KAMPUNI ya Simu Tanzania (TTCL) imekabidhi bidhaa mbalimbali za vyakula kwa vituo vitatu vya watoto wanaoishi katika mazingira magumu pamoja na wazee wasiojiweza vyote vya jijini Dar es Salaam, ikiwa ni zawadi ya Siku Kuu za Chrismas na mwaka mpya kwa makundi hayo.
Akikabidhi msaada huo leo Makao Makuu ya Ofisi za TTCL Dar es Salaam kwa niaba ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri w. Kindamba, Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa kampuni hiyo, Nicodemas Thomas Mushi alisema vituo vilivyopokea msaada huo ni pamoja na 'Green Pastures Orphanage' Mapinga-Bagamoyo, Kituo cha Bethel Center Mbagala na Kituo cha Wazee wasiojiweza cha Bethel cha Mbagala Kuu vyote vya jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya kugawa msaada huo, Mushi alisema huo ni utaratibu wa kawaida wa kampuni ya TTCL kutoa msaada kwa jamii hasa kwa makundi ya watu wasiojiweza ili yaweze kujumuika na Watanzania wengine katika kusheherekea siku kuu za Chrismas na Mwaka Mpya kwa makundi hayo yanayokabiliwa na changamoto anuai.
"Huu ni utaratibu wa kawaida wa kampuni yetu kila mara hali ya uchumi inaporuhusu huwa tunayakumbuka makundi yenye mahitaji maalum na nikupitia ule utaratibu wetu wa kawaida wa kurejesha sehemu kidogo ya faida yetu kwa jamii, tumechangua makundi haya baada ya kupitia maombi yao na kujiridhisha wana vigezo vya kusaidiwa kutokana na walivyojieleza changamoto walizo nazo," alisema kwa niaba ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo.
Alisema kuwa kampuni ya TTCL itaendelea kuyakumbuka makundi hayo maalum na kuyasaidia kwa chochote kadri inavyokuwa na uwezo wa kufanya hivyo, huku akishauri taasisi zingine na watu wanaojiweza kusaidia pale wanapokuwa na uwezo wa kufanya hivyo kwa wasiojiweza. "...Natoa wito pia kwa makampuni, taasisi na watu wengine wenye uwezo kuunga mkono juhudi hizi za kusaidia makundi ya wasiojiweza ili yaweze kufarijika kwa namna moja ama nyingine," alisema.
Aidha alibainisha bidhaa zilizokabidhiwa ni pamoja na mbuzi watatu, mchele kilo 300, mafuta ya kula ndoo 9, maharage kilo 300, Sukari kilo 150, Unga kilo 300, juisi, maji, soda na aina mbalimbali ya mafuta ya kujipaka na sabuni vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 5.
Mchungaji wa Kanisa la EAG, Dennis Shija ambaye ni msimamizi wa Kituo cha wa Toto na Wazee wasiojiweza Mbagala Kuu alimshukuru Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Bw. Kindamba kwa msaada walioutoa katika vituo hivyo na kumuhakikishia watautumia kama ulivyo kusudia.
Aliongeza kuwa makundi hayo yanakabiliwa na changamoto mbalimbali hivyo wanapata faraja kampuni kama TTCL kujitokeza kujitokeza kuwasaidia. "...Sisi tunashukuru sana kwa msaada tuliopokea leo kwa ajili ya maandalizi ya siku kuu za mwisho wa mwaka huu, hii sio mara ya kwanza kusaidiwa na TTCL naomba kuwahakikishia msaada huu utatumika kama ulivyokusudiwa," alisema mchungaji huyo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Kituo cha 'Green Pastures Orphanage' cha Mapinga Bagamoyo, Restiel Natai aliishukuru kampuni ya TTCL kwa kuamua kuwakumbuka watu wasiojiweza ili waweze kusherekea kwa furaha siku kuu hizi za mwisho wa mwaka. Pamoja na hayo alitoa wito makampuni na taasisi nyingine kujitokeza kuwasaidia makundi kama hayo kwani nayo yanaitaji faraja hasa kipindi kama hiki ambapo familia zinakutana na kusherehekea pamoja.
Hata hivyo, alitoa wito kwa Watanzania kuendelea kuiunga mkono kampuni ya kizalendo ya TTCL ambayo sasa imefanya mageuzi makubwa kihuduma kwa kutumia huduma zake mbalimbali za mawasiliano kama huduma za intaneti, simu za mkononi na mezani na vifaa vya mawasiliano anuai kufurahia huduma bora zenye bei nafuu.
No comments:
Post a Comment