Katika zoezi hilo, TTCL imekabidhi mashuka 100, Vyandarua 100, Maboksi ya dawa mbalimbali pamoja na vifaa tiba ili kukabiliana na changamoto anuai zinazokikabili kituo hicho kwa ajili ya kuwahudumiwa wakazi wa maeneo hayo kiafya.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi vifaa hivyo, Meneja Uhusiano wa kampuni ya TTCL, Nicodemas Mushi alisema zoezi hilo ni mwendelezo wa kampuni hiyo katika kurejesha faida kwa wananchi ambao ni wateja wa kampuni hiyo. Alisema wanaamini msaada huo unaenda kuwahudumia wananchi ambao ndiyo wateja wa kuu wa huduma za TTCL.
"...Vifaa hivi vinakwenda kuwatibu wananchi ambao tunaamini ni wateja wetu, hivyo wakiwa na afya njema ndiyo furaha kwetu na kuendelea kushirikiana nao kihuduma. Huu ni utaratibu wetu wa kawaida kila tunapopata kidogo tunakirudisha kwa wananchi...leo tumetoa mashine, mashuka 100, vyandarua 100 na dawa ambazo zitasaidia kuboresha huduma kwa wateja wetu," alisema Meneja huyo wa TTCL.
Alisema wanatambua mchango mkubwa unaotolewa na kituo hicho cha afya na hasa kuwahudumia wagonjwa wa kipindupindu ugonjwa ambao umekuwa changamoto kwa jiji la Dar es Salaam.
Kwa upande wake, Ofisa Muuguzi Mkuu wa Kituo cha Afya cha Buguruni, Alvera Mtembelea ameishukuru kampuni ya simu Tanzania kwa ukarimu wao na kuamua kukisaidia kituo hicho kwani wamesaidia kutatua changamoto anuai zinazokikabili kituo hicho katika kutoa huduma za afya. Aliomba makampuni mengine kufuata nyayo za TTCL kusaidia kutatua changamoto za huduma za afya katika vituo vya afya na hospitali anuai kulingana na mahitaji ya maeneo husika.
Kituo cha afya cha Buguruni ambacho leo kimenufaika na msaada huo ndicho kilichoteuliwa katika eneo hilo kuwahudumia wagonjwa wa kipindupindu ugonjwa ambao ulilipuka hivi karibuni kwa baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam na ambapo madhara yake yaliziathiri baadhi ya jamii jijini hapa.
No comments:
Post a Comment