Thursday, June 9, 2011

Mkulo asoma bajeti ya Serikali 2011/2012; daladala, wapenda starehe kuumia

Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo

BAJETI ya fedha ya mwaka 2011/2012 imeonesha kutoa matumani makubwa kwa mwananchi wa kawaida kutokana na dhamira ya Serikali kupunguza ukali wa maisha huku ikitangaza vipaumbele vyake ni umeme, maji, miundombinu, viwanja vya ndege, kuinua kilimo cha umwagiliaji na kupanua ajira.
 
Katika bajeti hii mpya Serikali inatarajia kutumia zaidi ya trilioni 13.5 ikiwa ni kiasi kikubwa zaidi ya ile ya mwaka 2010/2011 ambapo ilitumia trilioni 11.1; bajeti ambayo ilipingwa na wabunge wa upinzani jambo ambalo halikufua dafu dhidi ya uwingi wa wabunge wa chama tawala.

Akisoma bajeti hiyo jana bungeni mjini Dodoma, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo alisema kiujumla bajeti imelenga kupunguza ukali wa maisha kwa Mtanzania, kwa kuangalia kodi na tozo ambazo zimekuwa zikichangia kupanda kwa gharama za vitu mbalimbali muhimu.

“Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia sera za uchumi pamoja na misingi na sera za bajeti, sura ya Bajeti inaonesha kwamba jumla ya shilingi bilioni 13,525.9 zinahitajika kutumika katika kipindi cha 2011/12.

 Alisema Serikali inatarajia kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ya jumla ya sh. bilioni 6,775.9, sawa na asilimia 17.2 ya Pato la Taifa. Aidha, mapato kutoka vyanzo vya Halmashauri ni sh. bilioni 350.5. Kadhalika, kukopa kiasi cha sh. bilioni 2,475.9…,” alisema Mkulo.

Alisema kutoka kwa washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia bajeti kupitia misaada na mikopo ya jumla ya sh. bilioni 3,923.6. na kati ya fedha hizo, sh. bilioni 869.4 ni misaada na mikopo ya kibajeti huku sh. bilioni 3,054.1 ni misaada na mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ikijumuisha mifuko ya kisekta.

Katika bajeti hiyo pamoja na mambo mengine, Serikali imeendelea kuwakamua watumiaji sigara na bia kwa kuongeza kodi ukilinganisha na ile ya mwaka wa fedha uliopita; huku kwa watakaofanya makosa ya barabarani sasa kutakiwa kulipa sh. 300,000 badala ya sh. 20,000.
 
“Kumekuwepo na changamoto ambazo zinahitaji hatua za maksudi kuchukuliwa na wadau ikiwemo Serikali, sekta binafsi na mwananchi mmoja mmoja ili kupunguza makali ya maisha kwa mwananchi.
 
“Kasi ya ongezeko la bei za bidhaa na huduma nchini pamoja na mambo mengine inasababishwa na kuongezeka kwa bei za mafuta katika soko la dunia. Kutopatikana kwa umeme wa uhakika nalo ni tatizo lingine pamoja na upungufu wa chakula nchini. Hivyo Serikali itachukua hatua za kukabiliana na hiyo,” alisema Mkulo.
 
Akifafanua namna ya kupunguza ukali wa maisha Mkulo alisema bajeti ya mwaka wa 2011/2012 imeangalia maeneo mbalimbali muhimu na kuyafanyia marekebisho kwa maslahi ya Taifa ambapo, ili kupunguza bei ya mafuta, Serikali imeamua kufanya mapitio ya namna ya kuondoa tozo zinazotozwa na mamlaka mbalimbali kwa lengo la kupunguza kodi.
 
Waziri Mkulo alisema Serikali inakamilisha taratibu za ununuzi wa mafuta kwa wingi kwa lengo la kuyauzia kampuni ya usambazaji kwa bei ya jumla kufanya yatakavyo. Kanuni zitatoa muongozo katika uagizaji mafuta kwa pamoja zimekamilika na utaratibu huo unategemea kuanza kati kati ya mwaka wa fedha wa 2011/2012.
 
“Utaratibu huu unatarajiwa kupunguza bei na gharama za usafirishaji wa mafuta hayo. Pamoja na juhudi hizi za Serikali, sekta binafsi inahimizwa kuwezesha upatikanaji wa huduma ya kutumia gesi kama nishati mbadala wa mafuta ya petroli hasa mijini. Ni matarajia yangu hatua hizi zitaleta unafuu wa bei ya mafuta na hivyo kupunguza gharama za maisha,” alisema Mkulo.

No comments:

Post a Comment

SEIF SHARIFF HAMAD AKIRI KUWA YEYE NI BABU KIZEE.

Seif Shariff Hamad Seif Shariff Hamad KWA mara ya kwanza Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Seif Shariff Hamad amek...