Monday, February 28, 2011

Harusi ya Emmanuel Lymo na Gudila


Bw. Emmanuel Lymo akiwa na mkewe, Gudila katika hafla ya harusi yao iliyofanyika katika Ukumbi wa Kiramuu mara baada ya kufunga ndoa kwenye Kanisa la KKKT Dar es Salaam Februari 27, 2011.


Bw. Emmanuel akiwa na mkewe Gudila, nyuma yao ni wasimamizi wa ndoa yao.



Bi. Harusi Gudila akicheza muziki akiwa na mpambe wake.



Baadaye Emmanuel na mkewe Gudila walifungua muziki rasmi.



Baada ya muziki kufungulia mambo yalikuwa hivi...



Angalia hapa warembo wakijimwaga na mduara.



Baadhi ya wageni waalikwa wakilisakata rumba.



Hii ilikuwa ni keki waliolishana maharusi, lakini kama unavyojua mambo ya kichaga kulikuwa na ndafu kama tatu hivi ambazo zote zilitumika kupamba sherehe ya maharusi hawa.



Wakati wa kufungua shampeni haikumlazimu mgeni kusogea mbele ili apate mvinyo huo, kwani kila meza ilikuwa na shampeni yake. Hapa mmoja wa wageni waalikwa akifungua kinywaji hicho kwenye meza yetu.



Ulifika wakati wa maakuli, cheki.



Walianza maharusi kwanza



Waalikwa wakiendelea kulisakata rumba



Cheki waalikwa walivyokuwa bomba..!



Baadhi ya wanakamati wakiwa mbele ya wageni waalikwa.



Wanakamati wakipiga picha ya pamoja baada ya kutoa bonge la zawadi kwa maaharusi.



MC wa harusi hii ya kukata na shoka alikuwa mwendeshaji wa kipindi cha Cherekochereko kinachorushwa na televisheni ya TBC.



Mambo ilikuwa ni kata mti panda miti kwa upande wa vinywaji, cheki hapa; Peter Uisso (kulia) akiwa mmoa wa wageni waalikwa huku wakibadilishana mawazo ilhali meza ikiwa imesheheni vinywaji.



Pedejee John Uisso alikuwa mmoja wa waalikwa wa karibu wa maharusi, pichani anaonekana akitabaruku zaidi.



Waalikwa mbalimbali wakiendelea kupata moja moto moja baridi.
Picha zote na mdau Mkuu wa Harusi na Matukio. Tutaingiza picha zaidi na kurekebisha picha na maelezo mara baada ya kupata maoni ya wahusika kwenye sherehe hii. Karibu.








Friday, February 25, 2011

Chadema waandamana Mwanza

Baadhi ya viongozi wa Chadema wakiongoza maandamano.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA ) kimezindua mkakati wake wa kuwachochea wananchi kuiondoa Serikali kwa nguvu kama walivyofanya wananchi wa mataifa ya Tunisia, Misri, Libya na Baharin kinyume na Katiba ya Nchi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti viongozi wa chama hicho ngazi ya Taifa na baadhi ya wabunge wake katika uwanja wa furahisha Jijini Mwanza, walisema kuwa CHADEMA haikubaliani na serikali ya CCM pamoja na kueleza kutomtambua Rais Jakaya Kikwete kuwa ni kiongozi wa taifa hili na badala yake kuvunja katiba na kudai Dk.Willbrod Silaa kuwa ndiye rais ambaye hakutangazwa.

Akiwahuhutubia maelfu ya wananchi katika uwanja huo Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa Freeman Mbowe, alisema kuwa viongozi wakuu wa CHADEMA wamekuwa wakitoa kauli ambazo Serikali ya Kikwete na CCM wamekuwa wakizibeza na kuwakejeli hivyo wamefika Mkoani Mwanza kuungwa mkono na nguvu ya umma ili kuiondosha Serikali hiyo madarakani Serikali.

“Tumekuja kwenu kuomba kibali cha kuhakikisha mnatuunga mkono ili kuiondosha serikali ya CCM pamoja na Kikwete na hivyo tunaanzia mwanza kuzindua mkakati huu wa kupita kufanya kazi hiyo mkoa hado mkoa pamoja na kuwashukuru baada ya kuwachaguwa wabunge wa chadema,” alisema Mbowe .

Bei ya Sukari kushuka


Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami (Kushoto) na Naibu wake, Lazaro Nyalandu(Kulia) katika mkutano na waandishi wa Habari.


SERIKALI imefuta ushuru wa forodha kwa sukari kiasi cha tani 37,500 itakayoagizwa toka nje ya nchi za Afrika ya Mashariki, jambo ambalo linaweza kusababisha bei ya sukari kushuka nchini.
Agizo hilo limetolewa jana na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa baada ya kikao na wadau wa sukari nchini.

Waziri amesema kiasi cha tani 12,500 zitaagizwa toka nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika ya Mashariki hakihitaji kufutiwa kodi kwa kuwa hakuna tozo zozote kwa bidhaa hiyo.

Kutokana na mahitaji hayo kiasi cha tani 50,000 za sukari toka nje ya nchi, na kwa kuwa bei ya sukari katika soko la dunia imepanda kwa sasa, Serikali imeiagiza Mamlaka ya Bandari iweke utaratibu mahsusi wa kutoa kipaumbele kwa meli zitakazoleta sukari hiyo ili zipakuliwe haraka na kuifanya sukari imfikie mlaji mara moja.

Aidha, Mamlaka ya Mapato (TRA) wanaagizwa wachukue hatua za haraka kukamilisha taratibu za kutotoza ushuru wa forodha kwa sukari hiyo.

Serikali itaendelea kushirikiana na wadau katika sekta ndogo ya sukari ili kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa hii kwa bei nafuu. Ni imani ya Serikali kuwa kwa kuwa utekelezaji wa hatua hizi unaanza mara moja, mambo mawili yatatokea. La kwanza, sukari itamfikia kila Mtanzania popote alipo.

La pili, bei ya sukari itashuka; na kwa vyovyote vile, pamoja na bei kupanda katika soko la Dunia, Serikali inategemea kuwa bei ya sukari itakuwa chini ya sh. 1,700 kwa kilo, hata katika maeneo ya pembezoni kabisa, Aidha, Serikali imeweka utaratibu wa kukutana na wazalishaji na wasambazaji wa sukari mara kwa
mara ili kuongeza uzalishaji wa sukari nchini chini ya mpango wa Kilimo Kwanza na hivyo kuondoa tatizo la upungufu wa sukari nchini.

Mwisho

Thursday, February 24, 2011

‘Mkwe alininusuru kufa kwa mabomu’


Mzee Salum Mwinyi (kushoto) akifanya mahojiano na mwandishi wa makala haya, Joachim Mushi nyumbani kwake eneo la Majohe Kichangani hivi karibuni. (Picha na mdau Dotto Mwaibale)


‘Mkwe alininusuru kufa kwa mabomu’
*Niling’ang’ania ndani kutokana uzee

Na Joachim Mushi

YAWEZA ikawa inashangaza na wengine huenda hata wasiamini, lakini ndivyo ilivyokuwa. Mwanadamu unapoikimbia ajali hutokewa na nguvu za ghafla tena za ajabu ambazo zaweza kukusukuma kufanya mambo ambayo huwezi yafanya katika mazingira ya kawaida.

Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Salum Mwinyi kikongwe wa miaka tisini ambaye licha ya kutoweza kutembea kutokana na umri wake mkubwa na matatizo mengine, alipata nguvu za ajabu kukimbia hatari ya kifo. Hatari hii ilikuwa milipuko ya mabomu iliyotokea usiku wa Februari 16/17 mwaka huu kwenye kambi ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) kikosi namba 511 cha Gongo la Mboto.

“Namshukuru sana mkwe wangu (mke wa mtoto wake) naomba Mungu amjalie aweze kuishi maisha marefu, maana bila yeye nahisi muda huu nisingelikuwepo…ningelikuwa ni marehemu aliyeuawa kwa mabomu…ama kweli Mungu mkubwa,” anasema mzee Mwinyi huku akiwa amenyanyua mikono juu kuonesha ishara ya kumshukuru Mungu.

Mzee huyu anaonekana mchangamfu. Sijui kama ndivyo alivyo ama amekuwa mchangamfu baada ya kunusurika katika milipuko ya mabomu hayo. Nasema hivyo maana sikupanga kufanya mahojiano naye nilipomkuta, lakini nilijikuta nafanya hivyo baada ya maneno yake kunishawishi.

Anaishi nyumbani kwa mtoto wake wa kiume, Mkaeje Salum. Nyumba ya familia hii iliyopo eneo la Majohe Kichangani ni miongoni mwa majengo yaliyojikuta yakiangukiwa na mabomu yaliyokuwa yakilipuka bila mwelekeo. Hii imepigwa mabomu matatu.

Haijateketea yote lakini sehemu kubwa ya paa limefumuliwa na mabomu yaliyoelekea katika nyumba hiyo, yameangukia kwenye vyumba vitatu vya jengo hili. Viwili hutumika kulala na kimoja ndicho anacholala mzee Mwinyi. Yaliangukia kwenye vitanda. Vitanda vimeharibika vibaya.

Mzee Mwinyi anasema baada ya kusikia mlipuko wa kwanza wa bomu hakuamini kama kweli lilikuwa ni bomu. Walianza kubishana na mkwe wake pamoja na wajukuu wake. Yeye aliamini kishindo hicho kilikuwa ni kupasuka kwa gurudumu la gari (pancha imepasua gurudumu na kutoa mlio).

Anasema mtoto wake, Mkaeje alimuunga mkono. Naye aliamini huenda ni mlio wa kupasuka kwa gurudumu. Milipuko ya kishindo iliyofuatia ndiyo iliyomaliza mvutano kimabishano kati yake, mtoto wake na mkwe wake. Waliungana na wengine kisha kuamini yalikuwa ni mabomu.

Maana walishuhudia mwanga mkubwa wa moto ukiangaza maeneo ya jeshi. Milipuko iliendelea huku ikisafiri angani na moto ukiwaka. Anasema ilikuwa ni hatari. Aliamini ni mabomu. Kila mmoja akaanza kutafuta namna ya kujinusuru. Mzee huyu amechoka kiumri, miguu yake haina nguvu za kutembea sawia.

Mtoto wake na mkewe waligawana watoto ili waweze kukimbia nao kuwanusuru na mabomu ambayo muda huo yalionekana kusafiri angani na kuanguka ovyo baadhi ya maeneo. Mzee Mwinyi alishikwa mkono na mkwewe akimuongoza na watoto ili wakimbie.

Haikuwa raisi maana aligoma kabisa kwa madai hana nguvu za kukimbia alishauri apewe mjukuu wake mmoja abaki naye ndani kwani ni salama. Mkwewe alikataa na kuendelea kumsii waondoke kujinusuru.

Baada ya kuona anapingwa huku milipuko ikiendelea kwa zamu aliamua kukimbilia ndani kwenye chumba anacho lala. Mkwewe na wengine walianza kukimbia, hatua chache mama yule aligeuka nyuma akifikiri mzee Mwinyi wapo pamoja. Hapana alikuwa amerudi ndani ya nyuma.

Mama yule akiwa watoto wake alimfuata na kumtoa kwa nguvu. Alimshika mkono na kuanza kuondoka naye kana kwamba anamkokota, hapo hapo alikuwa na watoto wake wengine njia moja. Msafara wao haukudumu. Ulitawanywa na kishindo kikubwa kingine cha bomu.

Walianguka chini karibu wote na walipoinuka alijikuta peke yake. Ilikuwa ni mshikemshike kila mmoja alikimbia anapopajua. Hakumuona wala kumkumbuka mkwewe. Alijikuta akipata nguvu na kuanza kukimbia mwenyewe na makundi ya watu waliokuwa wakikimbia kunusuru maisha yao.

Anasema hakujua anakokwenda muda huo zaidi ya kufuata mkumbo wa watu. Hajui nguvu za kuweza kukimbia alizipata wapi, lakini safari iliendelea. Alijikuta akikimbia na kutembea toka majira ya saa mbili usiku hadi saa kumi asubuhi. Haelewi nguvu zilitoka wapi.

Anasema alikimbia kwa kufuata mkumbo hadi saa kumi za asubuhi ambapo alijikuta amefika eneo la Kigogo Freshi. Alikuwa amechoka sana na japokuwa hakusikia maumifu sehemu yoyote usiku huo. Labda kwasababu ya woga, haijulikani.

Baada ya kufika eneo hilo na kutulia kwa muda alipata kumbukumbu kuwa alikuwa ameongozana na mkwewe pamoja na baadhi ya wajukuu zake, muda huo hakujua walitengana vipi. Roho ilimuuma sana maana hakujua kama ni wazima au la.

“Nilikuwa na usingizi mzito lakini zikuweza kulala kabisa muda wote niliwakumbuka mkwe wangu na wajukuu nimewaacha wapi, roho iliniuma na kujikuta nakosa usingizi japokuwa tulikuwa tumepumzika eneo hilo muda mrefu na wengine wakiwa wamejipumzisha,” anasema Mwinyi.

Mzee Mwinyi ambaye ni mstaafu wa Shirika la Reli nchi (TRC sasa TRL) anasema alikuja kukutana na ndugu zake mchana baada ya siku ya milipuko. Wote wamesalimika. Nyumba yao wameikuta imeshambuliwa na mabomu ambayo yamebomoa sehemu kubwa ya paa la nyumba hiyo.

Na kibaya zaidi ni kwamba chumba ambacho alikuwa anaking’ang’ania abaki kutokana na hali yake kimepigwa bomu ambalo limeangukia kitanda chake na wajukuu zake huku kikiwa kimeharibiwa vibaya. Na endapo asingelitolewa kwa nguvu na mkwewe huenda angelikuwa marehemu sasa.

“Ndiyo maana kila siku nikiangalia nyumba yetu ilivyoshambuliwa namshukuru sana mkwe wangu…maana alininusuru na mabomu kwa kiasi kikubwa,” anasema Mwinyi.

“Cha ajabu sasa ndiyo naanza kusikia maumivu ikiwa ni siku moja baada ya milipuko hiyo. Wananikanda miguu sina nguvu za kutembea tena kama ilivyokuwa siku ya milipuko,” anasema mzee Mwinyi anayetembea kwa msaada wa fimbo kutokana na umri wake mkubwa.

Anasema fimbo yake inayomsaidia kujikongoja siku zote imenyooka, lakini sasa imepinda kutokana na mikiki mikiki aliyokumbana nayo akiwa anakimbia kujinusuru. Naongeza ukiadisiwa waweza usiamini, lakini hali ilikuwa ngumu siku hiyo ya milipuko.

Anaeleza kuwa hawezi kulilalamikia JWTZ hata siku moja kwa tukio la siku hiyo. Anaamini ilikuwa ajali hata wao wasingependa itokee kabisa. “Nasema kile ni kifo…usiombe kabisa mtu hawezi kufanya kitu kama kile kwa makusudi, labda kama hajipendi hii ni ajali haipangwi,” anasema Mzee huyo ambaye ni miongoni mwa watu walionusurika katika milipuko hiyo ya mabomu.

0717030066, 0756469470, barua pepe: jomushi79@yahoo.com


Rais Kikwete akutana na Rais Kabila


Rais Jakaya Kikwete akifanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Jeseph Kabila.  

Rais Kikwete ziarani Ivory Coast


Rais Jakaya Kikwete akipokelewa na kiongozi wa upinzani wa Ivory Coast Alassane Ouattara baada ya kuwasili nchini humo. (Picha na mdau Freddy Maro)



Rais Jakaya Kikwete akiwa na kiongozi wa upinzani wa Ivory Coast Alassane Ouattara (Katikati) pamoja na Rais wa Chad Idriss Deby (kulia) muda mfupi baada ya kumaliza mazungumzo ya upatanishi katika hoteli ya Golf iliyopo Abidjan (Picha na mdau Freddy Maro)


Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Bunge yatembelea Gongo la Mboto


Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Bunge, Edward Lowassa akiagana na Mkuu wa Majeshi ya Ulizi na Usalama, Davis Mwamunyange.


Waziri wa Ulinzi, Dk. Hussein Mwinyi (kulia) akiwa na baadhi ya maofisa wa juu wa Jeshi la Wananchi Tanzania, wapili kulia baada ya waziri ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Davis Mwamunyange.



Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, aliyesimama akimkaribisha Spika wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda, alipotembelea kituo cha kupokelea misaada kwa waathirika wa milipuko ya mabomu Gongo la Mboto.

Monday, February 21, 2011

Mabomu yalivyoitetemesha Dar es Salaam

Februari 16/17 huenda ikabaki historia ya pekee dhidi ya tukio la milipuko ya mabomu yaliyotokea katika Kikosi namba 511 cha Jeshi la Wananchi (JWTZ) kilichopo eneo la Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam.
Zifuatazo ni baadhi ya picha zikionesha namna wakazi wa maeneo ya Jiji la Dar es Salaam, hasa Gongo la Mboto walivyoathiriwa na mabomu siku hiyo na siku iliyofuatia.




Baadhi ya wananchi akiyakimbia maeneo ya milipuko siku ya kuamkia milipuko ya mabomu, wakihofia maeneo hayo si salama tena. Hata hivyo tetesi za uwongo ndiyo kilichoendelea kuyakimbia maeneo hayo, baadhi ya vibaka waliwaongopea wakazi kuwa yangelipuka mengine baadaye.



Watu walilazimika kubeba kile walichoweza na kutembea kwa muda mrefu. Hata hivyo ungelibahatika kumuuliza mmoja wao kuwa alikuwa akielekea wapi hawa kuwa na jibu zaidi ya kusema "hatujui"



Uwanja wa Uhuru ghafla ulibadilika na kuwa kambi ya kuwahifadhi 'wakimbizi' wa muda wa makazi yao, hawa waliopangwa na kukaa chini ni watoto zaidi ya mia 400 ambao walipotezana na wazazi wao. Uwanja huo ulipokea zaidi ya watu 4000 kwa siku moja.



Viongozi wa Kuu wa nchi kesho yake ya siku ya milipuko yaani Februari 17 walilazimika kuyatembelea eneo la Jeshi lililotokewa na milipuko hiyo, pichani ni Rais Jakaya Kikwete (aliyevaa miwani) akiwa na Mkuu wa JWTZ, Davis Mwamunyange alipokitembelea kikosi 511 ilipotokea milipuko.



Mabaki ya mabomu yalizagaa mitaani kwenye makazi ya watu, magari ya jeshi na polisi walilazimika kupita na kuyakusanya moja baada ya lingine. Gari likiwa limepakia shehena ya baadhi ya mabomu. Picha zote na mdau wa Harusi na Matukio. 

Wednesday, February 9, 2011

Wabunge wa Chadema watoka Bungeni tena


Wabunge wa Chadema wakiongozwa na Freeman Mbowe kutoka nje ya Bunge huku kikao kikiendelea



Wabunge hao wakitokomea nje baada ya kuzira kupitisha mabadiliko ya kanuni ya 15(2) tafsiri ya Kambi Rasmi ya upinzani bungeni. Habari kamili chini.


WABUNGE wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe jana walitoka tena nje ya ukumbi wa Bunge Ukumbi ya Bunge wakipinga azimio la kuondoa utata wa tafsiri ya Kanuni ya Bunge inayotaka chama chenye asilimia 12.5 ya wabunge wote kuunda kambi rasmi ya upinzani.

Mabadiliko hayo ya jana yanainyima Chadema kwa mujibu wa kanuni ya 15(2) tafsiri ya Kambi Rasmi ya upinzani bungeni sasa ni kambi inayoundwa na vyama vya upinzani vinavyowakilishwa bungeni.

Hata hivyo, bado Chadema kwa mujibu wa Kanuni za Bunge ndicho kitakachotoa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni na naibu wake. Pia kiongozi huyo ana mamlaka na uhuru wa kuteua Baraza la Mawaziri Kivuli kutokana na wabunge wa upinzani waliopo.

Azimio hilo linaondoa dhana iliyokuwepo kwamba Chadema ndicho kingetoa wenyeviti wa Kamati za Hesabu za Serikali ambazo kwa mujibu wa Kanuni za Bunge zinatakiwa kuongozwa na wapinzani.
Tofauti na ilivyokuwa ikifahamika awali, mabadiliko ya jana yanatoa fursa kwa mbunge yeyote wa upinzani kugombea nafasi hizo bila kuhitaji idhini ya  uongozi wa kambi ya upinzani.

Tukio la Chadema kutoka nje ya Bunge linafanana na lile la  Novemba 18, mwaka jana, ambapo wabunge hao walitoka baada ya Rais Jakaya Kikwete kuanza hotuba ya uzinduzi wa Bunge.

"Madamu Bunge limeona busara kuleta hoja hii, na vijembe vile, kwa masikitiko nasema hatutashiriki kumalizia hoja hii, naomba kutoa hoja," alisema Mbowe na kuanza kutoka nje akifuatiwa na wabunge wa chama hicho.

Wakati wabunge wa Chadema wakitoka nje, wabunge waliobaki wengi, walisikika wakitoa maneno ya kebehi dhidi ya wabunge Chadema. "...tumewazoea kukimbia, kwisha, uchoyo, weak politicians, na kwenye posho msije, mnadaiwa na mabenki," walisikika wabunge hao.

Mwisho.

Malangalarini Sec. yapewa msaada wa gari na diwani



Mkurugenzi wa Mipango Miji Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Blandina Bura akimkabidhi Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mlangarini, Elisa Pallangyo funguo za gari aina ya Hiace-Super Custom lenye thamani ya sh. mil 18 lilitolewa na Diwani wa Kata hiyo, Mathias Manga kwa ajili kusaidia shughuli mbalimbali za shule hiyo juzi wilayani Arumeru mkoani Arusha, PICHA NA MDAU JANETH MUSHI


Saturday, February 5, 2011

Maadhimisho miaka 34 ya CCM

Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, akiwapungia mkono wanachama wa CCM wakipita mbele ya jukwaa kuu na maandamano katika uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, wakati wa kilele cha sherehe za miaka 34 ya kuzaliwa CCM. Wengine kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, William Kusila, Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba (watatu kushoto) na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete. 


Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Jakaya Kikwete, akiwahutubia wananchi wakati wa kilele cha sherehe hizo za miaka 34 ya kuzaliwa CCM zilizofanyika mjini Dodoma. Picha zote na mdau Fredy Maro

Thursday, February 3, 2011

JK ana kwa ana na Mbowe

Jk akisalimiana na Mbowe

WANASEMA mpinzani wa kisiasa si ugomvi japokuwa kwa upande wa wanachama huwa ni tofauti kwa upinzani wa vyama. Viongozi wa juu wao wanapokutana husahau yote ya nyuma na kufanya shughuli zao kama kawaida tena kwa fura.

Ndivyo ilivyoonekana Februari 2 jijini Dar es Salaam baada ya Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM kukutana na mpinzani wake mkumbwa kisiasa Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe kwenye sherehe za maadhimisho ya siku ya Sheria nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo Rais Kikwete aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Mahakama Kuu.

Aliwataka watumishi wa mahakama kutambua kuwa mahakama zimewekwa kwa ajili ya kuwatumikia wananchi, hivyo wanatakiwa kutenda yale yanayostahili ikiwa ni pamoja na kutenda haki.

“Kuna fununu zimekuwa zikienea kuwa katika tasnia hii kuna vitendo vya rushwa vilivyokithiri, lakini iwapo mtafabya kazi kwa uadilifu na kwa kujali maslahi ya wananchi basi malalamiko hayo yataisha kwani haki itakuwa imetendeka,” alisema Rais Kikwete.

Alisema uamuzi wa mahakama ni wa mwisho hauwezi kutenguliwa na yeyote nchini. “Mara kadhaa nimekuwa nikipokea malalamiko na maombi ya msaaada kutoka kwa waliohukumiwa kesi mbalimbali, wengi wamekuwa wakidhani kuwa mimi nina uwezo wa kutengua kilichotolewa na mahakama jambo ambalo si kweli. Na mara nikiwajibu kuwa siwezi kufanya hivyo, huwa wananieleza kuwa sio kweli na kwamba wanaamini kuwa nimeshindwa kufanya kazi,” alisema Rais Kikwete


Rais Jakaya Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na jopo la majaji, Akiwemo Spika wa Bunge Anna Makinda na Waziri wa Sheria na Katiba, Selina Kombani.

Wednesday, February 2, 2011

Maadhimisho ya miaka 34 ya CCM


Moja ya vikosi vya umoja wa vijana wa CCM wakicheza paredi katika maadhimisho ya miaka 34 ya chama hicho.


Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Visiwani, Amani Abeid Karume (wa tatu kulia mbele) akipokea salamu za heshima zilizotolewa na kikosi cha vijana cha CCM, katika maadhimisho ya miaka 34 ya CCM.



Vijana wa UVCCM wakila kiapo mbele ya viongozi wao wa chama taifa, katika maadhimisho ya miaka 34 ya CCM.


Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba (kushoto), akibadilishana mawazo na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara, Pius Msekwa katika maadhimisho ya miaka 34 ya Chama Cha Mapinduzi, Viwanja vya Biafra Dar es Salaam. Picha zote na Mdau Dotto Mwaibale.




SEIF SHARIFF HAMAD AKIRI KUWA YEYE NI BABU KIZEE.

Seif Shariff Hamad Seif Shariff Hamad KWA mara ya kwanza Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Seif Shariff Hamad amek...