Na Mwandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete amefanya uteuzi wa Makatibu Wakuu watano wapya na kuwahamisha wengine wanne kutoka wizara moja kwenda nyingine. Uteuzi na uhamisho huo unaanza mara moja.
Taarifa iliyotolewa Dar Es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi, Phillemon Luhanjo inasema mabadiliko hayo yanatokana na Muundo mpya wa Serikali ambapo Wizara ya Miundombinu imegawanywa katika wizara mbil na baadhi ya Makatibu Wakuu kustaafu kazi kwa mujibu wa Sheria.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Kikwete amemteua Fanuel Mbonde kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Ikulu. Kabla ya uteuzi wake, Mbonde alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu.
Wengine walioteuliwa ni Hussein A. Kattanga kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa;John Haule kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa;
Herbert Mrango ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi; na Eric K. Shitindi kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Kazi na Ajira.
Kabla ya uteuzi wake, Kattanga alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto; Haule alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha;
Mrango alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Shittindi alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
Kuhusu uhamisho, Rais Kikwete amemhamisha Sazi B. Salula kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwenda kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais;
Maimuna K. Tarishi ametoka Ofisi ya Waziri Mkuu kwenda Wizara ya Maliasili na Utalii; Injinia Omar Chambo amekuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi akitokea Katibu Mkuu wa Wizara ya zamani ya Miundombinu;
Bibi Kijakazi R. Mtengwa amekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dkt. Ladislaus C. Komba aliyekuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii anapangiwa kazi maalum katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Taarifa hiyo imesema Rais Kikwete amemhamishia Elizabeth Nyambibo Wizara ya Fedha na Uchumi ambako anachukua nafasi ya Naibu Katibu Mkuu iliyoachwa wazi na John H. Haule.
Kabla ya uhamisho wake, Nyambibo alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Taarifa ya Luhanjo imesema Makatibu Wakuu wapya wataapishwa saa tatu asubuhi leo Ikulu.
Katibu Mkuu, Philemon Luhanjo, wa pili kushoto akisalimiana na makatibu wakuu wapya kabla ya hafla ya kuaapishwa Ikulu. Picha kwa hisani ya Ikulu.
Makatibu wakuu wapya wakiwa wameketi kabla ya kuapishwa na Rais Jakaya Kikwete. Picha na Ikulu.
No comments:
Post a Comment