Wednesday, May 2, 2018

GGM na TACAIDS kuzinduwa Kilimanjaro Challenge 2018



















Na Mwandishi Wetu

MGODI wa Dhahabu wa Geita (GGM) kwa kushirikiana na Tume ya Kuthibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) inatarajia kuzindua zoezi la upandaji wa mlima Kilimanjaro (Kilimanjaro Challenge 2018), litakalo kwenda sambamba na kuendesha harambee kuchangisha fedha kwa mwaka 2018 kwa ajili ya afua za UKIMWI nchini. Akizungumzia tukio hilo kwa waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Dk. Leonard Maboko alisema shughuli hiyo itafanyika Mei 4, 2018 katika Hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro Dar es Salaam. Dk. Maboko alisema mgeni rasmi katika uzinduzi huo anatarajia kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa ambapo atafanya zozezi la ugawaji wa fedha zilizokusanywa mwaka 2017 baada ya wadau mbalimbali kupanda na kuendesha baiskeli kwa kuzunguzuka Mlima Kilimanjaro. Aidha aliishukuru na kuipongeza kampuni ya GGM kwa kuendelea kuwa mdau mkubwa wa kuchangisha fedha kupitia Kilimanjaro Challenge against HIV & AIDS, fedha ambazo alisisitiza zimekuwa na mchango mkubwa katika mapambano kudhibiti ugonjwa huo maeneo mbalimbali. Akifafanua zaidi, Dk. Maboko alisema Kilimanjaro Challenge against HIV & AIDS, ni mfuko unachangia juhudi za serikali katika mapambano dhidi ya UKIMWI na kutoa elimu kwa jamii kuhusu maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU). Aliongeza kuwa, Kilimanjaro Challenge ni mfuko muhimu unaoshirikiana na taasisi za nje na ndani ya nchi katika kuendeleza mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI kwa jamii ya Kitanzania na Dunia kwa ujumla ili kuwapa matumaini ya kuhakikisha jamii inabaki bila kuathiriwa na VVU/UKIMWI katika miaka ijayo. Mfuko huo pia unalenga kuisaidia Serikali kukabiliana na VVU//UKIMWI sambamba na kutoa nafasi kwa watalii wa ndani na nje kuupanda mlima Kilimanjaro. Takwimu zilizotolewa na Tume ya Kuthibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), zimeonesha kupungua kwa maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka asilimia 5.1 % mwaka 2011/ 2012 hadi asilimia 4.7% mwaka 2016/17. “Mwaka wa 2016, inakadiriwa kuwa watu milioni 1.5 nchini wanaoishi na VVU na UKIMWI hadi sasa watu 225 wanapata maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa siku. Ugonjwa huu umewaathiri zaidi vijana na watoto yatima zaidi. Tunahitaji kubadilisha hali hii. Lengo la kukusanya fedha ni kuweza kusaidia serikali ya Tanzania katika jitihada zake kufikia sifuri tatu. Sifuri katika maambukizi mapya, sifuri ya unyanyapaa, sifuri katika vifo vitokanavyo na UKIMWI." " TACAIDS kwa kushirikiana na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) na wadau wengine kwa kupitia mpango huu wa Kili Challenge tunapenda kutoa mchango na ushirikiano wetu kwa Taifa ili kutunisha mfuko utakaowezesha kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa huu. Tuna matumaini ya kujenga timu imara yenye hamasa ya kupambana na janga hili. Tunatoa wito kwa makampuni na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi, wajitokeze ili tusaidiaane kutunisha mfuko wa Kili Challenge na mwishowe kufikia malengo yetu ya kuhakikisha tunakuwa na kizazi kisicho na maambukizi ya VVU/ UKIMWI,” alisema Dkt. Leonard Maboko. Naye Makamu wa Rais miradi endelevu wa Kampuni ya AngloGold Ashanti, GGM, Simon Shayo akizungumza alisema, watoto watakaoshiriki katika zoezi la Kilimanjaro Challenge mwaka huu ni wa kiume na wa kike wenye umri kuanzia miaka 13. Watoto hao yatima kutokana na tatizo la VVU/ UKIMWI wamesaidiwa na Kituo cha kulea watoto yatima cha Moyo wa Huruma Orphanage Center kilichopo Geita. Bw. Shayo alibainisha kuwa, changamoto kubwa inayotokana na janga la UKIMWI ni pamoja na maelfu ya watoto yatima wanaohitaji misaada baada ya wazazi wao kufariki, wajane wasiokuwa na kipato, pamoja na wazee wanaolazimika kuwalea wajukuu walioachwa na watoto wao ambao walifariki kutokana kwa ugonjwa huo. “Aidha, pia kuna tatizo linaloikabili jamii sasa ambapo baadhi yao wanawatenga na kukataa kuishi na watu wenye maambukizi ya VVU/ UKIMWI, kutokana na tatizo hilo Mgodi wa Dhahabu wa Geita, umeamua kuwekeza katika mradi huu kwa kuuwezesha kuwa mradi wa kitaifa na si wa GGM,” alisema Makamu wa rais miradi endelevu wa kampuni ya AngloGold Ashanti, GGM, Simon Shayo. “Huu ni mwaka wa 17 sasa tangu Kili Challenge ianze. Pia zaidi ya watu 750 kutoka pande mbalimbali za dunia wameshiriki. Taasisi zaidi ya 40 zimefaidika kutokana na utunishaji wa mfuko huu kwa sababu taasisi ambazo hazina fedha za kuendesha kampeni na shughuli mbalimbali za mapambano dhidi ya VVU/ UKIMWI zimekuwa zikifaidika na mfuko huu. Pamoja na mambo mengine, watoto waliopoteza wazazi wao sasa wanaweza kutabasamu tena kutokana na uangalizi pamoja na upendo wanaoupata kutokana na mfuko huu. “Tunapenda pia kutambua ushirikiano wa kampuni na taasisi mbalimbali kama vile ACACIA, AKO, Mantrac, NSSF, PUMA, TOYOTA, Prime Fuels, Coastal Aviation, Airtel, Capital Drilling, PPF, Serena Hotel, Geita Power Limited, SGS na wadau wengine tunaoshirikiana nao. Tunawashuruku kutokana na ushirikiano wenu katika mapambano dhidi ya VVU/ UKIMWI hivyo, tunaweza kufurahia mafanikio haya kwa kuwa na mradi endelevu,” aliongeza Simon Shayo. Balozi wa Kili Challenge ambaye pia ni mwanamuziki maarufu nchini Tanzania, Bw. Mrisho Mpoto ameileleza jamii ya Tanzania kuacha kuwa tegemezi kwa sababu ina uwezo wa kujisimamia kwa kutumia vyombo vya habari, na watu wenye ushawishi mkubwa na kwa pamoja UKIMWI unaepukiki. Tanzania inaweza kufikia malengo ya kuwa huru dhidi ya maambukizi ya UKIMWI kufikia mwaka 2030 kama tukishirikiana kwa pamoja katika vita hii. Aliongeza kuwa, ili kushiriki Kili Challenge, muhusika anaweza kuchangia mfuko huu kwa kujifadhili au kumfadhili mwingine kupanda au kuendesha baskeli kuzunguka mlima Kilimanjaro. Kuwa sehemu ya mafanikio. Kwa mawasiliano zaidi au kutoa mchango wasiliana nasi kupitia email: GGMkilichallenge@anglogoldashant.com, au tovuti www.geitakilichallenge.com. Geita Gold Mine na TACAIDS tunatumia mwamvuli huu wa Kilimanjaro Challenge katika kuelimisha jamii kuhusu janga hili la VVU/Ukimwi na tunatarajia siku moja Tanzania itatangaza kuisha kwa maambukizi ya VVU/ UKIMWI. Kwa maelezo zaidi tembelea tovuti ya www.geitakilichallenge.com Mwisho.

No comments:

Post a Comment

SEIF SHARIFF HAMAD AKIRI KUWA YEYE NI BABU KIZEE.

Seif Shariff Hamad Seif Shariff Hamad KWA mara ya kwanza Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Seif Shariff Hamad amek...