wenyewe uwezo wa kutekeleza mradi umefanyika, usanifu umefayika na zabuni imetolewa kwa kampuni iliyokidhi vigezo ili kuwasilisha gharama za mradi.

Ndyamukama alisema kesho wanatarajia watarejeshewa majibu na ndani ya siku 14 hatua zote zitakamilika ili ujenzi uanze.

Meneja huyo alisema katika upanuzi wa barabara hiyo kutajengwa madaraja matatu katika maeneo ya Kilivia, Kibamba na Mpiji pamoja na kuwepo barabara za mchepuko.

Aidha, alisema katika mradi huo kutakuwa na barabara za kupishana eneo la Mlonganzila ili kurahisisha kufika katika Hospitali ya Mlonganzila.

“Hatua zote zikimalizika ndio tutao taarifa rasmi kuwa ujenzi utagharimu shilingi ngapi kwa sasa tunakamilisha hatua muhimu," alisema.

No comments:

Post a Comment

SEIF SHARIFF HAMAD AKIRI KUWA YEYE NI BABU KIZEE.

Seif Shariff Hamad Seif Shariff Hamad KWA mara ya kwanza Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Seif Shariff Hamad amek...