Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Mohamed Mohamed akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari juu ya hatua iliyochukuliwa na Serikali kuagiza na kusambaza dozi mbalimbali za chanjo kupitia mpango Serikali wa kukabiliana na changamoto ya upungufu wa chanjo uliojitokeza nchini.
Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa Wizara hiyo Dk. Neema Rusimabayila akitoa ufafanuzi kuhusu Chanjo ya Homa ya Manjano na vitendo vya baadhi ya watumishi wa afya wasiowaaminifu ambao hulipwa fedha ili waweze kuwatengenezea wasafiri kadi za Chanjo ya Homa ya Manjano na kisha kuzitumia nje ya nchi jambo ambalo kinyume cha sheria na hatari kwa usalama wa Afya zao.
Meneja
Mpango wa Taifa wa Chanjo wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto Dk. Dafrosa Lyimo akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa Habari kuhusu
mpango wa utoaji wa chanjo zilizokuwa na
upungufu zikiwemo za kifua Kikuu, Polio, Surua na Lubela ambazo MSD wamekwisaha
anza kuzisambaza.
Na Aron Msigwa, Dar es
salaam
WIZARA ya Afya
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Bohari Kuu ya
Dawa (MSD) inatarajia kupokea dozi 14,000 za chanjo ya homa ya manjano mwanzoni
mwa mwezi Septemba, 2016 ili kutosheleza mahitaji ya wasafiri watakaohitaji
huduma hiyo kwa kipindi cha mwaka mzima.
Aidha, Wizara hiyo imekwisha
nunua dozi za chanjo ya Kifua Kikuu na Polio 739,700 na kusambaza dozi
zipatazo milioni 7 kwenye mikoa ya Morogoro, Singida, Dodoma, Tabora na Kigoma.
Akizungumza leo jijini Dar es salaam Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Mohamed Mohamed amesema kuwa uagizaji na usambazaji
wa dozi hizo ni mpango Serikali wa kukabiliana na changamoto ya upungufu wa
chanjo uliojitokeza nchini.
Akifafanua kuhusu
kukosekana kwa baadhi ya chanjo ikiwemo ya Homa ya Manjano amesema hali hiyo
imetokana na kutokea kwa mlipuko wa homa hiyo katika nchi za jirani ikiwemo
Angola jambo lililosababisha akiba ya chanjo hiyo dunia nzima kupelekwa kwenye
nchi zenye mlipuko wa ugonjwa huo kwa lengo la kuwachanja wananchi wote ili
kuzuia ugonjwa huo kusambaa.
Amesema kutokana na
hali hiyo akiba iliyokuwa imewekwa kwa ajili ya kuzigawia nchi nyingine hasa
matumizi kwa ajili ya wasafiri ilibidi ipelekwe katika maeneo yaliyokuwa na
upungufu wa dozi hizo kutokana na uharaka na uhitaji wa chanjo hizo.
Amesema wizara kwa
kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) inatekeleza mradi wa majaribio wa
kutokomeza kichaa cha mbwa kwenye mikoa ya Lindi, Mtwara, Morogoro, Pwani na
Dar es salaam ambayo sasa ina chanjo za kichaa cha mbwa.
Amebainisha kuwa jijini
Dar es salaam chanjo hizo zinapatikana katika hospitali ya wilaya ya Temeke,
Kituo cha Afya Magomeni.
Kwa upande wake Mkurugenzi
wa Huduma za Kinga wa Wizara hiyo Dk. Neema Rusimabayila akitoa ufafanuzi
kuhusu baadhi ya watoto waliokosa chanjo katika awamu tofauti amesema kuwa wote
waliokosa chanjo kuhakikisha kuwa wanamaliza chanjo zao kwa mujibu wa idadi ya
chanjo walizopangiwa pindi zitakapopatikana.
Ametoa wito kwa
wataalam wa afya wanaohusika na utoaji wa chanjo kuwapatia taarifa wazazi wenye
watoto ambao walihudhuria vituo vya afya kisha kukosa chanjo hizo, kuhakikisha
kuwa wanarudi katika vituo vya afya ili waweze kumalizia idadi ya chanjo walizotakiwa
kupata pindi zitakapofikishwa kwenye vituo vyao.
Kuhusu Mradi wa majaribio wa kipindi cha miaka
5 wa chanjo ya kichaa cha mbwa wenye lengo la kuondoa kichaa cha mbwa amesema
kuwa unalenga kupunguza idadi ya wagonjwa na vifo vya watu vinavyotokana na
kichaa cha mbwa.
Naye Meneja Mpango wa
Taifa wa Chanjo wa Wizara hiyo Dk. Dafrosa Lyimo akifafanua kuhusu mpango wa
utoaji wa chanjo zilizokuwa na upungufu hizo
amesema kuwa mpaka sasa utaratibu wa kupokea chanjo zaidi zikiwemo za kifua` Kikuu, Polio, Surua na
Lubela ambapo MSD wamekwisaha anza kuzisambaza.
Ametoa wito kwa wazazi
wenye watoto waliokosa chanjo kuwasiliana na vituo husika ili waweze kupangiwa
ratiba ya kupatiwa chanjo hizo kwenye vituo vya kutolea huduma vya serikali
ndani ya umri wa miaka 5.
No comments:
Post a Comment