Tuesday, September 19, 2017

Serikali kusimamia miradi ya umeme Kituo cha Tipper-Kigamboni

 Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani, (wakwanza kulia), Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania, (TANESCO), Mhandisi Dkt. Tito Mwinuka, (wakwanza kushoto), na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo anayeshughulikia Miradi, Mhandisi Khalid James, (watatu kushoto), wakimsikiliza Meneja Mradi wa TEDAP, Mhandisi Emmanuel Manirabona, (aliyenyoosha mkono), wakati Naibu Waziri na uongpozi wa TANESCO, ulipotembelea mradi wa TEDAP wa Gongolamboto jijini Dar es Salaam, Septemba 18, 2017. Mradi huo unahusu upanuzi na uendelezaji wa mradi wa kusafirisha umeme wa 132kv.

SERIKALI kupitia Shirika la Umeme Tanzania, (TANESCO), imeahidi kusimamia miradi ya umeme Kituo cha Tipper-Kigamboni,  Mbagala na Kurasini ili kuhakikisha inakamilika kwa haraka na kwa wakati na hatimaye wananchi wa maeneo hayo wanaondokana na adha ya kukatika kwa umeme mara kwa mara.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani, mwishoni mwa ziara yake ya kufuatilia uboreshaji wa vituo vya kupoza na kusambaza umeme pamoja na ujenzi wa kituo kipya cha kufua na kusambaza umeme huko Kimbiji  wilayani Kigamboni jijini Dar es Salaam Septemba 18, 2017.
Waziri pia amekagua ujenzi wa mradi wa maendeleo ya upanuzi na upatikanaji nishati (TEDAP), wa kusafirisha umeme wa 132kv ulioko Gongolamboto nje kidogo ya jiji.
“Wananchi wanataka umeme, hawahitaji kujua  nguzo za umeme zimepatikana wapi, au upembuzi yakinifu utakamilika lini, nimeagiza baada ya siku tano kuanzia leo (Septemba 18), fanyeni kazi usiku na mchana walau vituo viwili vya kupoza na kusambaza umeme viwe vimekamilika ili wananchi wa Mbagala na Kigamboni wapate umeme wa kutosha.” Alisema Dkt. Kalemani mbele ya Mbunge wa Kigamboni Dkt. Faustine Ndungulile, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Mhe. Hashim Mgandila na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi, Dkt. Tito Mwinuka na viongizi wengine wa Tanesco.
Dkt. Kalemani alisema, miradi hiyo imechukua muda mrefu, na kwamba hakuna muda zaidi utakaoongezwa kuikamilisha.
Serikali kupitia TANESCO, inatekeleza miradi mitano ya kuongeza kiasi cha umeme kwenye maeneo ya Mbagala na maeeno kadhaa ya wilaya ya Temeke, Kurasini na Kigamboni ili kukabiliana na ongezeko la kasi la watu na shughuli za kiuchumi katika maeneo hayo.
Aidha Naibu Waziri aliipongeza TANESCO, kwa kutekeleza agizo lake la kuhakikisha wakazi 3,500 wa Kigamboni waliolipia ili kuunganishiwa umeme, wawe wameunganishiwa ifikapo Septemba 15, 2017 ikiwa ni pamoja na kupeleka nguzo za umeme zaidi ya 1,000 maagizo ambayo yametekelezwa.
Hata hivyo naibu Waziri alimueleza Mheshimiwa Mbunge wa Kigamboni na Mkuu wa Wilaya hiyo kuwa tiba mahsusi ya upungufu wa umeme kwenye wilaya hiyo ni kukamilika kwa ujenzi wa kituo kipya cha kupoza na kusambaza umeme cha Kimbiji.
“Tiba kubwa ya matatizo ya umeme kwa watu wa Kigamboni, na Mbagala ni hapa Kimbiji(kituo kipya), vile vituo vingine vitapunguza tu matatizo lakini naomba Mheshimiwa Mbunge, uwafikishie ujumbe wananchi kuwa Serikali ya awamu ya Tano inayo dhamira ya kweli ya kuhakikisha inawapatia umeme wa uhakika sio tu wananchi wa Kigamboni bali watanzania wote kwa ujumla.” Alifafanua Dkt. Kalemani.
Naibu Waziri ameshuhudia hatua mbalimbali za ukamilishaji wa miradi hiyo zikiwa zimefikiwa ambapo katika kituo maeneo yote aliyotembelea.
Kuhusu ujenzi wa kituo kipya cha Kimbiji, Dkt. Kalemani amemuagiza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANSCO, Mhandisi Dkt. Tito Mwinuka, kuwaleta mafundi wa TANESCO wealiotekeleza kwa muda mfupi ujenzi wa mradi wa kituo cha kupoza na ksuambaza umeme kule Mtwara ili waje kuongeza nguvu.

Mbunge wa Kigamboni Mhe. Dkt. Faustine Ndungulile, (kushoto), akizungumza mbele ya Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani ambaye alifuatana naye kwenye ziara hiyo.

Sakafu ya kufungia transfoma mpya ya umeme wa 15mva kituo cha Tipper-Kigamboni, ikijengwa Septemba 18, 2017

Mshine mpya kwenye kituo cha Mbagala

Kituo cha Kurasini ambacho nacho kitakuwa tayari baada ya siku tano.

Dkt. Kalemani, (katikati), Dkt. Ndungulile (wapili kushoto) na Dkt. Mwinuka, (wakwanza kushoto), wakiwa na Meneja wa Mradi wa TADEP, Mhandisi Emmanuel Manirabona, (kulia), baada ya kujionea moja ya mashine mpya ikiwa bado imefunikwa ili kuzuia vumbi kwenye kituo cha Kurasini.

Fundi akiwa kazini kwenye kituo cha Kurasini.

Naibu Waziri Dkt. Kalemani, na Mbunge wa Kigamboni Dkt. Ndungulile, wakiwa na furaha baada ya kutembelea kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Mbagala, ambacho ujenzi wake umekamilika.

Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Mhe. Hashim Mgandila, akizungumza mwishoni mwa ziara ya Naibu Waziri, Dkt. Kalemani huko Kimbiji.

Naibu Waziri Dkt. Kalemani na Mhandisi Khalid James.

Msafara wa Naibu Waziri ukiwa kwenye eneo la mradi wa TEDAP. Gongolombaoto.

Mkandarasi anayejenga mradi wa TEDAP, Gongolamboto, akizunguzma.

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, anayeshughulikia usambazaji umeme na huduma kwa wateja mama Joyce Ngahyoma, akielezea hatua zilizochukuliwa na TANESCO katika kuhakikisha wateja 3,500 wa TANESCO Kigamboni waliolipia gharama za kuunganishiwa umeme, wanapatiwa huduma hiyo ikiwa ni pamoja na kupelekwa kwa nguzo zaidi ya 1,000 kwenye eneo la Kigamboni. Anayemsikiliza ni Naibu Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani.

Kituo cha Mbagala

Dkt. Kalemani, (kushoto), akimsikiliza Meneja wa TANESCO Mkoa wa Temeke, Mhandisi Jahulula akielezea hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Tipper-Kigamboni.

Dkt. Kalemani, (wapili kushoto), akizungumza jambo na Mhandisi Dkt. Tito Mwinuka, walipowasili eneo la Kimbiji ambako kunatarajiwa kujengwa kituo kipya cha kupoza na kusambaza umeme kitakachohudumia wakazi wa Kigamboni, Kurasini na Mbagala. Wakwanza kushoto ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO nayeshughulikia Miradi, Mhandisi Khalid James.

Namaingo Business Agency mradi mkubwa wa ufugaji kuku

Kampuni ya Namaingo Business Agency Co. Ltd imezindua Mradi mkubwa wa ufugaji kuku unaosimamiwa na Kikundi cha Ujasiriamali cha Shinyanga, Kishapu na Kahama (SHIKIKA) uliopo katika mtaa wa Sanjo kata ya Chamaguha katika manispaa ya Shinyanga.

Uzinduzi wa mradi huo umefanyika Septemba 18, 2017 katika mtaa wa Sanjo kata ya Chamaguha Manispaa ya Shinyanga. Kikundi cha SHIKIKA kinachotekeleza mradi huo, kilianzishwa Machi 16, 2017 baada ya kampuni ya Namaingo Business Agency Co. Ltd kuwaelekeza wanachama wake kuunda vikundi vya wanachama hamsini hamsini ili wakubaliane kuendesha mradi wanaoupenda.

Wanakikundi hao waliamua kuanzisha mradi wa ufugaji wa kuku wa kienyeji ndipo kampuni hiyo ikawachangia vifaranga 200, wakaanza ufugaji tarehe 9. 6. 2017 na mpaka sasa kikundi kina kuku zaidi ya 1300.

Akizungumza wakati wa kuzindua mradi huo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Namaingo Business Agency Co. Ltd, Biubwa Ibrahim aliwapongeza wanakikundi hao kwa kuchangishana fedha shilingi milioni 8 na kuamua kuanzisha mradi huo.

“Ndugu zangu jambo hili mlilofanya na mlilolitekeleza kwanza ni jambo la kitaifa kwa sababu wananchi wakiwa na uchumi mzuri serikali nayo inapata kodi lakini pia tunakuwa tumetengeneza ajira”, alisema Ibrahim.

“Pamoja na jitihada hizi mlizochukua kwa muda mfupi, Tunatamani kuona kila mtu anakuwa na kuku walau 1000 kwenye banda lake, najua changamoto kubwa iliyopo ni mitaji na riba kubwa kwenye mikopo lakini kuna fedha kwa ajili ya maendeleo ya akina mama na vijana zenye riba ndogo sana zipo kwenye benki mbalimbali, serikali inafanyia kazi suala la mikopo hiyo,” aliongeza.

Aidha Ibrahim aliwataka wananchi kuwa na maamuzi ya kutoka katika hali walizonazo kwa kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa na kuilaumu serikali.

“Hakuna haja ya kuilaumu serikali bali unapaswa kujiajiri ili kubadilisha maisha yako, hakuna maisha mazuri kama mtu ukijiajiri, hata hao waliojiriwa wakistaafu huwa wanarudi kujiajiri hivyo kujiajiri ndiyo kila kitu katika maisha yako”, aliongeza Ibrahim.

“Sisi Namaingo Bussiness Agency Co. Ltd kazi yetu ni kuwabadilisha kiakili ili muweze kubadilika kimawazo kwani fursa za kubadili maisha yenu,zipo nyingi,kufanikiwa kwa mtu ni maamuzi ya mtu mwenyewe”, alisema.

Akisoma risala, Katibu Msaidizi wa SHIKIKA, Beatrice Nangale alisema gharama za kuanzisha mradi huo ni shilingi milioni 8 lakini mpaka sasa umegharimu shilingi milioni 20 ambazo ni michango ya wanachama.

Alisema ili kufikia malengo yao, kundi hilo linahitaji eneo kubwa la ekari 3000 kwa ajili kupanua mradi wa kuku, kuwa na mashine za kutotolea, kutengeneza chakula cha kuku, kuchakata minofu ya kukuna ufugaji wa nyuki wa asali.

“Pia tunataka kufuga samaki, mbuzi, sungura na ng’ombe kisha kusindika nyama zao, kulima mboga mboga na matunda kama vile mapapai, kupanda miti na kujenga nyumba kwa ajili ya makazi”, alifafanua Nangale.

Hata hivyo alizitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili kuwa ni ukosefu wa chakula na dawa za kuku mjini Shinyanga, masharti magumu ya benki za utoaji mikopo, ukosefu wa wataalam wa masuala ya mifugo pamoja na kukosa wahisani na misaada ya wahisani kutokana na hali ngumu za kiuchumi za wanakikundi.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Chamaguha Deo Masalu alisema mradi huo utatumika kama shamba darasa na kuahidi serikali kuwapa ushirikiano wanachama wa kikundi ili kuhakikisha wanafikia malengo yao.


Mkurugenzi wa Kampuni ya Namaingo Business Agency Co. Ltd, Biubwa Ibrahim akijiandaa kukata utepe kwa ajili ya kuzindua mradi wa kuku unaosimamiwa na Kikundi cha Ujasiriamali kutoka Shinyanga, Kishapu na Kahama (SHIKIKA) Septemba 18, 2017. Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog 

Mkurugenzi wa Kampuni ya Namaingo Business Agency Co. Ltd, Biubwa Ibrahim akikata utepe.


Mkurugenzi wa Kampuni ya Namaingo Business Agency Co. Ltd,Biubwa Ibrahim akiangalia kuku wenye umri wa miezi miwili katika moja ya mabanda ya kundi la SHIKIKA.

Monday, September 18, 2017

Yajue 'Mapenzi Kaburini'....!


Tupokigwe Abnery Mwampondele amezaliwa,Seronera - Serengeti mkoani Mara. Alisomea shahada ya Isimu ya lugha ya Kiswahili Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM). 

Kwa sasa ni mwalimu wa somo la Kiswahili katika shule ya Sekondari ya Wasichana Precious blood iliyopo mkoani Arusha-Tanzania.

N’je na kazi ya uwalimu Tupokigwe Abnery ni mtunzi wa vitabu vya hadithi, mbunifu wa mavazi ya kiasili, mjasiriamali na mwandishi wa gazeti tando (blogger) inayoitwa Sinyati Blog.

Tupokigwe Abnery alikuwa na kawaida ya kupenda kujibembeleza au kujifariji akiwa anatembea kwa kutengeneza hadithi katika fikra zake ili kuweza kulala au kufika anakoelekea bila kuchoka, ndipo siku moja baada ya kushiriki shindano la uandishi wa Riwaya fupi kwa wanafunzi wa shule ya msingi, sekondari na vyuo vikuu Tanzania kwa ajili ya Tuzo ya mama Salma Kikwete iliyoandaliwa na TASAKI (Tamasha la Sauti ya Kiswahili) aliibuka mshindi wa pili wa riwaya fupi kwa wanafunzi wa vyuo vikuu Tanzania.

Hivyo hiki kitabu ni muendelezo wa Riwaya aliyopatia Tuzo. Soma kitabu hiki uweze kujionea ubunifu wa hali ya juu wa fani pamoja na mshikamano wa maudhui uliyopo ndani ya kitabu hiki.

Mapenzi Kaburini ni kitabu chenye mtazamo yakinifu, ni kitabu ambacho maudhui yake yamezitazama nchi za Afrika Mashariki na changamoto zilizopo katika nchi kwa upande wa viongozi pamoja na wananchi. 


Kimebeba maudhui yanayowalenga wananchi wote bila kujali utabaka.Kwa upande wa fani kimetumia majina ya halisi na kubuni hasa kwa upande wa maeneo ya miji mfano kuna miji kama Kinyonga, kupe, chatu ambayo ni majina yaliyopo katika nchi ya Simba. Nchi hii ya Simba ni nchi inayosimamia nchi zilizopo Afrika Mashariki.

Mbali na hilo pia visa na matukio vimepewa majina ya hifadhi za Taifa zilizopo katika nchi ya Tanzania.Mfano hifadhi ya Ruaha, Sanane, Manyara na kitulo kama ukisoma kitabu hiki utagundua kuwa sifa ya hifadhi inaendana na visa na matukio yaliyopo katika sehemu hiyo iliyoandikwa kwa jina la hifadhi.


Mfano hifadhi ya Kitulo inasifika kwa kuwa na maua,kama tujuavyo maua huashiria sifa nyingi moja wapo hapo ni upendo,watu wengi hutumia maua katika kuwapa wapenzi wao,mfano kuomba msamaha,kumfariji mtu,hata kuonesha upendo kwa mtu unayempenda.

Utakaposoma kitabu hiki utaburudika na kufundishwa baadhi ya mambo kama Kukuza imani yako kwa Mungu, uaminifu katika ndoa, uzalendo katika nchi yako na Madhara ya kujihusisha katika mahusiano na mtu usiye mjua.



Nitakupatia kionjo kidogo katika sura ya kwanza ili kuweza kuona mwanzo tu wa hadithi hii ambayo hutapenda kuacha kuifuatilia:


Sura ya kwanza
Hifadhi ya Sanane 


Ilikuwa siku ya Jumatatu katika ghorofa la tajiri mmoja, mmiliki wa hoteli maarufu katika nchi ya Simba. Tajiri huyo alifahamika sana kwa kuwa alikuwa akijitolea sana kwa wananchi wasiojiweza, katika miji mbalimbali ya nchi hiyo.Watu husemamfadhili punda kuliko mwanadamu vilevile tenda wema kisha nenda zako baraka utazipata kwa Mungu,usisubiri hisani za wanadamu.


Pamoja na misaada aliyoitoa kwa watu mbalimbali lakini wananchi wa Simba hawakujali misaada yake, walimteta kila kona kuwa anatumia nguvu za giza na amekwisha toa kafara ndugu, jamaa na hata watoto wake ili kujipatia utajiri mkubwa alionao. Siku hiyo ya Jumatatu katika pagala la tajiri huyo aliyefamika kwa jina la Pesa nyingi.
katika moja ya chumba cha ghorofa hilo kulikuwa na mwanamke mrembo na mzuri sana wa sura, mrefu mithili ya twiga, mwenye umbo zuri la kiafrika, chini alikuwa amevaa suruali ya chupa huku akiwa amevaa blauzi tatu juu zenye rangi tofauti na nywele timutimu zikiwa zime nakishiwa na vitu vya jaani kama vichana, visude, rasta chakavu na kufungwa kitambaa cha kitenge aina ya makenzi, uso wake ulikuwa kama paka mwenye madoa kutokana na kujipamba kwa majivu na masizi ya mkaa wa jaani. Pembeni ya ua hilo alikuwepo mnyama mwenye maringo

mbugani kuliko wote, sio mwingine bali ni kijana mtanashati aliyekwenda hewaani, rangi ya ngozi yake nyeusi ya kung’aa. Tabasamu la mwanaume huyo lililokuwa likimfariji mtoto mzuri, lili mvutia sana Savannah. Ghafla ilisikika sauti ya mwanamke huyo ikiita kwa sauti ya chini iliyojaaa simanzi na mateso ya muda mrefu,ilisema “John naumia mume wangu, hali yangu kila kukicha afadhali ya jana”.
John alijibu “usijali Savannah nipo hapa mke wangu kwa ajili yako utapona tu tutakwenda hospitali,subiri nikuandalie chakula ule, kisha nikupeleke hospitali malikia wangu”. Basi baada ya John kumfariji Savannah aliamka na kuelekea jikoni pembeni ya sehemu aliyokuwa amelala mpenzi wake. Watu hawa walipendana sana ni vile tu hali yao haikuwa nzuri kifedha waliishi kwa kuhangaika, kuomba msaada na wakati mwingine walifukuzwa na walimwengu pale walipokuwa wakiomba msaada, watu waliwapita kama mbwa waliokosa matunzo.
Wapenzi hao Walizoea maisha ya kuokota vyakula jalalani na kukimbilia magari ya taka sambamba na kusubiria mabaki ya chakula katika migahawa mbalimbali. Wakati huo John alikuwa akitimiza ahadi aliyo mhahidi malikia wake alimuandalia chakula walicho kiokota katika soko kuu la mji huo wa Chatu. John alimuinua Savannah pale alipokuwa amelala kwenye kanga chakavu akiwa amejifunika magunia yalionekana ni ya mpunga. John alimlisha Savannah chakula kile ambacho hawakujua kilipikwa lini na kutupwa na nani na lini. Savannah alisikika akisema “asante mume wangu hata

mwanangu anafurahi sasa naona napata nafuu, nahisi ni njaa ilikuwa inaniuma”. Mwanangu nisamehe mama kakushindisha njaa, nakupenda sana najua wewe utakuwa mrembo zaidi yangu mwanangu hata baba yako anakupenda”. John alikuwa anapenda sana utani alicheka na kusema “atakuwa mrembo kama wewe kweli mke wangu lakini rangi ya ngozi yake itakuwa kama yangu, yako iko kama ya nguruwe hahahaaaa!” Savannah alikuwa mweupe kama Nguruwe, ingawa alivyokuwa anaonekana ni kama mtu mwenye ngozi ya rangi ya maji ya kunde kutokana na ugumu wa maisha.
Wawili hao walifurahi pamoja na kusahau shida walizokuwa nazo.Walipomaliza kula wapenzi hao waliamua kutoka nje baada ya kukaa ndani ya paghala hilo kwa muda wa wiki moja, Dikidiki hao walikuwa na kaida ya kufanya hivyo wanapotafuta riziki na kujilimbikizia ndani ya paghala lao kisha wana kaa kwa muda huo bila kutoka. Usilolijua ni kama usiku wa kiza, basi Savannah na John walipotoka wakiwa n’je ya mgahawa mmoja uliokuwa unapendwa sana na wananchi wa mji huo wa Chatu zilisikika sauti za wanawake wakisema:
“haya jamani sasa ni ule wakati wa Pesa nyingi kuingiza hela sasa wenzi wametoka fungate”. Waliamini kuwa Pesa nyingi alikuwa anawatumia Dikidiki hao kama misukule inayotoka na kurudi ndani na wanapotoka basi mzee Pesa nyingi huingiza hela nyingi sana. Kwakuwa wenzi hao walikuwa hawaelewi kinachoongelewa waliendelea kuomba msaada kwa wateja waliokuwepo hapo mgahawani. Wanapokosa waliamua kucheza baadhi ya nyimbo zilizokuwa

zikipigwa katika mgahawa huo, wakicheza hupewa chakula na fedha ambazo hutoka katika mifuko ya wateja. John alikuwa anapenda sana kucheza,wakiwa wamekaa chini walisikia wimbo wa mwanamuziki maarufu Tanzania Diamond unaosema Je, Utanipendaga? John alimuinua Savannah aliyeonekana kachoka na mimba yake. 


Savannah aliamka na kucheza na mpenzi wake, walicheza kwa miondoko ya kihindi, machozi yalisafisha uso wa Savannah huku yakiosha kifua cha John kilichokuwa kimejaa kama mlima na mikono iliyokuwa na miinuko ya kupanda na kushuka ilizunguka juu ya kifua cha Savannah na kumfanya ahisi kazungukwa na jeshi kubwa la malaika wa ulinzi.

Baada ya kumaliza kucheza savannah alikuwa amechoka sana, kitendo cha kucheza kilimsababishia kuchokoza maumivu na kupelekea kupata uchungu katika kizazi chake. 


Baada ya kuona hivyo John aliinama na kuchukua zawadi walizozipata kutoka kwa hadhira iliyokuwa ikiwatazama huku baadhi ya hadhira wakibubujikwa na machozi walimpelekea hela na chakula John katika kapu lake la kukusanyia riziki. Watu waliokuwa wakiwatazama Savannah na John hawakujali maumivu ya mwanamke yule na kuona kawaida. 

Wapo waliosikika wakisema hawa vichaa wana akili, wengine walisema hawa si vichaa, vichaa gani wana akili ya kutafuta hela hivi, wamekusanya umati mkubwa hivi na kuwafanya watu kutoa kile walichonacho. Mama mmoja mwenye busara anayeuza katika mgahawa huo aliyefahamika kwa jina la mama ndaga akasema“Jamani mimi nawafahamu hawa vichaa kwanza hawakuwa wakitembea hivi pamoja kama Dikidiki, huyo kaka unayemuona alikuwa..........pata mwendelezo kwa kujipatia kitabu hiki.



Nicheki kwa mawasiliano haya:+255756377940
Instagram: @sinyatiblog
Facebook:Tupokigwe Abnery 


Au Blog yake : www.sinyatiblog.blospot.com 

Saturday, September 16, 2017

WATALII ZANZIBAR HAWAJAKAUKA....!



Na Jumia Travel Tanzania

Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio lukuki takribani kila sehemu utakayoipendelea. Mji Mkongwe uliopo visiwani Zanzibar ni mojawapo ya maeneo hayo yenye utajiri wa vivutio vya watalii kama vile maisha na vyakula vya wakazi wake, biashara pamoja na majengo ambayo yanayoakisi tamaduni za mataifa tofauti kama vile Waarabu, Waajemi, Wareno, Waafrika na Waingereza ambayo yamekuwepo tangu karne za 18 na 19.



Katika kuhakikisha maeneo hayo yanajulikana miongoni mwa watanzania na wageni wanaotembelea nchini, Jumia Travel wamezindua kampeni ambayo itakuwa ikiangazia maeneo mbalimbali. Ikiwa imejikita kwenye Mji Mkongwe wa Zanzibar, kampuni hii ambayo inajishughulisha na huduma za hoteli kwa njia ya mtandao ilifanya mahojiano na Meneja Operesheni wa Africa House Hotel, Bw. Justus Kisome na mazungumzo yalikuwa kama ifuatavyo.

JT: Unaizungumziaje hoteli yako?
Justus: Africa House Hotel ni hoteli ya nyota nne inayopatikana kwenye jengo la kihistoria linalomilikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar lililopo katika Mji Mkongwe wa Zanzibar. Hoteli yetu ina vyumba 15 vikiwa na hadhi tofauti kukidhi haja ya wateja mbalimbali wanaotembelea hapa. Miongoni mwa vyumba hivyo 6 vinatazamana na bahari ya Hindi ambavyo huwapatia wageni fursa ya kutazama tukio nadra na kuvutia la kuzama kwa jua. Vyumba 9 vinawapatia wateja mandhari nzuri ya Mji Mkongwe wa Zanzibar ambao umebarikiwa kuwa na majengo na tamaduni za kale kwa karne kadhaa sasa.

JT: Unadhani ni vitu gani vinaifanya hoteli yako kuwa ya kipekee?
Justus: Naweza kusema kwamba tunajivunia hoteli yetu kuwa ndiyo pekee yenye maktaba katika Mji Mkongwe huu wa Zanzibar ambapo wageni wanayo fursa ya kujisomea masuala mbalimbali. Lakini pia ukiachana na hilo, Africa House Hoteli ndiyo hoteli pekee yenye mgahawa unaopika vyakula vya Kichina katika Mji Mkongwe wa Zanzibar. Mgahawa huu tumeujenga hivi karibuni, hakuna hoteli yoyote hapa yenye huduma kama hii, mgahawa unaendelea vizuri kwani tunapata maombi ya huduma mpaka moja kwa moja kutoka nchini China.





JT: Je unafikiri wateja wako ni wa aina gani? Kutoka ndani au nje ya nchi?
Justus: Naweza kusema kwamba idadi kubwa ya wateja wetu ni mchanganyiko, wengi wakiwa ni kutoka nje ya hapa Mji Mkongwe. Kwa wageni wa hapa nyumbani wengi tunaowapokea hupendekezwa na serikali na kwa wenyeji pia huwaleta au kuwaelekeza wageni wao kuja hapa.

JT: Ni shughuli gani zinazopendelewa kufanywa au kuuliziwa zaidi na wateja pindi wanapotembelea hoteli yako?
Justus: Asilimia kubwa ya wageni tunaowapokea hapa huja kwa madhumuni ya kibiashara au kikazi sio kwa mapumziko. Kwa ujumla, kama zilivyo hoteli nyingi kwenye Mji Mkongwe, hufanya sehemu hii ni kama kituo na kisha kuendelea na safari zao. Hivyo basi, mara nyingi wageni wanaofika hapa hulala kwa siku moja au mbili na kisha kuendelea na safari zao kama vile kwenda sehemu za ufukweni, uwanja wa ndege au bandarini.

JT: Una maoni gani juu ya ukuaji wa utalii wa ndani? Je kuna mabadiliko yoyote uliyoyaona?
Justus: Ukuaji wa utalii wa ndani kwa hapa Mji Mkongwe ni mzuri kwani wageni huongezeka mara kwa mara kadiri siku zinavyokwenda. Ingawa hatupokea wageni wengi wazawa kwenye hoteli yetu lakini kuna idadi kubwa ambao huwaleta wageni wao hapa. Hata kama hawatembelei hapa lakini kuna maeneo mengi ambayo tunawaona watalii wazawa wakitembelea na kwenye mitaa ya Mji Mkongwe.



JT: Unaizungumziaje Zanzibar kama mojawapo ya sehemu inayopendelewa kutembelewa zaidi? Je unadhani umaarufu wake unaongezeka au kupundua kadiri miaka inavyozidi kwenda?
Justus: Zanzibar kama kitovu cha utalii bado ni imara na kinaedelea kukua kadiri siku zinavyozidi kwenda. Wateja ni wengi na wanaendelea kuongezeka. Kwa mfano, kuanzia mwezi wa Julai, Agosti na huu wa Septemba ni vipindi ambavyo huwa tunapokea wageni wachache lakini tofauti na kipindi cha nyuma wateja ni wengi na kuna baadhi ya hoteli zimejaza vyumba na zingine zikiwa zimebakisha vichache! Hii ni ishara na dalili nzuri kwamba hali ni shwari huku Zanzibar ambapo kwa kipindi kama hiki hapo awali hakukuwa na wageni wengi kama sasa.



JT: Unazungumziaje kuhusiana na tozo mbalimbali kwenye sekta ya utalii, ukiachana na 18% za VAT, je zinaathiri biashara yako?
Justus: Kwa upande wangu naweza kusema kwamba Zanzibar haijaathirika na hizo tozo mbalimbali na sidhani kama zimeathiri biashara yetu. Kwa mfano, tozo ambazo zinalipwa ni zilezile na wageni kutoka nje ambao wanakuja nchini kuja kutembelea vivutio mbalimbali zikiwemo kodi na viingilio. Kama kungekuwa na athari basi tungewasikia wageni wakilalamika lakini wanaridhika na kuelewa kuwa ni taratibu ambazo ziko kama sehemu nyingine ukizingatia ni vivutio ndivyo wamekuja kuviangalia na sanasana huwashawishi na wageni wengine kuja kutembelea Zanzibar.

JT: Una maoni gani juu ya shughuli za mitandaoni kwenye kukuza sekta ya utalii nchini Tanzania?
Justus: Ni kweli dunia imebadilika hususani kwenye namna biashara zinavyoendeshwa siku za hivi karibuni. Kama zilivyo sehemu zingine, Zanzibar nayo imeipokea teknolojia ya mtandaoni vizuri kwa sababu idadi kubwa ya wageni tunaowapokea tunawapata kwa njia ya mtandaoni. Na kitu kizuri ni kwamba wanaiamini mitandao hiyo katika kufanya huduma zao na sisi tunajiimarisha kila kukicha kwenye Nyanja hiyo.


JT: Kwa kuongezea, unauzungumziaje ushirikiano baina ya Jumia Travel na hoteli yako? Unadhani ni msaada katika uendeshaji wa biashara yako?
Justus: Mahusiano na ushirikiano wetu na Jumia Travel ni mazuri kwani wanatusaidia kwa kiasi kikubwa kwenye uendeshaji wa shughuli zetu. Jumia Travel inakuja vizuri na inakua kwa sasa kwani mchango wake kwenye uendeshaji wa shughuli zetu ni mkubwa kutokana na wao kuwepo kwenye soko. Ukilinganisha na mwanzo ambapo kulikuwa na changamoto kadhaa kama vile kutokuwepo na mawasiliano ya kutosha pale kunapokuwepo na matatizo. Hivi sasa wanatutembelea na kuwasiliana mara kwa mara kujua tunafanyaje shughuli zetu. Naweza kusema wanastahili pongezi kwa hilo na naamini timu ya sasa iliyopo inafanya kazi vema na inajitambua zaidi.

Marehemu Sister Jean Pruitt kuagwa Jumatano Dar

Ndugu, jamaa, marafiki na wadau wa sanaa na haki za watoto Tanzania.


Kamati ya Maandalizi ya Msiba inapenda kutoa Tangazo rasmi la shughuli ya kuaga na kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa mpendwa wetu marehemu Sister Jean Pruitt itakayofanyika siku ya Jumatano tarehe 20/09/2017.



Shughuli hii itafanyika katika Ukumbi wa Karimjee uliopo Posta, Mtaa wa Sokoine, mkabala jijini Dar es salaam. Wadau wote tunaombwa kuwasili mapema kwa ajili ya kutoa

heshima zetu za mwisho na kuaga mwili saa 3:30 asubuhi siku hiyo.


Baada ya hapo Mwili utasindikizwa kwenda kanisa la Mt. Joseph kwa ajili ya misa itakayoanza saa 9 Alasiri siku hiyo ya Jumatano.


Tunawaomba tuzidi kumwombea mama yetu Sista Jean Pruitt apumzike kwa Amani. Raha ya milele umpe eh Bwana na mwanga wa milele umwangazie,
apumzike kwa Amani - Amina

Kamati ya Maandalizi ya Msiba


NORDIC yamtangaza Zembwela kuwa balozi wa AfyaBando


Afisa TEHAMA wa Taasisi ya NORDIC, Dickson Leonard akiongea na wanahabari kumtambulisha Hilary Daudi ‘Zembwela’ kuwa Balozi wa Nordic Foundation Tanzania Dar es Salaam Septemba 15 2017. Balozi Zembwela atafanya kampeni ijulikanayo kama ‘AfyaBando’. Kushoto ni Mtaalam Mwelekezi wa Afyabando-Nordic Foundation TanzaniaDkt. Resipicius Salvatory. 

Balozi Zembwela akionesha namba ya kampuni na kumbukumbu kwa ajili ya kushiriki bahati nasibu ya kucheza 'Afyabando' ili kupata kadi ya Bima ya afya kwa shilingi 500. 

Clouds Media Group Washinda Tuzo ya Marehemu Daudi Mwangosi


Mkurugenzi wa Tanzania Media Foundation,Ernest Sungura akikabidhi tuzo Tuzo ya Uandishi wa Kishujaa na Ulitukuka ya Daudi Mwangosi mwaka 2017 kwa  Afisa Mahusiano kutoka Clouds Media Group Simalenga Simon leo Jumamosi Septemba 16,2017 mkoani Tanga.

JOPO la Majaji Tuzo ya Uandishi wa Kishujaa na Ulitukuka ya Daudi Mwangosi mwaka 2017 limeitangaza Clouds Media Group kuwa mshindi wa Tuzo hiyo kwa mwaka 2017. 
Tuzo hiyo imetolewa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari nchini UTPC wakati wa mkutano wake mkuu wa unaofanyika katika ukumbi wa Tanga Beach Resort mkoani Tanga. 
Tuzo hiyo imekabidhiwa  kwa uongozi wa Clouds Media Group na Mkurugenzi wa Tanzania Media Foundation,Ernest Sungura. 
Mbali na kupewa tuzo hiyo,pia Clouds fm imekabidhiwa hundi ya shilingi milioni 10 kama pole kwa changamoto waliyopitia baada ya kituo cha matangazo kuvamiwa na mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda aliyekuwa ameambatana na askari polisi. 
Mwenyekiti wa Jopo la Majaji Tuzo ya Uandishi wa Kishujaa na Ulitukuka ya Daudi Mwangosi mwaka 2017,Jenerali Ulimwengu alisema madhumuni ya tuzo ya mwangosi ni kumuenzi na kumkumbuka kwa kumpa mwanahabari au chombo cha habari tuzo yenye jina lake. 
“Jopo la majaji mwaka huu tunaitangaza Clouds Fm kuwa mshindi wa tuzo ya Daudi Mwangosi mwaka 2017 kwa sababu tarehe 17,Machi,2017 wanahabari wa Clouds walivamiwa na mkuu wa mkoa wa Dar es salaam akiwa na askari polisi akiwataka kutangaza habari ambayo hawakuitaka lakini wafanyakazi hao wakakataa kutangaza habari hiyo,huu ni ushujaa kwani hawakukubali kutii amri ambazo zilikuwa kinyume na kazi waliyofundishwa na uandishi wa habari”,alisema Ulimwengu. 
“Lengo la tuzo hii iliyoanzishwa mwaka 2013 na UTPC ni kupinga vitendo viovu wanavyofanyiwa waandishi wa habari , hutolewa kwa mwandishi wa habari anayefanya kazi nchini aliyekutana na madhila katika utendaji kazi wake ama chombo cha habari ambacho kimekutana na madhila”,alieleza Ulimwengu. 
Aliongeza kuwa tuzo hiyo inalenga kuwafanya wadau wa habari ikiwemo serikali kutambua kazi ya waandishi wa habari. 
“Daudi Mwangosi alikuwa mwenyekiti Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Iringa,aliuawa Tarehe 2 mwaka 2012 katika kijiji cha Nyololo mkoani humo,akitekeleza majukumu yake,ni mwandishi wa habari wa kwanza nchini Tanzania kuuawa akiwa kazini, kifo chake kilishtua na kusikitisha watu wengi duniani”,alieleza.

Mkurugenzi wa Tanzania Media Foundation, Ernest Sungura akikabidhi tuzo Tuzo ya Uandishi wa Kishujaa na Ulitukuka ya Daudi Mwangosi mwaka 2017 kwa Afisa Mahusiano kutoka Clouds Media Group Simalenga Simon.


Mkurugenzi wa Tanzania Media Foundation, Ernest Sungura cheti cha ushindi kwa Afisa Mahusiano kutoka Clouds Media Group Simalenga Simon.


Mkurugenzi wa Tanzania Media Foundation, Ernest Sungura akikabidhi hundi ya shilingi milioni 10 kwa Afisa Mahusiano kutoka Clouds Media Group Simalenga Simon. 

SEIF SHARIFF HAMAD AKIRI KUWA YEYE NI BABU KIZEE.

Seif Shariff Hamad Seif Shariff Hamad KWA mara ya kwanza Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Seif Shariff Hamad amek...