Thursday, February 24, 2011

‘Mkwe alininusuru kufa kwa mabomu’


Mzee Salum Mwinyi (kushoto) akifanya mahojiano na mwandishi wa makala haya, Joachim Mushi nyumbani kwake eneo la Majohe Kichangani hivi karibuni. (Picha na mdau Dotto Mwaibale)


‘Mkwe alininusuru kufa kwa mabomu’
*Niling’ang’ania ndani kutokana uzee

Na Joachim Mushi

YAWEZA ikawa inashangaza na wengine huenda hata wasiamini, lakini ndivyo ilivyokuwa. Mwanadamu unapoikimbia ajali hutokewa na nguvu za ghafla tena za ajabu ambazo zaweza kukusukuma kufanya mambo ambayo huwezi yafanya katika mazingira ya kawaida.

Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Salum Mwinyi kikongwe wa miaka tisini ambaye licha ya kutoweza kutembea kutokana na umri wake mkubwa na matatizo mengine, alipata nguvu za ajabu kukimbia hatari ya kifo. Hatari hii ilikuwa milipuko ya mabomu iliyotokea usiku wa Februari 16/17 mwaka huu kwenye kambi ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) kikosi namba 511 cha Gongo la Mboto.

“Namshukuru sana mkwe wangu (mke wa mtoto wake) naomba Mungu amjalie aweze kuishi maisha marefu, maana bila yeye nahisi muda huu nisingelikuwepo…ningelikuwa ni marehemu aliyeuawa kwa mabomu…ama kweli Mungu mkubwa,” anasema mzee Mwinyi huku akiwa amenyanyua mikono juu kuonesha ishara ya kumshukuru Mungu.

Mzee huyu anaonekana mchangamfu. Sijui kama ndivyo alivyo ama amekuwa mchangamfu baada ya kunusurika katika milipuko ya mabomu hayo. Nasema hivyo maana sikupanga kufanya mahojiano naye nilipomkuta, lakini nilijikuta nafanya hivyo baada ya maneno yake kunishawishi.

Anaishi nyumbani kwa mtoto wake wa kiume, Mkaeje Salum. Nyumba ya familia hii iliyopo eneo la Majohe Kichangani ni miongoni mwa majengo yaliyojikuta yakiangukiwa na mabomu yaliyokuwa yakilipuka bila mwelekeo. Hii imepigwa mabomu matatu.

Haijateketea yote lakini sehemu kubwa ya paa limefumuliwa na mabomu yaliyoelekea katika nyumba hiyo, yameangukia kwenye vyumba vitatu vya jengo hili. Viwili hutumika kulala na kimoja ndicho anacholala mzee Mwinyi. Yaliangukia kwenye vitanda. Vitanda vimeharibika vibaya.

Mzee Mwinyi anasema baada ya kusikia mlipuko wa kwanza wa bomu hakuamini kama kweli lilikuwa ni bomu. Walianza kubishana na mkwe wake pamoja na wajukuu wake. Yeye aliamini kishindo hicho kilikuwa ni kupasuka kwa gurudumu la gari (pancha imepasua gurudumu na kutoa mlio).

Anasema mtoto wake, Mkaeje alimuunga mkono. Naye aliamini huenda ni mlio wa kupasuka kwa gurudumu. Milipuko ya kishindo iliyofuatia ndiyo iliyomaliza mvutano kimabishano kati yake, mtoto wake na mkwe wake. Waliungana na wengine kisha kuamini yalikuwa ni mabomu.

Maana walishuhudia mwanga mkubwa wa moto ukiangaza maeneo ya jeshi. Milipuko iliendelea huku ikisafiri angani na moto ukiwaka. Anasema ilikuwa ni hatari. Aliamini ni mabomu. Kila mmoja akaanza kutafuta namna ya kujinusuru. Mzee huyu amechoka kiumri, miguu yake haina nguvu za kutembea sawia.

Mtoto wake na mkewe waligawana watoto ili waweze kukimbia nao kuwanusuru na mabomu ambayo muda huo yalionekana kusafiri angani na kuanguka ovyo baadhi ya maeneo. Mzee Mwinyi alishikwa mkono na mkwewe akimuongoza na watoto ili wakimbie.

Haikuwa raisi maana aligoma kabisa kwa madai hana nguvu za kukimbia alishauri apewe mjukuu wake mmoja abaki naye ndani kwani ni salama. Mkwewe alikataa na kuendelea kumsii waondoke kujinusuru.

Baada ya kuona anapingwa huku milipuko ikiendelea kwa zamu aliamua kukimbilia ndani kwenye chumba anacho lala. Mkwewe na wengine walianza kukimbia, hatua chache mama yule aligeuka nyuma akifikiri mzee Mwinyi wapo pamoja. Hapana alikuwa amerudi ndani ya nyuma.

Mama yule akiwa watoto wake alimfuata na kumtoa kwa nguvu. Alimshika mkono na kuanza kuondoka naye kana kwamba anamkokota, hapo hapo alikuwa na watoto wake wengine njia moja. Msafara wao haukudumu. Ulitawanywa na kishindo kikubwa kingine cha bomu.

Walianguka chini karibu wote na walipoinuka alijikuta peke yake. Ilikuwa ni mshikemshike kila mmoja alikimbia anapopajua. Hakumuona wala kumkumbuka mkwewe. Alijikuta akipata nguvu na kuanza kukimbia mwenyewe na makundi ya watu waliokuwa wakikimbia kunusuru maisha yao.

Anasema hakujua anakokwenda muda huo zaidi ya kufuata mkumbo wa watu. Hajui nguvu za kuweza kukimbia alizipata wapi, lakini safari iliendelea. Alijikuta akikimbia na kutembea toka majira ya saa mbili usiku hadi saa kumi asubuhi. Haelewi nguvu zilitoka wapi.

Anasema alikimbia kwa kufuata mkumbo hadi saa kumi za asubuhi ambapo alijikuta amefika eneo la Kigogo Freshi. Alikuwa amechoka sana na japokuwa hakusikia maumifu sehemu yoyote usiku huo. Labda kwasababu ya woga, haijulikani.

Baada ya kufika eneo hilo na kutulia kwa muda alipata kumbukumbu kuwa alikuwa ameongozana na mkwewe pamoja na baadhi ya wajukuu zake, muda huo hakujua walitengana vipi. Roho ilimuuma sana maana hakujua kama ni wazima au la.

“Nilikuwa na usingizi mzito lakini zikuweza kulala kabisa muda wote niliwakumbuka mkwe wangu na wajukuu nimewaacha wapi, roho iliniuma na kujikuta nakosa usingizi japokuwa tulikuwa tumepumzika eneo hilo muda mrefu na wengine wakiwa wamejipumzisha,” anasema Mwinyi.

Mzee Mwinyi ambaye ni mstaafu wa Shirika la Reli nchi (TRC sasa TRL) anasema alikuja kukutana na ndugu zake mchana baada ya siku ya milipuko. Wote wamesalimika. Nyumba yao wameikuta imeshambuliwa na mabomu ambayo yamebomoa sehemu kubwa ya paa la nyumba hiyo.

Na kibaya zaidi ni kwamba chumba ambacho alikuwa anaking’ang’ania abaki kutokana na hali yake kimepigwa bomu ambalo limeangukia kitanda chake na wajukuu zake huku kikiwa kimeharibiwa vibaya. Na endapo asingelitolewa kwa nguvu na mkwewe huenda angelikuwa marehemu sasa.

“Ndiyo maana kila siku nikiangalia nyumba yetu ilivyoshambuliwa namshukuru sana mkwe wangu…maana alininusuru na mabomu kwa kiasi kikubwa,” anasema Mwinyi.

“Cha ajabu sasa ndiyo naanza kusikia maumivu ikiwa ni siku moja baada ya milipuko hiyo. Wananikanda miguu sina nguvu za kutembea tena kama ilivyokuwa siku ya milipuko,” anasema mzee Mwinyi anayetembea kwa msaada wa fimbo kutokana na umri wake mkubwa.

Anasema fimbo yake inayomsaidia kujikongoja siku zote imenyooka, lakini sasa imepinda kutokana na mikiki mikiki aliyokumbana nayo akiwa anakimbia kujinusuru. Naongeza ukiadisiwa waweza usiamini, lakini hali ilikuwa ngumu siku hiyo ya milipuko.

Anaeleza kuwa hawezi kulilalamikia JWTZ hata siku moja kwa tukio la siku hiyo. Anaamini ilikuwa ajali hata wao wasingependa itokee kabisa. “Nasema kile ni kifo…usiombe kabisa mtu hawezi kufanya kitu kama kile kwa makusudi, labda kama hajipendi hii ni ajali haipangwi,” anasema Mzee huyo ambaye ni miongoni mwa watu walionusurika katika milipuko hiyo ya mabomu.

0717030066, 0756469470, barua pepe: jomushi79@yahoo.com


No comments:

Post a Comment

SEIF SHARIFF HAMAD AKIRI KUWA YEYE NI BABU KIZEE.

Seif Shariff Hamad Seif Shariff Hamad KWA mara ya kwanza Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Seif Shariff Hamad amek...