Wednesday, November 8, 2017

COSTECH yawapa wanafunzi Sikonge mbegu ya viazi lishe

 Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi wa COSTECH ambaye ni Ofisa Mwandamizi wa COSTECH, Audax Mutagwa (kulia), akimkabidhi mbegu ya mahindi aina ya Wema, Mkuu wa Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, Peres Boniface Magiri wakati wa uzinduzi na kukabidhi mbegu bora za Mahindi ya Wema 2109, mihogo na viazi lishe kwa ajili ya mashamba darasa katika vijiji vya Isunda, Kisanga, Udongo na Kanyamsenga wilayani humo jana.
 Wanakikundi cha Aliselema wakishusha mbegu ya mihogo tayari uzinduzi wa shamba darasa.
 Ofisa Kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Said Babu akizungumza kabla ya kuanza uzinduzi huo katika Kijiji cha Isunda kilichopo Kata ya Nkolye.
 Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Pares Magiri akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Isunda.
 Wanakikundi cha Aliselema wakiwa kwenye uzinduzi huo.
 Mtafiti wa mazao ya mizizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Maruku kilichopo mkoani Kagera Jojianas Kibura akielekeza namna ya kupanda mihogo.


  Mtafiti wa mazao ya mizizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Maruku kilichopo mkoani Kagera Jojianas Kibura akimuelekeza namna ya kupanda mbegu ya mihogo mkuu wa wilaya hiyo.
 Mwenyekiti wa Kikundi cha Aliselema, Amir Hassan akipanda mbegu ya mihogo.
 Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi wa COSTECH ambaye ni Ofisa Mwandamizi wa COSTECH, Audax Mutagwa akipanda mbegu ya mihogo katika shamba darasa.
 Mwenyekiti wa Kikundi cha Aliselema, Amir Hassan akizungumza na waandishi wa habari kuhusu changamoto waliyokuwa nayo ya kupata mazao kiduchu kwa kutumia mbegu zisiso bora.

 Wakulima wakisubiri kuelekezwa namna ya upandaji wa mbegu hizo za mihogo.
 Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Pares Magiri akizungumza na wakulima wa Kijiji cha Kisanga kabla ya uzinduzi wa shamba darasa la viazilishe.
 Mtafiti wa mazao ya mizizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Maruku kilichopo mkoani Kagera Jojianas Kibura akimuelekeza namna ya kupanda mbegu ya viazilishe katika kijiji cha Kisanga.
 Wanawake wa Kijiji cha Kisanga wakiwa kwenye uzinduzi huo wa shamba darasa la mbegu ya viazilishe.
 Mtafiti kutoka Kituo cha Utafiti cha Ukiriguru mkoani Mwanza, Mariana akielekeza namna ya upandaji wa viazilishe.
 Mkuu wa Wilaya, Peres Magiri akipanda mbegu ya viazilishe wakati wa uzinduzi wa shamba hilo.
 Mwalimu wa Baraka Kita wa Shule ya Msingi Sogea B, akipanda mbegu hiyo ya viazilishe.
 Mkulima, Mariam Said akipanda mbegu ya viazilishe 
Mwalimu George Adamu Mwalwizi, akizungumzia mbegu mpya ya viazi lishe walioletewa kuwa itakuwa ni mkombozi kwao na wanafunzi.

Na Dotto Mwaibale, Sikonge Tabora

WANAFUNZI wilayani Sikonge mkoani Tabora wataanza kunufaika na viazi lishe baada ya kupokea mbegu bora ya viazi hivyo, mihogo na mahindi ya Wema kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kushirikiana na Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB)

Hayo yameelezwa katika Kijiji cha Kisanga na Mkuu wa Wilaya hiyo, Peres Boniface Magiri wakati akizungumza na wakulima kwenye uzinduzi na kukabidhi mbegu bora za Mahindi ya Wema 2109, mihogo na viazilishe kwa ajili ya mashamba darasa katika vijiji vya Isunda, Kisanga, Udongo na Kanyamsenga.

Magiri alisema baada ya kuotesha mbegu hiyo ya viazilishe kwa wingi kitakachofuata ni kuanzisha utaratibu wa wanafunzi katika shule mbalimbali za wilaya hiyo kupata chakula cha mchana badala ya kwenda nyumbani.

Alisema wilaya hiyo kupelekewa mbegu hizo kwao ni fursa kubwa na kwa kushirikiana na wakulima na maofisa ugani atahakikisha mashamba darasa hayo yanatunzwa na kutoa mrejesho.

Aliongeza kuwa shule mbalimbali zitaanzisha mashamba ya viazilishe hivyo ili kumaliza tatizo la kukosa chakula kama sio kulipunguza.

"Tunahitaji matokeo chanya ya mashamba darasa hayo yawasaidie wakulima wengine katika wilaya hiyo na kuwa atahakikisha anatembelea mara kwa mara yalipo mashamba hayo" alisema Magiri.

Mtafiti wa mazao ya mizizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Maruku kilichopo mkoani Kagera Jojianas Kibura aliwaambia wakulima kuwa hekta moja ya muhogo kwa kutumia mbegu hiyo bora inaweza kutoa tani 25 hadi 32 wakati viazi itatoa tani 7 hadi 9 kwa Hekta moja.

Alisema kuwa endapo watafuata kanuni bora za kilimo cha mazao hayo kwa kuzingatia nafasi kati ya mche na mche na mstari kwa mstari na matumizi ya mbolea wataweza kuongeza uzalishaji zaidi tofauti na sasa ambapo kwenye hekta moja ya muhogo wanapata tani nane hadi kumi wakati kwenye viazi wanapata tani moja hadi 3.

Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi wa COSTECH ambaye ni Ofisa Mwandamizi wa COSTECH, Audax Mutagwa, alisema mbegu hiyo ya mahindi imefanyiwa utafiti na inavumilia ukame wakati ile ya mihogo ikivumilia magonjwa kama batobato na michirizi kahawia huku zikitoa mavuno mengi.

Tuesday, November 7, 2017

TAFITI ZA KILIMO ZAWAFIKIA WAKULIMA WA WILAYA YA URAMBO KWA MARA YA KWANZA

 Mshauri wa Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB), Dk.Nicholaus Nyange, akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Urambo mkoani Tabora, Angelina Kwinga mbegu ya mihogo inayostahimili ukame katika uzinduzi wa mashamba darasa ya mbegu hiyo ya mihogo, mahindi aina ya Wema 2109  pamoja na viazi lishe yalioanzishwa kwa ajili ya wakulima wa vijiji nane katika wilaya hiyo leo kwa ufadhili wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kushirikiana  OFAB.



 Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ugalla, Geofrey Magambo akizungumza katika uzinduzi huo wakati akiwatambulisha viongozi mbalimbali wa Kata hiyo na Kijiji cha Isongwa.
 Ofisa Kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Said Babu akizungumza katika uzinduzi huo.
 Mshauri wa Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB), Dk.Nicholaus Nyange (kulia), akizungumza kwenye uzinduzi darasa wa shamba la mahindi katika Kijiji cha Isongwa kilichopo Kata ya Ugalla Ussoke wilayani Urambo mkoani Tabora.
 Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora katika uzinduzi wa mashamba darasa hayo ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi Uchumi, Phillips Mtiba akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa huo.
 Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora katika uzinduzi wa mashamba darasa hayo ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi Uchumi, Phillips Mtiba, akikabidhiwa mbegu ya mahindi ya Wema na Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi wa COSTECH, Ofisa Mwandamizi wa COSTECH, Audax Mutagwa.
 Wananchi wa Kijiji cha Isongwa wakisubiri kupata mafunzo ya upandaji wa mbegu ya mahindi katika shamba darasa.
 Mtafiti, Ismail Ngolinda kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ilonga, mkoani Morogoro akitoa maelezo kwa wakulima wa Kijiji cha Isongwa jinsi ya kupanda mahindi aina ya Wema.
 Mkulima wa Kijiji cha Isongwa, Malando Malando akiuliza swali.
 Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Isongwa, Shabani Rajabu Mkokoteni akiuliza swali.
 Wanawake wakulima wa Kijiji cha Isongwa wakijumuika kwenye uzinduzi huo wakiwa na watoto wao.
 Mtafiti, Ismail Ngolinda kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ilonga, mkoani Morogoro, akionesha uchimbaji wa mashimo kabla ya kupanda mbegu hiyo ya mahindi.
 Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Isongwa, Shabani Rajabu Mkokoteni , akichimba mashimo.
 Mtafiti, Ismail Ngolinda kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ilonga, mkoani Morogoro, akionesha, akionesha namna ya kuweka mbolea kwenye mashimo yaliyochimbwa.
  Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora katika uzinduzi wa mashamba darasa hayo ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi Uchumi, Phillips Mtiba, akipanda mahindi.
 Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi wa COSTECH, Ofisa Mwandamizi wa COSTECH, Audax Mutagwa, akipanda mahindi.



 Mwenyekiti wa Halmshauri ya wilaya hiyo Adamu Malunkwi, akizungumza na wakulima wakati wa uzinduzi huo.
 Mtafiti wa Mazao ya Mizizi kutoka Kituo cha Ufatiti cha Maruku mkoani Kagera, Jojianas Kibura, akiwaelekeza wakulima wa Kijiji cha Usisya namna ya kupanda mbegu ya viazi lishe.
 Wakulima wa Kijiji cha Kapiluka wakijiandaa kupanda mbegu ya viazi lishe.
Mtafiti wa Mazao ya Mizizi kutoka Kituo cha Ufatiti cha Maruku mkoani Kagera, Jojianas Kibura, akiwaelekeza wakulima wa Kijiji cha Motomoto namna ya kupanda mbegu ya viazi lishe.

Na Dotto Mwaibale, Urambo Tabora

TAFITI za kilimo zinazofanywa hapa nchini na wataalamu zimewafikia wakulima wa Wilaya ya Urambo mkoani Tabora kwa mara ya kwanza.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Halmshauri ya wilaya hiyo Adamu Malunkwi wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye uzinduzi na kukabidhi mbegu bora za Mahindi ya Wema 2109 na mihogo kwa ajili ya mashamba darasa kwa wakulima wa vijiji nane vya Isongwa, Ussoke, Usisya, Kapiluka, Vumilia, Kamalendi, Muungano na Songambele.

Alisema mara nyingi tafiti zilizokuwa zikifanyika zilikuwa zikibaki kwenye makabati bila ya kuwafikia walengwa na jambo lililofanywa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kushirikiana na Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB) kuwafikishia wakulima matokeo ya tafiti hizo ni jambo zuri na limefurahiwa na kwa hapa kwetu ni mara ya kwanza kutokea.

"Tuna amini kuwa hivi sasa uchumi utastawi kuanzia ngazi ya familia, wilaya na hadi taifa na tutakuwa na chakula cha kutosha" alisema Malunkwi.

Malunkwi alisema katika wilaya hiyo walikuwa na changamoto kubwa ya kupata mbegu bora kwani wakulima wengi walikuwa wakitumia mbegu za zamani walizozizoea na kujikuta wakipata mazao kiduchu lakini kwa ujio wa mbegu hizo ni ukombozi mkubwa kwao.

Alitaja changamoto nyingine ambayo inapaswa kuangaliwa kwa karibu kuwa ni bei kubwa ya mbegu hiyo ya mahindi ambayo inauzwa shilingi 12,000 kwa kilo mbili huku kukiwa na debe moja la mahindi linalouzwa shilingi 10,000 ambalo wakulima wamekuwa wakilikimbilia kutokana na bei yake kuwa ya chini ingawa mazao yake hayana tija.

Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi wa COSTECH ambaye ni Ofisa Mwandamizi wa COSTECH, Audax Mutagwa, alisema mbegu hiyo ya mahindi imefanyiwa utafiti na inavumilia ukame wakati ile ya mihogo ikivumilia magonjwa kama batobato na michirizi kahawia huku zikitoa mavuno mengi.

Alisema COSTECH katika mkoa huo imetoa kilo 60 za mbegu ya Wema, mihogo 40,000 na viazi lishe 75 ambapo katika wilaya hiyo vijiji nane vimenufaika kwa ajili ya kutengeneza mashamba darasa ambayo yatatoa mbegu zitakazosambazwa kwa wakulima katika maeneo mengine. 

Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora katika uzinduzi wa mashamba darasa hayo ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi Uchumi, Phillips Mtiba alisema hivi sasa mwajiriwa ni mkulima ambaye analima kilimo chenye tija na si vinginevyo na kuwa serikali siku zote imekuwa ikihimiza kilimo bora ambapo aliwataka maofisa ugani kupanga ratiba za kuwafikia wakulima.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Angelina Kwinga aliishukuru COSTECH na OFAB kwa kutekeleza ahadi ya kuwapelekea mbegu kama walivyo ahidi walipokuwa wakitoa mafunzo kwa maofisa ugani wa wilaya hiyo mapema mwaka huu.


Monday, November 6, 2017

MBEGU ZA COSTECH ZILIZOTOLEWA WILAYANI MBOGWE KUONGEZA UZALISHAJI

Wakulima wa Kijiji cha Iponya katika Halmshauri ya Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita wakifurahia kupata mbegu bora ya mihogo aina ya Mkombozi waliokabidhiwa na  Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kushirikiana na Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB), kwa ajili ya kuanzisha shamba darasa la mbegu hiyo wilayani humo jana.
Mshauri wa Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB), Dk.Nicholaus Nyange (kulia), akimkabidhi mbegu ya mihogo , Mwakilishi wa Mkurugenzi wa wilaya hiyo, Furaha Chiwile wakati wa uzinduzi wa shamba hilo katika Kijiji cha Iponya. Katikati mwenye shati la kitenge ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Nsika Sizya.


 Watafiti wakiandaa shamba darasa la mahindi katika Kijiji cha Mponda.
 Wananchi wa Kijiji cha Mponda wakisubiri uzinduzi wa shamba darasa la mahindi.
 Ofisa Kilimo wa Wilaya Mbogwe, Stephen Shilemba akizungumza na wakulima wa Kijiji cha Mponda kabla ya ufunguzi wa shamba darasa.
 Ofisa Kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, David Makabila, akitoa maelezo kwa wakulima wa Kijiji cha Mponda wakati wa uzinduzi wa shamba darasa la mahindi ya WEMA.
 Mtafiti kutoka COSTECH, Dk.Beatrice Lyimo (kulia), akizungumza na wakulima wa Kijiji cha Mponda.
  Mtafiti kutoka COSTECH, Dk.Beatrice Lyimo, akimkabidhi mbegu ya mahindi ya Wema, Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Mbogwe, Stephen Shilemba. Kulia ni Mshauri wa Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB), Dk.Nicholaus Nyange.
 Mtafiti kutoka COSTECH, Dk.Beatrice Lyimo, akimkabidhi mbolea ya kupandia mahindi aina ya DAP, Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Mbogwe, Stephen Shilemba.
 Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Mbogwe, Stephen Shilemba, akimkabidhi mbegu ya mahindi aina ya WEMA, Ofisa Ugani wa Kata ya Lugunga, Dickson Namlanda.

 Wanawake wa Kijiji cha Lwazeze wakishuhudia uzinduzi huo.
 Mkulima wa Kijiji cha Lwazeze, Charles Kangai akichimba mashimo kwa ajili ya upandaji mbegu ya mahindi ya WEMA.




 Mtafiti wa Mazao ya Mizizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Maruku mkoani Kagera, Jojianas Kibula, akielekeza jinsi ya upandaji wa mbegu hiyo ya mihogo aina ya Mkombozi.
 Makamu Mwenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, Nsika Sizya, akipanda mbegu ya mihogo katika shamba darasa katika Kijiji cha Iponya.
Mshauri wa Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB), Dk.Nicholaus Nyange, akipanda mbegu ya mihogo aina ya Mkombozi kwenye shamba darasa katika Kijiji cha Iponya.

Na Dotto Mwaibale, Mbogwe, Geita.

MAKAMU Mwenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, Nsika Sizya amesema mbegu bora ya mahindi ya WEMA 2109 na mihogo aina ya Mkombozi waliyokabidhiwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kushirikiana na Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB) itaongeza chachu ya kilimo wilayani humo.

Sizya aliyasema hayo wilayani humo jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika uzinduzi na kukabidhi mbegu bora za Mahindi ya Wema yanayostahimili ukame na mihogo kwa ajili ya mashamba darasa kwa wakulima wa vijiji vinne vya Mponda kilichopo Kata ya  Luganga, Kijiji cha Ushetu kilichopo Kata ya Ushirika, Kijiji cha Lwazeze kilichopo Kata ya Ngemo na Kijiji cha Iponya kilichopo Kata ya Iponya.


Alisema changamoto kubwa waliyokuwa nayo wakulima katika Halmshauri hiyo ni kukosekana kwa mbegu bora za mihogo na mahindi ambapo alisema kwa kupata mbegu hizo kutaongeza ari na chachu ya kilimo kwa wananchi.

Aliishukuru CSTECH na OFAB kwa kuwapelekea mradi huo katika wilaya hiyo na kuupokea kwa shangwe kwa kuzingatia kuwa mihogo ni zao la biashara na chakula ambapo aliwataka wananchi kubadilika na kufanya kilimo chenye tija kama wataalamu wanavyowaelekeza.


Mtafiti wa Mazao ya Mizizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Maruku mkoani Kagera, Jojianas Kibula aliwaambia wakulima hao kuwa hekta moja ya mihogo iwapo watalima kwa kufuata ushauri wa wataalamu wataweza kupata tani 25 hadi 32 kwa zao la mhogo na viazi watapata tani 7 hadi 9 kwa hekta moja.

Alisema matokeo hayo watayapata endapo watafuata kanuni bora za kilimo cha mazao hayo kwa kuzingatia nafasi kati ya mche na mche na mstari kwa mstari na matumizi ya mbolea hivyo wataweza kuongeza uzalishaji zaidi tofauti na sasa ambapo kwenye hekta moja ya mihogo wanapata tani nane hadi kumi wakati kwenye viazi wanapata tani moja hadi 3.

Mtafiti huyo alisisitiza kuwa mbegu hiyo ya Mihogo ya Mkombozi imefanyiwa utafiti na kuonekana kustahimili magonjwa hatari ya mihogo ya batobato kali na michirizi ya kahawia ambayo imekuwa ikiwapatia hasara kubwa wakulima wengi na kupoteza hadi asilimia 90 za mazao.

Mtafiti kutoka COSTECH, Dk. Beatrice Lyimo aliwataka wakulima wa wilaya hiyo kwa kushirikiana na maofisa ugani kuyatunza mashamba hayo na wao kuwa walimu kwa wakulima wenzao.

"Nawaomba nyinyi mliobahatika kupata mashamba darasa haya muwe walimu wa kutoa mbegu bora ambayo mtaisambaza katika vijiji vingine ili kila mkulima aweze kufaidika" alisema Dk.Lyimo.

Ofisa Kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, David Makabila alisema asilimia 75 ya wakulima katika mkoa huo wanategemea kilimo hivyo mafunzo yaliyotolewa kwa maofisa ugani kupitia COSTECH na OFAB yataongeza kasi ya uzalishaji hasa baada ya kupata mbegu hizo bora.

Alisema changamoto kubwa waliyonayo ni wakulima kushindwa kufuata kanuni bora za kilimo ingawa wameanza  kubadilika pole pole baada ya kupata mafunzo.

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni upungufu wa maofisa ugani kwani waliopo kwa mkoa mzima ni 189 wakati wanaohitajika ni 512 na kuwa katika maeneo mengine ofisa ugani mmoja anahudumia vijiji tisa tena bila ya kuwa na usafiri wa uhakika.

Hadi jana Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kushirikiana na Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB), imeweza kuwafikia wakulima katika vijiji 22 vya wilaya za Mikoa ya Kagera na Geita na kutoa elimu kwa vitendo kwenye matumizi ya Sayansi na Teknolojia za kilimo kwa uzalishaji wenye tija ambapo kuanzia kesho kutwa Jumatatu Novemba 6,2017 watafanya kazi hiyo katika wilaya zote za Mkoa wa Tabora kwa kuanzisha mashamba darasa ya mbegu za mahindi ya WEMA na Mihogo.

Friday, November 3, 2017

Mohammed Dewji apongeza jitihada za Rais Magufuli kufufua viwanda

Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL Group), Mohammed Dewji akizungumza katika mkutano wa Global Business Forum 2017 kuhusu Viwanda kwa Nchi za Afrika, mkutano huo wa siku mbili umefanyika Dubai, UAE na kuhudhuriwa na watu 5860 wakiwepo viongozi wa serikali za nchi za Afrika na wafanyabiashara. (Picha na Clouds Media)

MKURUGENZI Mtendaji wa Kampuni ya Mohammed Enterprises (MeTL Group), Mohammed Dewji amepongeza uamuzi wa Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda kwa kufufua viwanda ambavyo vilikuwa havifanyi kazi.
Dewji ametoa pongezi hizo wakati akizungumza katika mkutano wa siku mbili wa Global Business Forum 2017 (GBF) kuhusu Viwanda kwa Nchi za Afrika uliofanyika Dubai, Falme za Kiarabu (UAE).
Mfanyabiashara huyo ambaye anamiliki viwanda 41 alisema uamuzi aliochukua Rais Magufuli ni mzuri hasa katika kipindi hiki ambacho Tanzania inaelekea katika uchumi wa kati.

Dewji alisema kampuni yake ya MeTL Group itaendelea kushirikiana na serikali na katika kipindi cha miaka kadhaa ijayo amejipanga kuhakikisha anatoa ajira kwa Watanzania 100,000 jambo ambalo litasaidia kukuza uchumi wa nchi na kwa wananchi..
 “Nianze kwa kumpongeza Mhe. Rais John Pombe Magufuli kwa shabaha yake ya viwanda, ni nzuri sababu kuna ongezeko la thamani lakini pia watu wanaweza kupata ajira na pia hizi biashara zitalipa kodi ambazo zitaisaidia serikali kuwekeza kwenye mambo ya afya na maji na huduma za jamii. Mimi shabaha yangu kwenye miaka saba au nane ijayo MeTL Group tunataka tuajiri watu 100,000,” alisema Dewji.
Dewji ambaye kwa mujibu wa jarida la Forbes ni tajiri namba moja nchini aliongeza kuwa utendaji wa Rais Magufuli ni wa kasi hivyo anategemea kuwa katika kipindi cha miaka michache ijayo uchumi wa Tanzania utakuwa umekuwa  sana.
“Mimi naona kwa kasi ya Mhe. Rais kwenye miaka miwili au mitatu ijayo tutakuwa tumefika mbali sana, uchumi wetu kwasasa ni asilimia sita au saba lakini kama tukitaka kuondoa umaskini lazima nchi yetu ukuaji wa uchumi uanze kukua kwa zaidi ya asimilia 10, mimi nina muamini sana Mhe. Rais na shabaha yake kwahiyo Mungu atutangulie na sisi tupo nyuma yake tutafika hivi karibuni,” alisema Dewji.
Pia Dewji alizungumzia umuhimu wa mkutano wa GBF ambao umekutanisha watu kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika wakiwepo viongozi wa serikali za nchi za Afrika na wawekezaji alisema ni nafasi ya kipekee kwani pamoja na kujadili viwanda pia amepata nafasi ya kuwaelezea washiriki wa mkutano fursa za uwekezaji zilizopo hapa nchini.
“Umuhimu ni mkubwa sana nakuja hapa kama MO lakini pia nawakilisha nchi yangu Tanzania, nimeitangaza nchi yangu ili watu waje na wawekeze, nimewaeleza mazingira yetu ya uwekezaji ni mazuri, tuna malighafi na tunahitaji viwanda angalau watu wetu wa Tanzania wapate ajira na serikali ipate kodi,” aliongeza Dewji.

WAKULIMA BUKOMBE WALILIA MBEGU ZA MAHINDI YA WEMA 2109

WAKULIMA WILAYA YA BUKOMBE WALILIA MBEGU ZA MAHINDI YA WEMA 2109 YANAYOSTAHIMILI UKAME
Mshauri wa Jukwaa la Matumizi ya Bioteknolojia katika kilimo (OFAB), Dk.Nicholaus Nyange (kulia), akimkabidhi mbegu ya mahindi ya Wema 2109, Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Bukombe, Joseph Bachibya kwa ajili ya kupanda katika shamba darasa katika Kijiji cha Msasa kilichopo Kata ya Runzewe wilayani humo leo. Wengine kutoka kulia ni Mtafiti wa Mazao ya Mizizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Maruku mkoani Kagera, Jojianas Kibula na Mtafiti, Dk. Beatrice Lyimo  kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH)
Maofisa Ugani wakiandaa shamba darasa la mahindi ya Wema  katika Kijiji cha Kabagole kilichopo Kata ya Busonzo litakalosimamiwa na Kikundi cha Igembensabho.
Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Bukombe, Joseph Bachibya, akizungumza na wakulima wa Kikundi cha Igembensabho.
Wanakikundi cha Igembensabho wakiwa wameshosha mikono ikiwa ni ishara ya mshikamano.
Mshauri wa Jukwaa la Matumizi ya Bioteknolojia katika kilimo (OFAB), Dk.Nicholaus Nyange (kulia), akimkabidhi mbegu ya mhogo aina ya Mkombozi, Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Bukombe, Joseph Bachibya kwa ajili ya kupanda katika shamba darasa katika Kijiji cha Msasa kilichopo Kata ya Runzewe wilayani humo leo. Wengine kutoka kulia ni Mtafiti wa Mazao ya Mizizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Maruku mkoani Kagera, Jojianas Kibula na Mtafiti, Dk. Beatrice Lyimo  kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH)
Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Bukombe, Joseph Bachibya akikmabishi mbegu ya Wema Ofisa Ugani wa Kijiji cha Kabagole, Ponsian Pancras.
Mtafiti wa Kilimo kutoka Kituo cha Utafiti wa Ilonga mkoani Morogoro, Ismail Ngolinda, akiwafundisha wakulima wa Kijiji cha Kabagole namna ya kupanda mahindi ya Wema. Kulia ni Ofisa Ugani, David Makabila kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Katibu wa Kikundi cha Igembensabho, Jacob Nsunzu akizungumza na waandishi wa habari.
Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Bukombe, Joseph Bachibya akikmabishi mbegu ya Wema Ofisa Ugani wa Kijiji cha Msasa, Mohamed Mwangeni. Katikati ni Mshauri wa Jukwaa la Matumizi ya Bioteknolojia katika kilimo (OFAB), Dk. Nicholaus Nyange.

Mtafiti wa Kilimo kutoka Kituo cha Utafiti  Ilonga mkoani Morogoro, Ismail Ngolinda, akiwafundisha wakulima wa Kijiji cha Msasa, namna ya kupanda mahindi ya Wema.

Na Dotto Mwaibale, Bukombe Geita

WAKULIMA wilayani Bukombe Mkoani Geita wameiomba Serikali na wasambazaji wa mbegu bora za mahindi ya WEMA 2109 yanayostahimli ukame kufikisha mbegu hizo wilayani humo ili kuweza kutatua changamoto ya  mavuno kidogo wanayoyapata kila mwaka kutokana na mabadiriko ya tabia nchi na wadudu.

Ombi hilo limetolewa na wana Kikundi cha Igembensabho kwenye Kijiji cha Kabagole Kata ya Busonzo wilayani Bukombe mkoani Geita wakati wakipokea mbegu bora za mahindi  yaliyozalishwa na Mradi wa WEMA kwa ajili ya kupanda kwenye shamba darasa la kikundi hicho ili waweze kuyalinganisha na aina za mahindi wanayolima kila mwaka na mahindi hayo yenye sifa ya kustahimili ukame yaliyotolewa na  Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kupitia Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB)

Akizungumza  kwa niaba ya wanakikundi hicho, Adam Kasalamsigwa alisema kuwa kutokana na sifa walizoambiwa na wataalamu kwenye mahindi hayo yatakuwa mkombozi kwa wakulima wengi kutokana na aina zingine za mahindi waliyozoea kupanda kushindwa kutoa matokeo waliyokuwa wakiyatarajia baada ya mvua kukata mapema kabla mahindi hayajazaa.

“Tunashukuru mmetuletea mbegu hizi ili tufanye majaribio na kuona jinsi mahindi haya yanavyostahimili ukame lakini mmetuambia tayari mmeshayafanyia majaribio kwenye maeneo mengine ya Tanzania na kuonyesha mafanikio makubwa hivyo hatuna sababu ya kusubiri hadi msimu ujao tuleteeni mbegu hizo tununue na kupanda” alisisitiza Kasalamsigwa.

Aidha wakulima hao wameiomba Serikali kuona sababu ya kuziingiza mbegu hizo kwenye ruzuku ya pembejeo ili ziweze kuwafikia hadi vijijini kwa bei nafuu ili ziweze kukinzana na mabadiliko ya taba nchi ambayo yamekithiri sana kwenye wilaya hiyo na maeneo mengine.

Akitoa maelekezo ya namna ya kupanda mahindi hayo Mtafiti kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ilonga mkoani Morogoro, Ismail Ngolinda aliwaambia mahindi hayo baada ya kufanyiwa utafiti kupitia mradi wa mahindi yanayotumia maji kwa ufanisi (WEMA) waliyajaribu kwenye maeneo mbalimbali kwenye mikoa ya Morogoro na Tanga na kuonyesha kufanya vizuri kuliko aina nyingine za mahindi wanayolima wakulima.

Ngolinda aliwasisitiza kuwa pamoja na wao kupata mbegu hizo zinazostahimili ukame lakini ni lazima wazingatie kanuni bora za kilimo cha mahindi ikiwemo matumizi ya mbolea za kupandia na kukuzia ,kupanda kwa mistari na nafasi  na kufanya Palizi lakini wasipofanya hivyo hawawezi kupata mavuno yanayostahili badala yake watapata hasara kama mahindi mengine.

Aliwataka kuzingatia suwala la kupanda kwa mistari na nafasi ili kuweza kumshakikishia mkulima anatumia shamba lake vizuri badala ya kupanda holela na kujikuta amepanda miche michache kwenye shamba akidhani ni ekari moja kumbe ni miche inayoenea kwenye nusu ekari iliyopandwa vizuri.

Ngolinda aliwashauri wakulima kulima ekari moja kitaalamu na kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo ili apate mavuno makubwa badala ya kulima ekari tano ambazo anatumia nguvu nyingi na gharama kubwa lakini mwishoni anapata mavuno sawa na mtu mwenye ekari moja.

“ Unalima ekari tano bila kufuata kanuni bora za kilimo alafu unapta magunia 25 ya mahindi wakati mwenzako analima ekari moja tuu kwa kufuata kanuni bora za kilimo na anapata hadi gunia 30 hii ni tofauti kubwa sana kwa hiyo wakulima naomba mbadilike” alisistiza Ngolinda.

Aidha Mtafiti huyo wa zao la mahindi aliwaambia kuwa kufanya majaribio hayo kupitia mashamba darasa kwenye mkoa mzima wa Geita ni kutaka kuwaonyesha wakulima hao mbinu za kisasa za kilimo na matumizi ya mbegu bora yanavyoweza kumsaidia mkulima kuzalisha kwa tija ili aachane na kilimo cha mazoea ambacho hamkimsaidii mkulima kuondokana na umasikini lakini kupata chakula cha kutosha.

Awali akizungumza na watafiti hao kutoka COSTECH, Kituo cha Utafiti wa Kilimo Ukiriguru Mwanza na Maruku mkoani Kagera kabla ya kwenda kutembelea mashamba darasa na kufanya uzinduzi huo kwenye wilaya hiyo ,Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya hiyo,  Dionis Myinga ameishukuru COSTECH na OFAB kwa kusaidia kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya wakulima kwa kuwapelekea mbegu hizo bora ambazo zinajibu changamoto mbalimbali sugu za wakulima.

Myinga alisema sio wataalamu hao wametembea umbali mrefu kutoka Dar es salaamu hadi Geita ili kufikisha matunda ya utafiti kwa wakulima hivyo wilaya yake itafanya kazi bega kwa bega katika kuhakikisha malengo ya mpango huo yanafikiwa ili kuchochea uzalishaji wa mazao hayo kupiti mashamba darasa hayo.

“Tafiti zipo nyingi sana kwenye vituo vya utafiti na vyuo vikuu lakini zinabaki kwenye makabati tuu na hazitumiwi kwenye kutatua tatizo lililokusudiwa lakini kila utafiti ungefika kwa mlengwa naamini Tanzania tungekuwa mbali sana kwenye mambo mbalimbali hususani kilimo” alisema Myinga.

Katika kuonyesha kuridhika kwake na maelezo ya mbegu za mahindi na mihogo iliyoletwa kwenye wilaya yake akaomba  mbegu za kununua za mihogo hiyo aina ya Mkombozi za kutosha kupanda shamba la ekari kumi ili iwe mfano kwa wakulima wilayani humo pamoja na kuwa chanzo cha kusambaza mbegu nyingi kwa wakulima wengi zaidi.

Vijiji vilivyonufaika na uanzishwaji wa mashamba darasa katika wilaya hiyo ni Kijiji cha Msasa na Kabagole ambapo mashamba hayo yatasimamiwa na vikundi.

Watafiti hao kesho siku ya Ijumaa wanatarajia kwenda Halmshauri ya Mji wa Buchosa Sengerema kwa ajili ya kazi ya kuanzisha mashamba darasa na kisha wiki ijayo kwenda kumalizia  kazi ya kusambaza mbegu hizo Mkoa wa Tabora.

Thursday, November 2, 2017

MPANGO UENDESHAJI WA KIJINSIA KWA AJILI YA MWITIKIO WA UKIMWI TANZANIA BARA WATAMBULISHWA

Mratibu wa Jinsia kutoka TACAIDS, Jacob Kayombo na Afisa Jinsia kutoka TACAIDS, Judith Luande wakijadili baadhi ya maoni, maswali na mapendekezo ya wajumbe ambao ni timu ya kudhibiti Ukimwi ya Mkoa wa Singida wakati wa Mafunzo juu ya mpango wa uendeshaji wa kijinsia.

Mjumbe wa mafunzo juu ya mpango wa uendeshaji wa kijinsia Afisa wa Serikali za Mitaa Hussein Mwatawala akipitia fomu zitakazotumika katika kukusanya taarifa za masuala ya Kijinsia mkoani Singida.

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI kupitia Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) imeandaa Mpango wa uendeshaji wa Kijinsia kwa ajili ya mwitikio wa Masuala ya Ukimwi ambao umetambulishwa rasmi kwa timu ya Kuthibiti Ukimwi Mkoani Singida.

Mratibu wa Jinsia Kutoka TACAIDS Jacob Kayombo ameongoza mafunzo hayo kwa timu ya kuthibiti Ukimwi Mkoa wa Singida ambapo amewaeleza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kuratibu na kutoa dira katika utekelezaji wa program mbalimbali za Ukimwi kwa ngazi ya Mkoa.

Kayombo amesema Mafunzo hayo yamelenga kuutambulisha mpango huo pamoja na fomu zitakazotumika katika ukusanyaji wa taarifa zihusuzo jinsia na Ukimwi.

“Mafunzo haya tunayotoa yamejikita katika kuufafanua mpango huu utakavyotumika pamoja na namna ambavyo fomu hizi zitatumika kukusanya taarifa za jinsia na Ukimwi kwa Mkoa wa Singida na jinsi ambavyo taarifa hizo zitasaidia kufanya maamuzi sahihi kuhusu masuala ya Ukimwi”, amesema Kayombo.

Ameongeza kuwa matarajio yanayotegemewa baada ya mafunzo hayo kutolewa ni kuona masuala yote ya kijinsia yanapewa kipaumbele katika program mbalimbali za Ukimwi.

Kayombo amesisitiza kuwa mpango huu utakuwa ni mwongozo wa wadau wa masuala ya Ukimwi ili waweze kutekeleza shughuli zao kwa kuzingatia usawa wa kijinsia hasa katika kuweka mikakati ya kuthibiti Ukimwi yenye uelekeo wa Usawa wa kijinsia.

Amebainisha kuwa mpango huu ambao umedumu katika kipindi cha mwaka 2016 mpaka 2018 una mwelekeo mpya wa program za ukimwi wenye kuzingatia masuala ya kijinsia pamoja na kuondoa changamoto zitokanazo na mila na desturi potofu za masuala ya kijinsia.

Naye Mjumbe wa mafunzo hayo Afisa wa Serikali za Mitaa Hussein Mwatawala amesema mafunzo hayo yametoa mwanga na mwelekeo utakawaosaidia katika kusimamia wadau wanaotekeleza shughuliza Ukimwi ili wazingatie usawa wa kijinsia mkoani hapa.

Mwatawala amesema maafisa waliopata mafunzo hayo wamepewa elimu ya kutosha juu ya mpango na wameufahamu vema kazi iliyobaki ni kuhakikisha masuala ya usawa ya kijinsia yanapewa kipaumbele katika kila program ya Ukimwi inayotekelezwa na wadau mkoani hapa.

Mpango wa uendeshaji wa masuala ya Kijinsia 2016-2018 umeanzishwa kwa lengo la kutoa mwongozo kwa wadau wa masuala ya Ukimwi ili watekeleze program zao katika mtazamo wa usawa wa kijinsia.

Mpango huu unashughulikia tofauti za kijinsia zikiwemo ukatili wa kijinsia, unyanyapaa na ubaguzi ili kulinda haki za watu wote wakiwemo wanaume,wanawake,wasichana na wavulana ili wapate huduma za uzuiaji wa maambukizi ya VVU, tiba, matunzo na msaada.

Aidha mpango huu unahusianishwa na Mkakati wa tatu wa taifa wa kuthibiti Ukimwi 2013-2018 na Mkakati wa tatu wa kuthibiti VVU na Ukimwi wa Sekta ya Afya 2013-2017 ambapo mikakati hiyo ina kanuni ambazo zinajumuisha usawa wa kijinsia na ulinzi wa haki za binadamu.


SEIF SHARIFF HAMAD AKIRI KUWA YEYE NI BABU KIZEE.

Seif Shariff Hamad Seif Shariff Hamad KWA mara ya kwanza Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Seif Shariff Hamad amek...