Tuesday, January 23, 2018

NAIBU WAZIRI WA ELIMU ATAKA VIFAA VYENYE THAMANI YA SH 14 BILIONI VIFUNGWE HARAKA


Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,William Ole Nasha akitoa hotuba yake wakati wa mahafali ya tisa ya Chuo cha Ufundi Arusha (ATC)

Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,William Ole Nasha(wa pili kuli) akiwapongeza wanafunzi wahitimu waliofanya vizuri zaidi katika kozi walizosomea

Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,William Ole Nasha(katikati),Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha(ATC),Dk Masudi Senzia(wa pili kulia),Makamu Mkuu wa Chuo,Utawala,Fedha na Mipango,Dk Erick Mgaya pamoja na viongozi wengine wakiwa katika picha ya pamoja na wahitimu wasichana.
NAIBU  Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,William Ole Nasha ameuagiza uongozi wa Chuo cha Ufundi Arusha(ATC) uwe umefunga vifaa vya kisasa vyenye thamani ya Sh 14 bilioni ndani ya wiki nne badala ya siku 67 ili vianze kutumika mara moja.

Ametoa agizo hilo kwenye mahafali ya tisa ya wahitimu 465 wa fani mbalimbali za ufundi jijini hapa  kuwa ukarabati na upanuzi wa karakana ufanyike ndani ya muda alioutoa ili vifaa hivyo vitumike kwa malengo yaliyokusudiwa.

"Nilipotembelea Chuo hiki Desemba 2,mwaka jana nilitoa maagizo mharakishe ujenzi na ukarabati wa miundombinu itakayotumika kufunga vifaa hivyo kutoka Austria,nafarijika kusikia kuwa utaanza mara moja kwani Wizara ilishatoa kibali cha kutumia watalaam wenu wa ndani na fedha mnayo,"alisema Ole Nasha

Alisema sekta ya elimu ya ufundi kwa mujibu wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2015 inatarajiwa kuleta maendeleo ya haraka ya rasilimali watu walioelimika na kupenda kujielimisha zaidi ili kulifanya taifa lipate maendeleo.

Ole Nasha aliongeza kuwa elimu ya ufundi ina mchango mkubwa katika kufikia uchumi wa kati unaotegemea viwanda na nchi zilizoendelea kama Japan na China zimefikia hapo zilipo kwa kutilia mkazo elimu ya ufundi.

"Katika Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo 2016/17 hadi 2020/21 tunalenga  kuongeza idadi ya wahitimu wa Vyuo vya Ufundi Stadi(Veta) kutoka 150,000 hadi 700,000  na Vyuo vya Elimu ya Ufundi vinavyotoa elimu ya Kati kutoka 40,000 hadi 80,000,"alisema

Kuhusu idadi ya wasichana wanaosoma elimu ya ufundi kuwa ndogo alivitaka vyuo vyote vya ufundi nchini kuweka mikakati ya kuongeza udahili ikiwa ni pamoja na kutoa kipaumbele maalum kwa kwa wanafunzi wa kike wanaomba kujiunga.

Pia aliagiza Mamlaka ya Elimu nchini(TEA)kuharakisha upatikanaji wa fedha kiasi cha Sh 1.7 bilioni kilichotengwa kwaajili ya ujenzi wa hosteli za wasichana katika Chuo hicho ili kupunguza pengo katika wavulana na wasichana.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo cha ATC,Dk Masudi Senzia alisema wahitimu 465 wamemaliza katika ngazi za Astashahada ya awali,Astashahada ,Stashahada na Shahada  huku wahitimu wa kike ni 101 sawa na silimia 21  na wahitimu wa kiume  ni 364 sawa na asilimia 78.

Rais Dk. Magufuli aongoza Kikao cha Baraza la Mawaziri Ikulu Dar

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiongoza kikao cha Barala la Mawaziri Ikulu jijini Dar es salaam leo Januari 22, 2018. PICHA NA IKULU.

ElimikaWikiendi kuwaunganisha wapenda Kiswahili


#ELIMIKAWikiendi ilianzishwa mnamo tarehe 15.01.2016 kama jamvi wazi kwa wapenda Kiswahili ili kujadili mambo mbalimbali yanayohusu jamii zao
 Kutafiti, kuhoji, kufahamiana, kujifunza mambo kadha wa kadha ikiwemo ubunifu wa Tehama, elimu juu ya afya, maendeleo jamii, ujasiliamali, mitindo, michezo na mengine mengi.

#ElimikaWikiendi hufanyika kila jumamosi kwa njia ya Twitter kuanzia saa 2:00 asubuhi mpaka saa 7:00 mchana kupitia #tag #ElimikaWikiendi . Saa moja la kwanza huwa ni wakati wa kukienzi Kiswahili kwa misemo,nahau,mafumbo na methali tofauti, na ikifuatiwa saa nyingine kwa ajili ya elimu juu ya afya kutoka kwa wataalam mbalimbali, Ikimalizia na masomo mchanganyiko ikiwa ni pamoja na teknolojia,maendeleo ya jamii au mada tofauti zenye mlengo wa kuelimisha jamii. 




Baadhi ya Jumbe mbalimbali ambazo zilitumwa wakati wa kutambulisha rasmi Tovuti ya Elimika Wikiendi.
Ili Kujiunga na Mtandao huu wa Elimika Wikiendi Bofya hapa www.elimika.co.tz 
 Twitter @EW_Tanzania

Saturday, January 20, 2018

UBA Tanzania yahamasisha watanzania kushiriki fursa ya wajasiliamali Tony Elemelu

Mkuu wa Idara ya Masoko na Habari wa UBA Tanzania, Ms Brendansia Kileo akizungumza katika mkutano huo na wanahabari.

Mmoja wa wanufaika wa USD 5,000 kutoka Tony Elemelu Foundation akizungumza katika mkutano huo.

Mkurugenzi wa Jagrin Agriculture Co. Ltd, Riziki Messa akizungumza katika mkutano huo.

Mkutano huo ukiendelea na wanahabari.

Washiriki katika picha ya pamoja mara baada ya mkutano huo ulioandaliwa na UBA Tanzania.


BENKI ya UBA Tanzania yahamasisha watanzania kujitokeza kwa wingi katika kutumia fursa ya kupewa mitaji kwaajili ya wajasiliamali ambayo inatolewa na taasisi ya Tony Elemelu Foundation.

Katika Semina iliyofanyika jijini Dar Es Salaam jana Mkuu wa idara ya Masoko na Habari wa UBA Tanzania, Ms Brendansia Kileo amesema kuwa kwa sasa maombi bado yanaendelea na wale wote wenye wazo la biashara wanaweza kushiriki kwa mujibu wa waelekezo.

Aliwataka wenye wazo na ndoto za biashara kuzitimiza kwa kuomba nafasi ya kupewa mtaji kupitia asasi ya 'Tony Elemelu Foundation' ambayo watakaofanikiwa kupata watapewa USD 5,000 ikiwa ni mtaji wa mawazo ya biashara yao.

Alisema maombi kuhusiana na kuomba na kupata mtaji yanafanyika kupitia tovuti ya Tony Elemelu Foundation http://www.tonyelemelufoundation.org.

Kwa upande wao baadhi ya wanufaika wa USD 5,000 kutoka Tony Elemelu Foundation walioshinda kutokea Tanzania katika miaka ya nyuma wamewataka idadi kubwa ya Watanzania kushiriki katika fursa hiyo ili waweze kufikia malengo yao.

Akizungumza mmoja wa wanufaika Mkurugenzi wa Jagrin Agriculture Co. Ltd, Riziki Messa alisema yeye pamoja na wenzake waliowahi kunufaika na fursa hiyo ya ujasiliamali amesema wamedhamiria kuhamasisha Watanzania wengi kushiriki katika fursa hiyo kutoka taasisi ya Tony Elemelu Foundation.

Aliwataka wanahabari kutumia fursa hii kwa ajili ya kuutangazia umma wa Watanzania kuomba kwa wingi ili kusudi Tanzania iweze kuwa na vijana wengi watakaonufaika na programu hii ya kutoa mitaji kwa ajili ya kuendeleza biashara au kuanzisha biashara.

Watoto Mwanza wataja 'kichocheo' cha mimba za utotoni

Watoto wakiwa katika mafunzo ya siku tatu kwa wafanyakazi wa nyumbani Jijini Mwanza, kuhusu Elimu ya Afya ya uzazi yaliyoandaliwa na Shirika la Kutetea Haki za Watoto Wafanyakazi wa Nyumbani nchini WOTESAWA.


George Binagi-GB Pazzo

WATOTO wafanyakazi wa nyumbani Jijini Mwanza wameeleza kwamba suala la ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi ni chanzo kikuu cha tatizo la mimba za utotoni na hivyo kuomba elimu hiyo izidi kutolewa katika makundi mbalimbali ya watoto ili kupambana na tatizo hilo.

Watoto hao waliyasema hayo jana kwenye mafunzo ya siku tatu kwa wafanyakazi wa nyumbani Jijini Mwanza, kuhusu Elimu ya Afya ya uzazi yaliyoandaliwa na Shirika la Kutetea Haki za Watoto Wafanyakazi wa Nyumbani nchini WOTESAWA.

“Ukosefu wa elimu ya uzazi, umaskini, tamaa pamoja na makundi maovu yenye ushawishi ni miongoni mwa sababu zinazosababisha mimba za utotoni hivyo mafunzo haya yatatusaidia kuepukana na tatizo hilo”. Alisema Christina William ambaye ni mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo.

Akiwasilisha mada kuhusu mimba za utotoni, Veronica Rodrick ambaye ni Afisa Miradi shirika la WOTESAWA, alisema ni wakati mwafanya wazazi na walezi nchini kuvunja ukimya na kuzungumza na watoto wao kuhusu afya ya uzazi ili kuwanusuru na mimba za utotoni pamoja na magonjwa ya zinaa.

“Tumeamua kuvunja ukimya kwa sababu inaonekana hata huko nyumbani wazazi wanaogoka kukaa na watoto wao kuzungumza juu ya masuala ya afya ya uzazi ikiwemo mimba, virusi vya ukimwi na kinga”. Alisisitiza huku akiwahimiza kujiepusha na mapenzi katika umri mdogo, na hata ikitokea mtu ameshindwa kujizuia basi wazingatie matumizi ya kondom.

Katika mada hiyo, kulikuwa na mjadala mpana juu ya matumizi sahihi ya kondom ambapo walihoji ikiwa ni kweli kondomu inazuia mimba pekee ama inazuia pia na magonjwa ya kuambukiza ikiwemo virusi vya ukimwi, hatua iliyoashiria kwamba watoto wengi katika ya miaka 14 hadi 18 bado hawana elimu ya kutosha kuhusu elimu hiyo.

Baadhi ya watoto walikuwa wakiamini kwamba kondom inazuia mimba pekee na haiwezi kuzuia virusi vya ukimwi huku wengine wakiamini kondom zina vitundu vidogo vidogo vinavyoweza kupitisha virusi vya magonjwa ya kuambukiza, jambo ambalo si sahihi kwani matumizi sahihi ya kondom huzuia mimba na maambukizo ya magonjwa ya kujamiana.

UNESCO yaombwa kutoa elimu ya afya ya uzazi Kisiwani Pemba

Kipindi cha mazoezi cha kuendesha mahojiano kwa ajili ya kupata habari kati ya Mtangazaji wa Redio Jamii Micheweni, Time Khamis na Mkuu wa Kitengo cha Elimu ya Afya ya Kujamiiana na Uzazi wa Mpango Wilaya ya Micheweni, Pemba Dk. Suleiman Faki Haji. Mahojiano hayo ni miongoni mwa vielelezo katika mafunzo ya Elimu ya Kujamiiana na Uzazi iliyofanyika Micheweni, Pemba yenye lengo la kuwapa ujuzi stadi wanafunzi wa shule nne za sekondari na kikundi cha akina mama Wilayani Micheweni Kutayarisha Vipindi vya redio vinavyohusu masuala yao.
Kikundi kazi cha wanafunzi na akina mama kikifanya zoezi la kuwapima uelewa wao kuhusu somo walilopewa na malengo ya mafunzo hayo katika shule ya Sekondari ya Chwaka Tumbe, Micheweni kisiwani Pemba.

SHIRIKA la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limetakiwa kutoa elimu ya afya ya uzazi kisiwani Pemba ili kuokoa kizazi kutokana na kukua kwa wimbi la kuingiliana kinyume cha maumbile.

Kauli hiyo imetolewa na washiriki wa mafunzo ya Elimu ya afya ya Uzazi na Elimu kwa mtoto wa kike yanayoendelea Micheweni, Kisiwani Pemba .

Wakichangia mada ya afya ya Uzazi, iliyotolewa na Mkuu wa Elimu ya Afya Wilayani Micheweni, Sulemani Faki Haji, mshiriki kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali anayeratibu masuala ya Jinsia, Hidaya Khamisi amesema kwamba takwimu za udhalilishaji za hivi karibuni zinaonesha Kisiwa cha Pemba hususan wilaya ya Wete inaongoza kwa asilimia 70 kwa vitendo vya ulawiti na ubakaji.

Amesema vitendo hivyo vinasababisha fedheha katika jamii na kukatisha ndoto za mtoto kufikia malengo yake maishani.

Wakionyesha ukubwa wa tatizo washiriki wamesema kuwa kwa hivi sasa si shuleni, kwenye madrasa wala nyumbani ni mahali salama kwa watoto wa kiume na wa kike kwani kwa sababu si ajabu kumwona mtu anayeheshimika katika jamii hususan mzazi wa kiume akifanya mapenzi na watoto wake wa kuwazaa na kuwapa mimba huku walimu wa dini kuwadhalilisha watoto.

Hivi karibuni mkazi mmoja wa shehia ya Kiungoni Kimango, Hamad Omari Hamad mwenye miaka 56 alikamtwa na polisi kutokana na vitendo vya ubakaji alivyowafanyia watoto wake watatu akiwemo mtoto mdogo wa miaka minne na mmoja wao kupewa mimba na baba huyo.

Kwa mujibu wa Mratibu wa Masuala ya Jinsia, Hidaya Khamisi, kuna mtandao ujulikanao kama cheni ridhia unaendelea katika baadhi ya shule Kisiwani Pemba wa watoto kwenda kufanya vitendo viovu iwe kupiga punyeto, kufanya ngono au kulawitiana.

Utafiti uliofanyika wilaya ya Wete mwaka 2016 kuhusiana na masuala ya unyanyasaji wa watoto iligundulika kwamba darasa zima lenye watoto 60 walisema kwamba wanataka wawekewe mazingira ili wasidhalilishwe kwa sababu watoto wote darasa hilo wamefanyiwa vitendo vya udhalilishaji hususan kulawitiwa.

Aidha ripoti nyingine kutoka shule moja wilayani Micheweni kwa mujibu wa Meneja wa Kituo cha Redio Jamii Micheweni, Ali Kombo imeonyesha kwamba kati ya wanafunzi 60 ni wanafunzi 10 tu ambao walikuwa bado hawajafanyiwa udhalilishaji wa kingono.

Mafunzo  ya Elimu ya afya ya Uzazi na Elimu kwa mtoto wa kike yanayoendeshwa na UNESCO yana lengo la kuunda Vikundi vya Vijana Shuleni na Akina Mama Watayarishaji Vipindi vya redio kwa kushirikiana na Redio Jamii Micheweni, ambavyo vitasambaza Elimu rika kwa Vijana na Akina Mama.

Mhe. Samia Suluhu awataka viongozi Dar kukabiliana mafuriko

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.


MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka Viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam kuchukua hatua za haraka katika kukabiliana na mafuriko katika jiji la Dar es Salaam.

Makamu wa Rais ameyasema hayo leo wakati wa mkutano na Wadau wa Mazingira kuhusu changamoto ya mafuriko na hifadhi ya mazingira katika mkoa wa Dar es Salaam. Makamu wa Rais alisema kulikosekana umakini katika kusimamia mazingira na miundo mbinu katika jiji la Dar es Salaam.

Makamu wa Rais alizungumzia changamoto za kuwepo kwa taka ngumu ambazo zingeweza kuzalisha umeme na gesi, “kuna miradi watu wanaomba kuzalisha umeme kwa taka, anazungushwa mtu miaka mitano, sita, saba, haambiwi ndio wala haambiwi hapana “

Makamu wa Rais amesema kuna uhitaji sana wa elimu ya mazingira kwa jamii na kupeana taarifa mbali mbali zinazohusiana na mazingira.

Makamu wa Rais alisema moja ya tatizo kubwa ni kuchukua nyezo za uthibiti kufanya nyenzo za mapato “Vibali, leseni hivi ni vitu vinavyotolewa kwa ajili ya uthibiti lakini tumevigeuza kuwa vyombo vya mapato” kutokana na hali hiyo vibali vimeendelea kutolewa hovyo bila kuzingatia taratibu.

Makamu wa Rais alitoa maagizo ya kuundwa kwa Kamati ya Mazingira ya mkoa wa Dar es Salaam ambayo itaundwa na Waziri wa Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba na kuratibiwa  na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda.

Makamu wa Rais aliwashukuru wadau wa maendeleo wakiongozwa na Benki ya Dunia katika kusaidia kupambana na tatizo la uharibifu wa mazingira na mafuriko jijini Dar es Salaam.

Awali Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba alisema ni wakati wa kutafakari na kupata jawabu la kudumu la suala la mafuriko yanayotokea katika jiji la Dar es Salaam.

SEIF SHARIFF HAMAD AKIRI KUWA YEYE NI BABU KIZEE.

Seif Shariff Hamad Seif Shariff Hamad KWA mara ya kwanza Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Seif Shariff Hamad amek...