Thursday, November 2, 2017

DC NYANG'WALE ALIA NA USALAMA WA CHAKULA NCHINI...!


 Mkuu wa Wilaya ya Nyang'wale Mkoa wa Geita, Hamim Buzohera Gwiyama (katikati), akizungumza na watafiti wa kilimo kutoka  Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Maruku mkoani Kagera, Ukiriguru Mwanza, Ilonga mkoani Morogoro na Waandishi wa Habari kabla ya kukabidhiwa mbegu bora za mahindi na mhogo kwa ajili ya kuzipanda kwenye mashamba darasa katika vijiji vinne wilayani humo leo hii. Kulia ni Diwani wa Kata ya Nyugwa, Ndozi Manual na kushoto ni Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Fabian Sospeter ambaye alikabidhiwa mbegu hizo na kuhutubia wananchi kwa niaba ya mkuu huyo wa wilaya.


 Wananchi wakiwa kwenye mkutano wa uzinduzi wa upandaji wa mbegu katika mashamba darasa uliofanyika Kata ya Nyugwa wilayani humo.

 Diwani wa Kata ya Nyugwa, Ndozi Manual, akizungumza katika uzinduzi huo.

 Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Fabian Sospeter, akihutubia wananchi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo.


 Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi na Viumbe Hai wa COSTECH, Dk. Bakari Msangi, akimkabidhi mbegu ya mhogo aina ya Mkombozi Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Fabian Sospeter kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo.


 Mtaalamu wa Mazao ya Mizizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Maruku mkoani Kagera, Jojianas Kibula, akiwaelekeza wananchi wa Kata ya Nyugwa jinsi ya upandaji wa mbegu ya mhogo aina ya Mkombozi kwenye shamba darasa.


 Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Fabian Sospeter akipanda mbegu ya mhogo aina ya Mkombozi kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo.
 Mtafiti kutoka  Kituo cha Utafiti wa Kilimo  cha Ilonga, mkoani Morogoro, Ismail Ngolinda akitoa maelekezo kwa wakulima wa Kijiji cha Kakora  jinsi ya upandaji wa mbegu ya mahindi aina ya Wema 2109 yanayostahimili ukame. Kushoto ni Mkuu wa Idara ya Kilimo wa Wilaya ya Nyang'wale,Gudala Kija Tabu na katikati ni mkulima wa kijiji hicho.
 Wananchi wa kijiji cha Kakora wakiwa wamesimama mbele ya shamba la mahindi ambalo mahindi yake ni duni kutokana na mimea yake kushambuliwa na wadudu.
 Mkulima Pendo Sangoma akishiriki kupanda mbegu ya Wema katika shamba darasa katika Kijiji cha Kakora wilaya humo. Kushoto ni Ofisa Ugani, David Makabila kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.
 Watoto, Michael  na Getruda Bundala wa Kijiji cha Kakora wakiwa wamebeba mbegu ya mahindi aina ya Wema wakati wa uzinduzi wa shamba darasa katika kijiji hicho.
 Ofisa Ugani wa Kijiji cha Nyang'wale, akitoa maelekezo kwa watafiti wa kilimo kuhusu masuala ya kilimo.
Mshauri wa Jukwaa la Matumizi ya Bioteknolojia katika Kilimo (OFAB), Dk.Nicholaus Nyange, akizungumza na viongozi wa Kijiji cha Kanegele, maofisa ugani na watafiti kabla ya kupanda mbegu ya mhogo katika shamba darasa kwenye kijiji hicho. Wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa kijiji hicho, Makoye Malikwisha.

Na Dotto Mwaibale, Nyang'wale, Geita

MKUU wa Wilaya ya Nyang'wale Mkoa wa Geita Hamim Buzohera Gwiyama amesema bila ya kuwepo kwa usalama wa chakula nchini bado kutaendelea kuwepo na changamoto nyingi za maendeleo na kuwa pasipo chakula hakuna kitakachoweza kufanyika.

Hayo yalisema na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Fabian Sospeter  kwa niaba ya Mkuu wa wilaya hiyo, Hamim Gwiyana wilayani humo jana wakati akipokea mbegu bora za mahindi aina ya Wema na mhogo aina ya Mkombozi kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kushirikiana na Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB) kwa ajili ya kuanzisha mashamba darasa ya mbegu katika vijiji vya Kakora, Nyang'wale, Kanegele na Nyugwa.

"Bila ya kuwepo kwa chakula cha kutosha hakuna kitu kitakachoweza kufanyika kwani shughuli zote zitasimama hivyo ni muhimu kuhimizana katika kilimo chenye tija kama tunavyo himizwa na wataalamu wetu kutoka COSTECH, Kituo cha Utafiti wa Kilimo Ukiriguru Mwanza na Maruku mkoani Kagera" alisema Gwiyama.

Alisema usalama wa kujilinda na adui hauna shida kwani mtu anaweza kuandaa jeshi lake la kukabiliana na adui huku akiwa na silaha nzito lakini sio usalama wa chakula ambao unahitaji maandalizi ya kutosha na watu kujituma na kufanya kazi kwa bidii hasa za kilimo chenye tija.

Alisema kukosekana kwa chakula mara nyingi kunachangiwa na tabia za baadhi ya watu kuharibu mazingira kwa kukata miti hovyo hivyo kusababisha mvua kushindwa kunyesha  na maeneo mengi kuwa na ukame.

Alisema katika wilaya yake njaa imechangia kwa kiasi kikubwa wanafunzi kuwa watoro na kushindwa kumaliza shule na kuwa kukosekana kwa chakula kwa watu ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

Diwani wa Kata Nyugwa, Ndozi Manual akizungumza kwa niaba ya wananchi wa vijiji hivyo aliwata wananchi kuyatunza mashamba darasa hayo kwa kuwa ni mali yao baada ya kuletewa na COSTECH na OFAB na kuwa baada ya kupata mbegu bora wanatarajia kupata mavuno mengi.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi na Viumbe Hai wa COSTECH, Dk.Bakari Msangi akizungumza kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, alisema kuwa kazi kubwa ya COSTECH ni kuishauri serikali katika masuala yote yanayohusu  Sayansi na Teknolojia na kusimamia tafiti zote za kisayansi katika maeneo mbalimbali na kuhakikisha matunda ya tafiti hizo yanawafikia walengwa.

Alisema mbegu hizo walizozikabidhi ikiwamo ya mahindi yanayostahimili ukame ya Wema 2109 na mhogo zimefanyiwa utafiti na zitapandwa katika mashamba darasa na baadae kusambazwa kwa wakulima wengine ili kuondoa changamoto ya kukosekana kwa mbegu bora kutokana na wakulima kukabiliwa na mbegu ambazo zilikuwa na magonjwa. 

Dk. Bakari aliwataka wakulima na maofisa ugani kuyatunza mashamba darasa hayo ili kazi kubwa iliyofanyika isipotee bure na baada ya muda mfupi watarudi kuangalia maendeleo yake.




KAMPENI YA WANAWAKE NA ARDHI YAZIDI KUNUFAISHA WENGI ....!

KAMPENI ya Wanawake na Ardhi imekutanisha wadau mbalimbali jijini Dar es salaam kujadili juu ya 'Nafasi ya Wanawake katika michakato ya usimamizi wa ardhi'. Warsha hiyo imehusisha wawakilishi kutoka Wizara ya Ardhi, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo, Mashirika na wawakilishi wa wakulima na wafugaji.

Kiujumla warsha ilikuwa na malengo mbalimbali ikiwemo  pamoja; kuelewa michakato ya mabadiliko mbalimbali ya taratibu za usimamizi wa Ardhi (mfano marejeo ya sera ya Taifa ya ardhi) na athari chanya au hasi kwa wanawake wa Tanzania.
Pia ililenga kusambaza ujumbe wa kampeni ya wanawake na ardhi kama ulivyokusanywa kutoka kwa wadau ambao ni wakulima wadogo wanawake, wafugaji na mashirika mbalimbali, pia kupata fursa ya kuipatia Serikali maoni ya wanawake katika marejeo ya sera ya ardhi ya Taifa.


 Bi. Wiyagi Kisandu kutoka WLAC akitoa mada juu ya uelewa wa maswala ya kijinsia kwa jamii na wanawake kwa ujumla, ambapo alisema kuwa ni muhimu Serikali na wadau wengine washirikiane kuwapa elemu ya haki miliki ya ardhi ili iwe rahisi hata kipindi cha mchakato wa kushughulikia kupata hati hizo uwe rahisi.


 Bi. Naomi Shardrack Mratibu wa Miradi ya Ardhi kutoka Shirika la Kimataifa la Oxfam akielezea kuhusu dhana ya kuwawezesha wanawake kumiliki rasilimali ardhi, pia alielezea utafiti wa maswala ya umiliki wa ardhi uliofanywa na shirika la Oxfam na namna mifumo dume inavyo wakandamiza wanawake katika kumiliki Ardhi.


 Bw. Stephano Mpangala kutoka RUDI akielezea kisa mkasa kilichohusu mzee Kuzenza Magoso (80) ambaye alikuwa na wake sita (6), kwa kutambua umuhimu wa hati milki ya ardhi aliwapatia  wake zake wote hati za kumiliki ardhi ili kuondoa migogoro ambayo ingeweza kujitokeza mbeleni.

Bi.
Elisa Simioni aliyewahi kushiriki shindano la Mama wa chakula linaloendeshwa na Shirika la Kimataifa la Oxfam Tanzania akieleza kisa mkasa cha namna akina amama  walivyoweza kushiriki kikamilifu katika kupigania na kurejesha msitu  kijijini kwao ambao ulivamiwa na kutumika vibaya

 Bw. Adam Ole Mwarabu akielezea zaidi juu ya Kisa mkasa alichozungumzia Bi. Elisa Simion kuhusu uharibifu wa misitu na kusisitiza kuwa licha ya akina mama hao kupigania msitu isiharibiwe, lakini pia akina mama takribani 100 walikwenda kulala katika msitu huo kwa lengo la kuonesha kuwa hawakufurahishwa na uharibifu huo, na mpaka sasa hakuna tena wavamizi katika eneo hilo.


 Bi. Rehema Abdallah mhamasishaji wa umiliki wa ardhi kwa wanawake, alisema kuwa wao wapo tayari katika kushiriki kuchangia gharama za mchakato wa kuhakikisha wanapata hati miliki za ardhi kwa kuwa ni kitu cha muhimu.


 Mh. Yannick Ndoinyo  Diwani wa kata ya Ololosokwani- Longido akielezea namna wakina mama walivyopewa nafasi kubwa katika kumiliki ardhi.


 Dk. Adam Nyaruhume Mkuu wa Chuo cha Ardhi Morogoro, alieleza kuwa ni muhimu kuwajulisha na kuwaelimisha wanakijiji hasa kuhusiana na maswala ya mipango na matumizi ya ardhi pamoja na umilikishwaji wa ardhi, pia aliwapongeza Asasi ya RUDI kwa kufanya vizuri katika mipango na matumizi ya ardhi katika maeneo mbalimbali wanayoyashughulikia.

 Bw. Joseph Rutaizibwa, Mchumi Mwandamizi kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya makazi akitoa ushauri kuwa Baraza la Taifa la Uwekezaji Wananchi kiuchumi lishirikishwe katika michakato hii muhimu inayohusu maswala ya ardhi.

 Bi. Eva Mageni akielezea changamoto mbalimbali ambazo wanakutana nazo wanawake hasa katika umilikishwaji wa ardhi.

 Bi. Rosada Msoma Afisa Maliasili Mkuu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii,alisema kuwa Wizara inatoa ushirikiano wa karibu kwa wananchi katika kuhakikisha kuna utunzaji bora wa maliasilizetu.


 Wawakilishi mbalimbali kutoka Wizara ya Ardhi, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo, Wawakilishi wa wakulima na wafugaji, Asasi za Kiraia za Nchini pamoja na za kimataifa, na wadau wengine wakiwa katika makundi mbalimbali kujadili mipango mikakati ya kuendeleza haki za wanawake katika rasilimali ardhi nchini.


 Bi. Anne Manangwa Mtafiti kutoka TNRF akitoa mapendekezo kwa niaba ya Asasi za Kiraia ambapo kati ya mambo waliyo omba yafanyiwe kazi katika kampeni  ya wanawake na ardhi ni pamoja na, Elimu itolewe kwa njia ya vyombo vya habari juu ya kumiliki ardhi, haki za wanawake katika kumiliki ardhi pamoja na ushirikishwaji wa wanawake katika kuandaa Sera,uandaaji wa mikakati pamoja na kutunga Sheria.

 Bi. Marcelina Kibena Mwakilishi kutoka MVIWATA, wao katika kikundi chao walitoa maoni kuhusu kutambua makundi mbalimbali kupitia elimu itasaidia kuondoa mfumo dume,kuhamasisha wanawake katika kushika nyadhifa mbalimbali za maamuzi, vyombo vya habari kuandaa programu mbalimbali za uelewa kuhusu kumiliki ardhi na mgawanyo wa rasilimali kuanzia ngazi ya kijiji.

Wadau mbalimbali wakiwemo wawakilishi kutoka Wizara ya Ardhi, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo, Care International, WLAC, PINGOs, UCRT, FFH, LANDESA, PWC, NES na ILRI pamoja na waendeshaji wa kampeni hiyo Shirika la Kimataifa la Oxfam Tanzania pamoja na TALA wakiwa katika warsha hiyo.


WAKULIMA CHATO WAFURAHIA MBEGU BORA YA VIAZI KUTOKA COSTECH

 Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi na Viumbe Hai wa COSTECH, Dk.Bakari Msangi (kushoto), kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), akimkabidhi mbegu ya viazi lishe kwa ajili ya shamba darasa la Kijiji cha Kibehe, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato, Mhandisi Joel Hari wakati wa uzinduzi wa shamba hilo wilayani Chato leo. 

 Wanakikundi cha Umoja cha Kijiji cha Kibehe kilichopo Kata ya Kigongo wakiandaa shamba lao la mbegu.

 Wanakikundi cha Umoja cha Kijiji cha Kibehe kilichopo Kata ya Kigongo wakiwa kwenye uzinduzi wa shamba darasa la viazi lishe na mihogo.

 Mtafiti wa Mazao ya Mizizi wa Wilaya ya Chato, Monica Mulongo akizungumzia vitamini A inayopatikana kwenye viazi lishe ambayo ni muhimu kwa watoto.


Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi na Viumbe Hai wa COSTECH, Dk.Bakari Msangi, akizungumza wakati wa uzinduzi wa shamba darasa la mbegu ya viazi lishe. Kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato, Mhandisi Joel Hari.

 Mtafiti Ismail Ngolinda kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ilonga mkoani Morogoro akizungumzia ubora wa mbegu ya Wema pamoja na upandaji wake.


 
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri ya Wilaya ya Chato, Mhandisi Joel Hari , akionesha mbegu ya mahindi ya Wema baada ya kukabidhiwa.


 Mtafiti wa mazao ya mizizi kutoka Kituo cha Utafiti cha Maruku mkoani Kagera, Jojianas Kibula, akiwaonesha wakulima wa Kibehe jinsi ya kupanda mbegu ya mhogo.

 Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ipandikilo, Clara Fidelis akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kijiji hicho.

  Mtafiti wa mazao ya mizizi kutoka Kituo cha Utafiti cha Maruku mkoani Kagera, Jojianas Kibula akitoa maelezo kwa wakulima wa vijiji vya Ipandikilo na Kitongoji cha Kaseni jinsi ya kupanda mbegu ya mhogo.

 Watafiti Bestina Daniel na Ismail kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ilonga wakijadiliana jambo wakati wa uzinduzi wa shamba darasa la mahindi katika Kijiji cha Bukiliguru.

 Mshauri wa Jukwaa la ioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB), Dk.Nicholaus Nyange akipanda mbegu ya mhogo katika shamba darasa la Kijiji cha Itale.

 Wakulima wa Kijiji cha Bukiliguru wakishiriki kuapanda mbegu za mahindi katika shamba darasa.

 Mtafiti Ismail Ngolinda kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ilonga mkoani Morogoro akiwaelekeza wakulima jinsi ya kupanda mbegu bora ya mahindi ya Wema inayovumilia ukame.

Wakulima wa Kijiji cha Bukiliguru wakifuatilia uzinduzi wa shamba la mihogo.

Na Dotto Mwaibale, Chato

WAKULIMA Wilaya Chato mkoani Geita wamefurahia mbegu bora ya mihogo, mahindi na viazi lishe waliopewa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ili kuanzisha mashamba darasa ya mbegu hizo na kuzisambaza kwa wakulima wengine katika maeneo mengine.

Wakizungumza wilayani hapa leo kwa nyakati tofauti wakati wa uzinduzi wa mashamba darasa ya mbegu hizo katika vijiji vya Kibehe, Ipandikilo, Kitongoji cha Kaseni, Kijiji cha Itale na Bukiliguru kilichopo Kata ya Bwanga walisema mbegu hizo walizokabidhiwa na COSTECH kwa kushirikiana na Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo ni mkombozi kwao.

Ofisa Kilimo wa Kata ya Kachwamba,  Hamisi  Matesi alisema Costech kuwapelekea wakulima mbegu hizo itawasaidia sana kupata chakula wananchi wa kata hiyo ziada watauza.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ipandikilo, Clara Fidelis akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kijiji hicho alisema wakulima walikuwa wakipata mavuno machache ya mahindi na mihogo kwa kuwa hawakuwa na mbegu bora hivyo baada ya kufunguliwa kwa shamba darasa la mbegu hizo katika maeneo yao wanategemea kupata mazao mengi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri ya Wilaya ya Chato, Mhandisi Joel Hari aliwataka wananchi hao kutambua kuwa mpango huo wa serikali ya awamu ya tano unawategemea sana wakulima katika kilimo hivyo fursa hiyo walioipata ya kupelekewa mbegu hizo wasiipoteze.

“Hakikisheni  mbegu hizi bora za mihogo mnazopewa mnazitunza  ili kutoa nafasi kwa wananchi wengi zaidi kujifunza mbinu bora za kilimo hiki kupitia shamba darasa hili ili kila mkazi wa Chato aweze kulima na kuzalisha kwa tija” alisema Mhandisi Hari.

Hari ameishukuru COSTECH kwa kuamua kuipatia wilaya hiyo mashamba darasa katika vijiji hivyo kwani anaamini mbegu hizo zitasimamiwa vizuri na kisha kuwafikia wakulima wengi zaidi ili waweze kuachana na mbegu zao za zamani ambazo zinashambuliwa na magonjwa ya batobato na michirizi ya kahawia.

Akizungumza kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH wakati wa kukabidhi mbegu hizo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi na Viumbe Hai wa COSTECH, Dk.Bakari Msangi alisema kazi kubwa ya COSTECH ni kuishauri serikali katika masuala yote yanayohusu  Sayansi na Teknolojia na kusimamia tafiti zote za kisayansi katika maeneo mbalimbali na kilimo na kuhakikisha matunda ya tafiti hizo yanawafikia walengwa.

Alisema mbegu hizo walizozikabidhi ikiwamo ya mahindi yanayostahimili ukame ya Wema 2109 zimefanyiwa utafiti na zitapandwa katika mashamba darasa na baadae kusambazwa kwa wakulima wengine ili kuondoa changamoto ya kukosekana kwa mbegu bora kutokana na wakulima kukabiliwa na mbegu ambazo zilikuwa na magonjwa kama batobato katika mihogo.

Dk. Bakari aliwataka wakulima hao kuyatunza mashamba darasa hayo na kubwa baada ya muda mfupi watarudi kuangalia maendeleo yake. 




SEIF SHARIFF HAMAD AKIRI KUWA YEYE NI BABU KIZEE.

Seif Shariff Hamad Seif Shariff Hamad KWA mara ya kwanza Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Seif Shariff Hamad amek...