Tuesday, September 19, 2017

Namaingo Business Agency mradi mkubwa wa ufugaji kuku

Kampuni ya Namaingo Business Agency Co. Ltd imezindua Mradi mkubwa wa ufugaji kuku unaosimamiwa na Kikundi cha Ujasiriamali cha Shinyanga, Kishapu na Kahama (SHIKIKA) uliopo katika mtaa wa Sanjo kata ya Chamaguha katika manispaa ya Shinyanga.

Uzinduzi wa mradi huo umefanyika Septemba 18, 2017 katika mtaa wa Sanjo kata ya Chamaguha Manispaa ya Shinyanga. Kikundi cha SHIKIKA kinachotekeleza mradi huo, kilianzishwa Machi 16, 2017 baada ya kampuni ya Namaingo Business Agency Co. Ltd kuwaelekeza wanachama wake kuunda vikundi vya wanachama hamsini hamsini ili wakubaliane kuendesha mradi wanaoupenda.

Wanakikundi hao waliamua kuanzisha mradi wa ufugaji wa kuku wa kienyeji ndipo kampuni hiyo ikawachangia vifaranga 200, wakaanza ufugaji tarehe 9. 6. 2017 na mpaka sasa kikundi kina kuku zaidi ya 1300.

Akizungumza wakati wa kuzindua mradi huo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Namaingo Business Agency Co. Ltd, Biubwa Ibrahim aliwapongeza wanakikundi hao kwa kuchangishana fedha shilingi milioni 8 na kuamua kuanzisha mradi huo.

“Ndugu zangu jambo hili mlilofanya na mlilolitekeleza kwanza ni jambo la kitaifa kwa sababu wananchi wakiwa na uchumi mzuri serikali nayo inapata kodi lakini pia tunakuwa tumetengeneza ajira”, alisema Ibrahim.

“Pamoja na jitihada hizi mlizochukua kwa muda mfupi, Tunatamani kuona kila mtu anakuwa na kuku walau 1000 kwenye banda lake, najua changamoto kubwa iliyopo ni mitaji na riba kubwa kwenye mikopo lakini kuna fedha kwa ajili ya maendeleo ya akina mama na vijana zenye riba ndogo sana zipo kwenye benki mbalimbali, serikali inafanyia kazi suala la mikopo hiyo,” aliongeza.

Aidha Ibrahim aliwataka wananchi kuwa na maamuzi ya kutoka katika hali walizonazo kwa kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa na kuilaumu serikali.

“Hakuna haja ya kuilaumu serikali bali unapaswa kujiajiri ili kubadilisha maisha yako, hakuna maisha mazuri kama mtu ukijiajiri, hata hao waliojiriwa wakistaafu huwa wanarudi kujiajiri hivyo kujiajiri ndiyo kila kitu katika maisha yako”, aliongeza Ibrahim.

“Sisi Namaingo Bussiness Agency Co. Ltd kazi yetu ni kuwabadilisha kiakili ili muweze kubadilika kimawazo kwani fursa za kubadili maisha yenu,zipo nyingi,kufanikiwa kwa mtu ni maamuzi ya mtu mwenyewe”, alisema.

Akisoma risala, Katibu Msaidizi wa SHIKIKA, Beatrice Nangale alisema gharama za kuanzisha mradi huo ni shilingi milioni 8 lakini mpaka sasa umegharimu shilingi milioni 20 ambazo ni michango ya wanachama.

Alisema ili kufikia malengo yao, kundi hilo linahitaji eneo kubwa la ekari 3000 kwa ajili kupanua mradi wa kuku, kuwa na mashine za kutotolea, kutengeneza chakula cha kuku, kuchakata minofu ya kukuna ufugaji wa nyuki wa asali.

“Pia tunataka kufuga samaki, mbuzi, sungura na ng’ombe kisha kusindika nyama zao, kulima mboga mboga na matunda kama vile mapapai, kupanda miti na kujenga nyumba kwa ajili ya makazi”, alifafanua Nangale.

Hata hivyo alizitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili kuwa ni ukosefu wa chakula na dawa za kuku mjini Shinyanga, masharti magumu ya benki za utoaji mikopo, ukosefu wa wataalam wa masuala ya mifugo pamoja na kukosa wahisani na misaada ya wahisani kutokana na hali ngumu za kiuchumi za wanakikundi.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Chamaguha Deo Masalu alisema mradi huo utatumika kama shamba darasa na kuahidi serikali kuwapa ushirikiano wanachama wa kikundi ili kuhakikisha wanafikia malengo yao.


Mkurugenzi wa Kampuni ya Namaingo Business Agency Co. Ltd, Biubwa Ibrahim akijiandaa kukata utepe kwa ajili ya kuzindua mradi wa kuku unaosimamiwa na Kikundi cha Ujasiriamali kutoka Shinyanga, Kishapu na Kahama (SHIKIKA) Septemba 18, 2017. Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog 

Mkurugenzi wa Kampuni ya Namaingo Business Agency Co. Ltd, Biubwa Ibrahim akikata utepe.


Mkurugenzi wa Kampuni ya Namaingo Business Agency Co. Ltd,Biubwa Ibrahim akiangalia kuku wenye umri wa miezi miwili katika moja ya mabanda ya kundi la SHIKIKA.

No comments:

Post a Comment

SEIF SHARIFF HAMAD AKIRI KUWA YEYE NI BABU KIZEE.

Seif Shariff Hamad Seif Shariff Hamad KWA mara ya kwanza Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Seif Shariff Hamad amek...