Wednesday, February 9, 2011

Wabunge wa Chadema watoka Bungeni tena


Wabunge wa Chadema wakiongozwa na Freeman Mbowe kutoka nje ya Bunge huku kikao kikiendelea



Wabunge hao wakitokomea nje baada ya kuzira kupitisha mabadiliko ya kanuni ya 15(2) tafsiri ya Kambi Rasmi ya upinzani bungeni. Habari kamili chini.


WABUNGE wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe jana walitoka tena nje ya ukumbi wa Bunge Ukumbi ya Bunge wakipinga azimio la kuondoa utata wa tafsiri ya Kanuni ya Bunge inayotaka chama chenye asilimia 12.5 ya wabunge wote kuunda kambi rasmi ya upinzani.

Mabadiliko hayo ya jana yanainyima Chadema kwa mujibu wa kanuni ya 15(2) tafsiri ya Kambi Rasmi ya upinzani bungeni sasa ni kambi inayoundwa na vyama vya upinzani vinavyowakilishwa bungeni.

Hata hivyo, bado Chadema kwa mujibu wa Kanuni za Bunge ndicho kitakachotoa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni na naibu wake. Pia kiongozi huyo ana mamlaka na uhuru wa kuteua Baraza la Mawaziri Kivuli kutokana na wabunge wa upinzani waliopo.

Azimio hilo linaondoa dhana iliyokuwepo kwamba Chadema ndicho kingetoa wenyeviti wa Kamati za Hesabu za Serikali ambazo kwa mujibu wa Kanuni za Bunge zinatakiwa kuongozwa na wapinzani.
Tofauti na ilivyokuwa ikifahamika awali, mabadiliko ya jana yanatoa fursa kwa mbunge yeyote wa upinzani kugombea nafasi hizo bila kuhitaji idhini ya  uongozi wa kambi ya upinzani.

Tukio la Chadema kutoka nje ya Bunge linafanana na lile la  Novemba 18, mwaka jana, ambapo wabunge hao walitoka baada ya Rais Jakaya Kikwete kuanza hotuba ya uzinduzi wa Bunge.

"Madamu Bunge limeona busara kuleta hoja hii, na vijembe vile, kwa masikitiko nasema hatutashiriki kumalizia hoja hii, naomba kutoa hoja," alisema Mbowe na kuanza kutoka nje akifuatiwa na wabunge wa chama hicho.

Wakati wabunge wa Chadema wakitoka nje, wabunge waliobaki wengi, walisikika wakitoa maneno ya kebehi dhidi ya wabunge Chadema. "...tumewazoea kukimbia, kwisha, uchoyo, weak politicians, na kwenye posho msije, mnadaiwa na mabenki," walisikika wabunge hao.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment

SEIF SHARIFF HAMAD AKIRI KUWA YEYE NI BABU KIZEE.

Seif Shariff Hamad Seif Shariff Hamad KWA mara ya kwanza Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Seif Shariff Hamad amek...