MTANDAO wa wanawake na katiba/uchaguzi na uongozi leo umekutana na wahariri wa habari na waandishi waandamizi kujadiliana masuala mbalimbali juu ya umuhimu wa kuzingatia misingi na usawa wa kijinsia katika siasa na uongozi nchini.
Akiwasilisha mada kwa wahariri na wanahabari waandamizi katika mkutano huo, mtoa mada na mjumbe wa WFT, Dk. Dinah Richard Mmbaga aliwataka wanahabari kuangalia mfumo mzima wa siasa za vyama vingi na nini kinachoitenganisha siasa ya Tanzania na nchi nyingine bila kujali tofauti za itikadi za vyama kwenye masuala yanayohusu utu wa mwanamke, ushiriki wa mwanamke kuchangia fikra za siasa na uongozi.
Aliwataka kuchambua na kuangalia mambo yapi yatakayounganisha wanasiasa wote katika kutetea masuala ya kitaifa ikiwa ni pamoja na utu na haki za mwanamke na pia mfumo wa uongozi utakaowezesha vyama vya siasa kuimarisha demokrasia shirikishi yenye mrengo wa jinsia ndani ya vyama.
Pia kuchambua mfumo wa uongozi unaowezesha vyama kutatua migogoro ndani ya vyama vyao bila kutumia vitisho, na hususani vinavyoashiria kumsababisha mwanamke wa Tanzania asipende kushiriki katika shughuili za siasa au anaposhiriki ajisikie yuko salama.
Kwa upande wake Mjumbe wa Wanawake na Katiba/uchaguzi na uongozi, Bi. Laeticia Mukurasi akizungumza katika majadiliano hayo, alisema malengo ni kujadili kwa pamoja umuhimu wa kuzingatia misingi ya usawa wa jinsia katika masuala ya siasa na uongozi nchini nchini.
Kujenga makubaliano ya pamoja jinsi waandishi wa habari watakavyochechemua umuhimu wa kuzingatia misingi ya jinsia kwenye masuala ya siasa na uongozi katika majukumu yao, na kujengeana uwezo wa masuala ya usawa wa jinsia na uongozi kwa ujumla.
Baadhi ya washiriki katika mkutano wa Mtandao wa wanawake na katiba/uchaguzi na uongozi pamoja na wahariri wa habari na waandishi waandamizi wakifuatilia mijadala anuai katika mkutano huo. |
No comments:
Post a Comment