Tuesday, February 27, 2018

Shirika la TTCL lazinduwa huduma ya 'Fiber Connect Bundle'

Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL Corporation, Bw. Waziri Kindamba akizungumza katika uzinduzi huo.


SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL CORPORATION) limezinduwa rasmi huduma mpya inayojulikana kama 'Fiber Connect Bundle' inayokwenda pamoja na kauli mbiu ya "Rudi nyumbani, kumenoga" kuchagiza uzinduzi huo.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL Corporation, Bw. Waziri Kindamba alisema huduma hiyo ni mwendelezo wa ubunifu wa kampuni ya kizalendo katika kuwapatia Watanzania huduma za kipekee, nafuu na zenye ubora wa hali ya juu.

Bw. Kindamba alisema TTCL Corporation imedhamiria kuwafuata wateja nyumbani na kufanya mapinduzi makubwa ya kimawasiliano hasa ya mtandao wa intanenti yenye kasi ya juu.

Alisema kupitia huduma hiyo mpya ya Fiber Connect Bundle, wateja wao watapata huduma nne kwa pamoja zikiwa na unafuu mkubwa wa gharama na ubora wa hali ya juu ukilinganisha na mitandao mingine ya simu.

Bw. Kindamba amefafanua huduma kwa kuanzia wanatarajia kuzifikia nyumba 500 katika maeneo ya Mikocheni na nyumba nyingine 500 katika eneo la Mbezi Beach jijini Dar es Salaam pamoja na nyumba 200 eneo la Medeli mkoani Dodoma.

Aidha aliongeza kuwa baada ya hapo wataendelea na maeneo mengine kwani lengo lao ni kuhakikisha kila mahali katika nchi yetu kunakuwa na huduma za mawasiliano ya Shirika hilo hasa kwa kuzingatia wao ndio wanaousimamia mkongo wa Taifa wa mawasilano.

Kindamba amesema kupitia kifurushi cha Fiber Connect, mteja wao atanufaika na huduma mbalimbali ikiwamo ya  kupata intanenti yenye kasi isiyo na kikomo (Unlimited). Pia mteja atapata huduma ya simu za sauti kwa simu za mezani na simu card ambayo ataitumia kwenye simu yake ya mkononi na kupata huduma ya Intanenti sawa na simu ile anayopata katika simu ya mezani.

Ameongeza kuwa mteja wao pia atapata huduma za Wireless Service (WIFI) katika nyumba yake ambapo vifaa vyote vinavyotumia teknolojia ya intaneti vitaunganishwa  ili kutumia kutumia huduma hiyo.

Ametoa mfano kuwa huduma ambayo wameizundua mteja anaweza kuunganisha kwenye Smart Tv, Tablets na kompyuta mpakato.Pia mteja atapatiwa vifaa vyote bure na uhakika wa huduma za baada (After Sell Services) endapo itahitajika.

Amesema kuwa wamejipanga kuhakikisha wanaendelea kutoa huduma bora kwa ajili ya Watanzania ambao kimsingi shirika hilo ni mali yao na wanatakiwa kuunga mkono jitihada hizo.

“Tumeendelea kujipanga ili kufikia malengo yetu ambayo kimsingi ni kuwatumikia Watanzania kwa kiwango bora katika eneo la mawasiliano na kwa gharama nafuu,” amesema Bw. Kindamba.

Akizungumzia shirika hilo, Kindamba amesema, Februari moja mwaka 2018, Shirika la Mawasiliano Tanzania lilizaliwa kwa sheria ya Shirika la Mawasiliano Tanzania Na. 12 mwaka 2017. Amesema kwa sasa shirika hilo limechukua sura  ya iliyokuwa Kampuni ya Simu Tanzania( TTCL),  ambayo shughuli zake ziliisha Januari  31 mwaka 2018.

Amemshukuru Rais, Dk. John Magufuli kwa kuona umuhimu wa kuwa na Shirika madhubuti la mawasiliano la Taifa kwa maslahi mapana ya Taifa. Pia amemshukuru kwa kuendelea kuonesha imani kubwa kwa uongozi wao.

No comments:

Post a Comment

SEIF SHARIFF HAMAD AKIRI KUWA YEYE NI BABU KIZEE.

Seif Shariff Hamad Seif Shariff Hamad KWA mara ya kwanza Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Seif Shariff Hamad amek...