Wakazi wa vijiji vilivyopo kandokando ya mto Ruvuma wilayani Nyasa mkoani Ruvuma na wafanyakazi wa Bobari ya Dawa (MSD), wakisaidia kushusha maboksi yenye dawa na kuyaingiza kwenye mtumbwi baada ya kupelekewa na MSD Kanda ya Iringa leo na baadae kuyapeleka katika Zahanati ya Kijiji cha Mitomoni.
Maboksi ya dawa yakiingizwa kwenye mtumbwi.
Wakazi wa Kijiji cha Mitomoni wakisubiri mtumbwi ili kuwavusha upande wa pili wa mto Ruvuma.
Dawa zikipelekwa Zahanati ya Mitomoni
Maboksi ya dawa kutoka MSD yakishushwa
Wananchi wakishusha maboksi hayo kutoka katika mtumbwi.
Mkazi wa Kijiji cha Mitomoni Khadija Salum, akizungumzia upatikanaji wa dawa kutoka MSD.
Mkazi wa kijiji hicho, Mbwana Koloma, akizungumzia changamoto ya miundombinu ya barabara na jinsi wanavyopokea dawa kutoka MSD.
Mwenyekiti wa kamati ya Afya wa Kijiji cha Mitomoni Omar Hassan akizungumza wakati wa kupokea dawa hizo.
Mmoja wa viongozi wa Kijiji cha Nakawale, Ima Komba akisaini fomu maalumu ya kupokelea dawa kutoka MSD.
Na Dotto Mwaibale, Ruvuma
WANANCHI wanaoishi katika Vijiji vya Mkenda na Mitomoni vilivyopo kandokando ya mto Ruvuma wilayani Nyasa mkoani Ruvuma wamesema changamoto kubwa waliyonayo ni
mazingira magumu ya miundo mbinu ambayo inasababisha ugumu wa ufikishaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kutoka Bohari ya Dawa (MSD).
Wakazi hao wamesema kuwa, mazingira ya kufikisha dawa kwenye vijiji hivyo hutegemea zaidi usafiri wa kuvuka mto Ruvuma ambapo hulazimika kutumia boti,ambapo hata hivyo maisha yao yanakuwa na mashaka ndani ya mtumbwi hiyo ambayo iko wazi kutokana na mto huo kuwa na mamba wengi.
"Changamoto yetu kubwa ni usafishaji wa dawa kuja hapa kijijini kutokana na kutegemea zaidi mto huu ambao una mamba wengi, hata mwaka huu mwanzoni mtumbwi huu mnaouona ulipinduka na watu wakiwapo wauza mitumba waliuawa na mamba; lakini tunashukuru Bohari ya Dawa (MSD) kwani wao wanaweza kutuletea dawa kwa wakati" alisema Mwenyekiti wa kamati ya Afya wa kijiji cha Mitomoni Omar Hassan.
Alisema ili kuondoa changamoto hiyo, wanaiomba serikali kuhakikisha inaboresha miundombinu ya barabara, ili dawa hizo zisafirishwe kwa njia ya barabara badala ya kutegemea mto huo.
Alisema yeye na kamati yake wamekuwa wakipokea dawa mara nne kwa mwaka kutoka MSD na kuzihakiki kwa ajili ya matumizi.
"Pamoja na changamoto ya miundombinu lakini tumekuwa tukihakikisha dawa zinazoletwa na MSD zinafika kituoni na kutumika ipasavyo,"alisema.
Alisema kutoka Songea mjini hadi Kijiji cha Mitomoni, Songea vijijini, katika kituo hicho cha afya ni km 135 na MSD imekuwa ikihakikisha dawa hizo zinafika.
Alisema changamoto zinakuwa kubwa zaidi kipindi cha mvua kwa kuwa miundombinu ya barabara hadi kufika kivukoni ni tatizo na kuna wakati dawa zinafika usiku na zinatakiwa kuvushwa usiku huo huo.
Hassan alisema changamoto hiyo ya mamba katika mto huo anaijua vizuri kwani mtoto wake Sanifu Omar (27), alipoteza maisha kwa kuliwa na mamba wakati alipokuwa akisafirisha abiria kwa kutumia mtumbwi.
Mkazi wa Kijiji cha Mitomoni Khadija Salum alisema wamekuwa wakipata dawa zote muhimu katika kituoni hicho ikiwemo za mama mjamzito na mtoto bila ya ubaguzi na kwa wakati.
"Mimi nina watoto watano kuanzia ujauzito wa kwanza sijawahi kukosa dawa hapa pamoja na ugumu wa miundombinu lakini dawa zinafika hivyo serikali ione haja ya kuboresha barabara zetu," alisema.
Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Mitomoni, Ivo Hekela, alisema kijiji hicho kinahudumia agonjwa 12,000 kutoka vijiji vitano ambavyo ni Mitomoni, Mipotopoto,Konganywita,Mkenda,Uhuru na Mozambique.
Meneja wa MSD Kanda ya Iringa, John Sipendi, alisema wamekuwa katika changamoto ya kufikia vituo hivyo vya pembezoni ikiwa ni pamoja na kutumia muda mrefu kufikisha dawa na wakati wa mvua kukwama kwa magari njiani na gharama za usafirishaji kuogezeka.
Madereva wa MSD Kanda ya Iringa wamesema wamekuwa wakishindwa kushusha dawa wakati wa mvua za masika kutokana na mto huo kujaa maji hivyo hulazimika kulala kijijini hapo kwa siku mbili hadi tatu.
No comments:
Post a Comment